Ticker

7/recent/ticker-posts

MZEE CHAI: UHARIBIFU WA MAZINGIRA UMEKIMBIZA MVUA

 

Mzee Ramadhani Kihiyo Chai akielezea namna misitu iliyokuwa ikiwasaidia kupata mvua za uhakika kabla ya kuharibiwa kwa Mazingira.

NA JIMMY KIANGO-ALIYEKUWA MUHEZA

 

Tanzania ni moja ya nchi zilizobarikiwa ardhi yenye rutuba na eneo kubwa la misitu iliyokuwa ikizalisha uhakika wa mvua.

 

Hata hivyo hali sasa ni tofauti, mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababishwa na shughuli za kibinadamu zimesababisha kutoweka kwa uhakika wa upatikanaji wa mvua katika vipindi muhimu.

 

Kimsingi Tanzania inavyo vipindi viwili vya mvua kwa mwaka ambavyo hutanguliwa na kipindi cha joto linaloanza Desemba na kufikia kikomo Februari.

 

Kipindi cha kwanza cha mvua ni zile za Masika ambazo huanza kunyesha mwezi Machi na kutamatika Mei.

 

Mvua za Masika ndio zinatajwa kuwa mvua zinazonyesha kwa muda mrefu nchini Tanzania zikifuatiwa na mvua za Vuli ambazo zenyewe zinaanza mwezi Oktoba na kutamatika Desemba.

 

Vipindi hivi vya mvua vinaweza kutofautiana kidogo kulingana na maeneo mbalimbali ya nchi hasa kati ya Pwani na nyanda za juu.

 

Ngoma na pembe ni zana zilizotumiwa na Mzee Chai kukusanya watu sehemu moja kwa jailli ya kuzungumza macula mbalimbali yanayohusu kijiji cha Kazita. 

Hata hivyo hali sasa imekuwa ni tofauti, uhakika wa mvua katika miezi ya Machi, Aprili, Mei,Oktoba, Novemba na Desemba haupo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

 

Ukweli wa hili inathibitishwa na Mzee Ramadhani Kihiyo Chai ambae ni mkazi wa Kijiji cha Kazita, kilichomo katika Tarafa ya Amani, wilayani Muheza mkoani Tanga.

 

Mzee Chai anaefahamika kama mzee wa Mtambiko kijijini hapo kwa sasa ana umri wa miaka 102, lakini bado anaona vizuri, ingawa anatembea kwa mkongoji, lakini miguu yake bado iko imara, anapandisha na kushusha vilima vilivyopo Kijiji hapo.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kazita William Hiza.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kazita William Hizza, anasema kuwa Mzee Chai ni mmoja ya wazee wachache waliobaki kwenye mjini wa Amani ambao wanaweza kuyazungumzia mazingira kwa upana zaidi kwani yeye ndie aliyepewa jukumu la kuitumia baadhi ya misitu kwa ajili ya tambiko.

 

Timu ya waandishi wa Habari za Mazingira wakiongozwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) chini ya Mkurugenzi wake John Chikomo ikiwa katika mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na USAID, ilifika katikati ya Kijiji cha Kazıta.

 

Lengo la ziara hiyo pamoja na mambo mengine ni ufuatiliaji wa namna wananchi wanavyoulinda ushoroba wa Amani-Nilo, pia kuzungumza nao juu ya wanavyonufaika na kilimo hai, pamoja na kuwapa uelewa wa utunzaji wa Maliasili.

Mwandishi wa Afrinewsswahili Jimmy Kiango (kulia) akiwa na Mzee Chai, kijijini Kazita.

 
Katika mazungumzo na Mzee Chai, ambae anamiliki ngoma na pembe maalum vilivyokuwa vikitumika kukusanya watu kwa ajili ya kupeana taarifa za Kijiji na matambiko mbalimbali, akisaidiwa na Mzee Hiza ameeleza mambo kadhaa likiwemo la uharibifu wa mazingira ulivyokimbiza mvua katika eneo lao.

 

“Zamani kabla ya ujio wa kiwanda cha kuchakata magogo cha Sikh saw Mills cha Tanga, tulikuwa na misitu mikubwa iliyosheheni miti minene na mirefu.

 

“Hii ilikuwa ikitusaidia kupata mvua za uhakika kila mwaka, hatukuwa na kilio cha ukame wa aina yeyote, tofauti na sas, hali imekuwa mbaya, mvua zimekuwa ni za kuviziavizia.

 

“Sisi tulikuwa tunaweza kuiita mvua wakati wowote na inakuja, lakini sasa hali ni kama imekuwa tofauti, hawa watu wa kukata mbao walituharibia misitu yetu hadi pale walipokuja kupigwa marufuku.”alisema Mzee Chai.

Mzee Chai aliongeza kuwa kama hakutafanyika jitihada za makusudi za kuilinda misitu iliyobaki, upo uwezekano wa kukaribisha ukame zaidi.

 

“Kuna haja ya kuitunza mizitu yetu ili kujihakikishia mvua kwa nyakati zote stahiki, vinginevyo hali itakuwa mbaya zaidi,”alisema.

Mzee Chai akita katika matembezi yake kijijini Kazita.

Misitu ya asili ya Amani, iliyopo wilayani Muheza mkoani Tanga, ilianza kutunzwa rasmi mwaka 1997. 

Hii ilikuwa baada ya kutambuliwa kuwa ni eneo muhimu kwa bioanuwai, likiwa na aina nyingi za mimea na wanyama, ikiwa ni pamoja na spishi adimu za viumbe wanaopatikana tu katika maeneo hayo ya milima ya Usambara. 

 

Misitu hiyo ni sehemu ya hifadhi ya Milima ya Usambara ambayo ina umuhimu mkubwa wa ikolojia nchini Tanzania na duniani.

 Hifadhi ya Usambara ni maarufu kwa aina nyingi za mimea na wanyama, ikiwa ni pamoja na baadhi ya spishi ambazo hazipatikani mahali pengine duniani. 

 

Misitu ya milima hii inajulikana kwa kuwa na aina adimu za miti, maua, ndege, na viumbe wengine kama vile amfibia na wanyama wadogo wa ardhini. 

Mimea ya kipekee kama mti wa mkangazi na miti ya aina ya camphor hupatikana katika maeneo haya.

Post a Comment

0 Comments