Ticker

7/recent/ticker-posts

FARU MWEUSI,MBWA MWITU HATARINI KUTOWEKA TANZANIA

Kamishna wa Uhifadhi -TAWA, Mabula Nyanda.

NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-BAGAMOYO


Dunia isiposhiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali zilizopo sasa, uko uwezekano mkubwa wa wanyama na viumbe pori vingi kutoweka kama ilivyo kwa mnyama dynasol.

 

Miongoni mwa wanyama walio hatarini kutoweka Tanzania na pengine duniani kwa ujumla ni faru mweusi. Ikumbukwe kuwa duniani kuna aina tano za faru. Kwa Afrika kuna aina mbili za faru, weupe na weusi na Tanzania inayo aina moja tu ya faru, ambaye ni mweusi.

 

Aidha faru mweusi nae amegawanyika katika spishi nne na kati ya hizo, mbili ndio zinapatikana Tanzania ambazo ni Diceros na Bicornis Michael.

 

Faru weusi wanatofautiana na wengine kwa sababu wao wana manyoya yanayoota kwenye kingo za masikio, hata ngozi yao ya pembeni mwa tumbo huonekana michirizi ambayo huwa kama mbavu za mnyama.

 

Bahati mbaya bila kujali spishi iliyopo, ukweli ni kwamba faru mweusi anatajwa kuwa mbioni kutoweka, ingawa kumekuwa na jitihada kadha wa kadha za kuwalinda.

 

Juhudi zinazoendelea za uhifadhi barani Afrika zimesaidia kuongeza idadi ya faru weusi kutoka kiwango cha chini cha kihistoria cha miaka 20 iliyopita ambacho kilikuwa chini ya Faru 4000 hadi zaidi ya 6,000 kwa sasa.

 

Afisa Uhifadhi Kitengo cha Uchunguzi, kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Tryphone Kanoni amewathibitishia Waandishi wa Habari za Mazingira walio chini ya Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kuwa ni kweli faru mweusi yuko hatarini kutoweka.

 

Kanoni ameyasema hayo Machi 14, 2024 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa semina maalumu kwa waandishi wa Habari za Mazingira iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la USAID.

 

Amesema wamegundua faru weusi wako hatarini kutoweka nchini na ili kuwanusuru na hilo, wameamua kuwaongezea ulinzi.

 

“Faru weusi na hata wale weupe wote wameorodheshwa kama viumbe walio hatarini kutoweka, kwa kulitambua hilo serikali imeweka jitihada za makusudi za kuwalinda kila wanapokuwa.

 

Afisa Uhifadhi Kitengo cha Uchunguzi, kutoka TAWA, Tryphone Kanoni. 

“Tumeelekeza nguvu katika kumlinda faru kwa kuwa ni mnyama aliye hatarini kutoweka, hii imetufanya tumlinde kwelikweli, popote atakapokuwepo, nasi tupo. Ulinzi wake ni mkubwa na unaonyesha mafanikio, lakini pia ni jukumu la Watanzania wote kuhakikisha tunashiriki kumlinda mnyama huyu, watu wanaokaa pembezoni mwa Hifadhi wakatae kutumiwa na majangili kuua faru weusi” alisema.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF), Tanzania imepoteza takribani asilimia 98 ya Faru weusi.

 

Katika kuinasua nchi na kukosekana kwa faru weusi, mwaka 2019 serikali ilizindua mpango wa taifa wa miaka mitano (2019 - 2023) wa usimamizi na uhifadhi wa faru weusi Tanzania.

 

Mpango huo pamoja na mambo mengine ulibeba mikakati ya kuhakikisha faru weusi wanaongezeka walau kufikia 205 ifikapo mwaka 2023 na katika kuliharakisha hilo Serikali ya Tanzania mwaka huo huo ilipokea faru weusi tisa kati ya 10 waliotakiwa kuletwa nchini wakitokea nchini Afrika Kusini.

 

Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru akishauriana jambo na Mkurugenzi wa JET, John Chikomo.


Tukio hilo lilikuwa la kihistoria kwa kuwa ilikuwa ndio mara ya kwanza kupokea idadi kubwa ya faru kwa wakati mmoja, faru hao walipelekwa kwenye hifadhi mbalimbali nchini.

 

Serikali iliahidi kuwalinda faru hao  kwa gharama yoyote na kuhakikisha hawapungui kama ilivyotokea kwenye miaka ya 1970-1980 na serikali  iliagiza faru hao wafungiwe vifaa maalumu vitakavyobaini mienendo yao popote watakapokuwa.

 

Changamoto ya ujangili ndio sababu kubwa inayosababisha kupungua kwa faru na kutishia hata kutoweka kabisa na kubaki historia.

Shirika la kimataifa la muungano wa uhifadhi duniani pia limeorodhesha faru weusi kuwa miongoni mwa wanyama walio hatarini kutoweka.

 

Faru ni miongoni mwa Wanyamapori wanaolindwa na Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.

 

Wataalamu wa masuala ya uhifadhi wanaitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi chache Afrika zenye makazi ya faru weusi hali iliyosaidia kuongeza idadi ya faru.

 

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia darasa la uandishi wa tija wa masuala ya uhifadhi.


Akiongea na AFRINEWS SWAHILI, Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Nyanda amesema mazingira rafiki yaliyopo kwenye Hifadhi mbalimbali nchini yamesaidia kuongeza uzao wa wanyama hao walio hatarini kutoweka. 

 

Hata hivyo Kamishna Nyanda ameweka wazi kuwa pamoja na kuwapo kwa ongezeko la wanyama hao nchini, bado wako kwenye tishio la kutoweka na ili kuwanusuru kasi ya kuwalinda inapaswa kuongezwa.

 

“Faru wako kwenye hatari ya kutoweka, hili halina ubishi, katika kukabiliana na hilo tumeongeza ulinzi was aa 24 kwa myama huyu, tunamfuatilia popote alipo, hata hivyo ili faru aendelee kuwepo ni lazima wote tushiriki kumlinda,”alisema Kamishna Nyanda.

 

MBWA MWITU

Kanoni pamoja na kumzungumzia faru mweuzi kuwa hatarini kutoweka, pia amesema Mbwa mwitu nao wanaingia kwenye kundi hilo kwani kwa sasa wanauliwa sana na jamii ya wafugaji.

 

Anasema kuna uadui mkubwa kati ya wafugaji na Mbwa mwitu kwa sababu, wanyama hao wana tabia ya kuvamia Mazizi na kushambulia mifugo. Hatua hiyo inawasukuma wafugaji kuua Mbwa mwitu popote wanapokutana nao, lengo likiwa ni kupunguza hatari ya mifugo yao kushambuliwa.

 

 

 


Post a Comment

0 Comments