Mchezaji wa Azam FC Feisal Salim |
Feisal Salim 'Fei Toto' mchezaji wa zamani wa Yanga ni kama vile alikuwa akiisubiri nafasi maalum ya kuwaomba msamaha mabosi wake wa zamani ndani ya 'pitch'.
Hatimae nafasi akaipata jana Machi 17,2024 katika siku ambayo imelirejesha taifa miaka mitatu nyuma, ambapo tarehe kama hiyo mwaka 2021 nchi iliingia kwenye simanzi baada ya kutangaziwa kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kufariki dunia.
Ni wazi Feisal aliitamani hiyo nafasi na matamanio yake yalimfanya kucheza kwa kujituma na nguvu kubwa katika dakika zote za mchezo. Kila mpira ulioelekezwa kwake ulikuwa na madhara mbele ya wapinzani wao Yanga.
Katika kipindi cha kwanza wakati Yanga ikiongoza bao 1-0 ni Feisal ndie aliyechagiza na kuzalisha pasi iliyokwenda kusababisha goli la kusawazisha. Muunganiko wa Feisal na Kipre Junior uliwasahaulisha kabisa mashabiki wa Azam juu ya mwana mfalme Dube (Prince Dube) ambae amejiondoa kwenye kikosi cha wana lambamba kwa nyodo.
Wakati mashabiki wakiamini mechi huenda ikawa ya mafanikio kwa Yanga kutokana na namna walivyokuwa wakilisakama lango la Azam, Feisal alizima fikra hizo katika dakika ya 51. Na hapo ndipo alipoiona haja ya kuitumia nafasi hiyo kuwaomba msamaha Yanga kwa kufunga mikono ikiwa ni ishara ambayo watu wengi wanaitumia kama alama ya unyenyekevu.
Azam ilipata ushindi huo ikitokea nyuma baada ya kufungwa katika dakika ya 10 na mshambuliaji mzawa, Clement Francis Mzize.
Winga Mgambia, Gibrill Sillah aliisawazishia Azam katika dakika ya 19 na Fei toto aliizamisha Yanga katika dakika ya 51.
Kwa ushindi huo, Azam FC imefikisha pointi 47 katika mchezo wa 21 na inasalia katika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tano na Yanga ambayo pia ina mechi moja mkononi huku Simba ikiwa na pointi 45 ikiwa imecheza mechi 19.
0 Comments