Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi, Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-BAGAMOYO |
“Mmeshawahi kusikia stori za watu waliokuwa wanaishi Mwadui, miaka ya nyuma jinsi walivyokuwa wakichezea Almasi kama mawe ya kuchezea bao.
“Naamini wengi wetu tuliposikia Habari hizo, tuliwacheka hao babu na bibi zetu, na pengine tuliwaona hawakuwa na maarifa, kwa sababu walichezea mali. Basi na sisi tujiandae, tutakuja kuchekwa na kudharauliwa na vizazi vijavyo kwa sababu sasa tunachezea mali,”alisema Dkt. Elikana Kalumanga ambae ni Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi, Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
Dkt. Kalumanga amesema hayo Machi 15,2023 Bagamoyo, mkoani Pwani kwenye semina iliyolenga kuwanoa Waandishi wa Habari za Mazingira juu ya uandishi wenye tija unaohusu masuala ya uhifadhi.
Waandishi hao walikutanishwa kwa pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani -USAID.
Dkt. Kalumanga ameweka wazi kuwa kwa sasa watu wanachezea maliasili tulizo nazo hasa wanyama pori, hatujali kama wanaweza kutoweka, hatushiriki kuwatunza, badala yake tunakuwa mstari wa mbele kuwamaliza, hali hii itakakuja kuwa na matokeo mabaya katika miaka ijayo na njia pekee ya kuepukana na hilo ni watanzania wote kushiriki katika kulinda hifadhi zetu.
Dkt. Kalumanga akieleza umuhimu wa jamii kushirikishwa kwenye masuala ya uhifadhi wa Wanyamapori mbele ya waandishi wa Habari za mazingira.
Amesema ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori ni muhimu na utasaidia kulinda wanyamapori na kwakuliona hilo wao tayari wameshaanza kushirikisha jamii na matokeo chanya yameanza kuonekana.
“Utaratibu wa kushirikisha jamii inayozunguka hifadhi unapaswa kupewa kipaumbele, na namna pekee ya kulifanikisha hili ni kutumia miradi ya kuelimisha jamii, katika miradi tuliyoifanya kwa kushirikiana na jamii tayari wameanza kuona faida inayopatikana kutokana na kuishi kwao pembezoni mwa hifadhi na wananufaika moja kwa moja na fursa mbalimbali zinazohusu ulinzi wa hifadhi.
“Sisi kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili tumeona fursa kama vile biashara, uhifadhi, kilimo, ufugaji wa nyuki na hata jamii husika sasa inaaminika katika taasisi za kifedha, jambo ambalo awali halikuwepo,” amesema.
Dkt. Kalumanga amesema maeneo ya hifadhi yana faida katika kulinda vyanzo vya maji ambayo yanatumika kwa jamii yote, hivyo hakuna njia mbadala katika hilo tofauti na kuhakikisha kasi ya kuhifadhi mazingira inaongezeka.
“Uhifadhi una faida nyingi ikiwemo kuongeza viumbepori, maji, hali ya hewa nzuri na mengine, hivyo hakuna namna ambayo unaweza kufanya uhifadhi uwe endelevu bila kushirikisha wadau wote zikiwemo sekta binafsi,” amesema.
Baadhi ya Waandishi wa Habari za Mazingira, waliohudhuria mafunzo ya uandishi wa Habari za Uhifadhi zenye tija.
USHIRIKI WA JAMII
Sera ya Wanyama pori sehemu ya 3.0 kifungu cha 3.1 ( c)(e )(h) na (i) zinatambua umuhimu wa kuhamashisha ushiriki wa jamii za vijijini katika shughuli za kuhifadhi wanyamapori ndani na nje ya mtandao wa maeneo yaliyohifadhiwa (Pas) pamoja ma kuoanisha uhifadhi wanyamapori na maendeleo vijijini.
Pia katika mambo ya kukabili, sera inasisitiza kutia nguvu utambuzi wa thamani na faida ya kudumu ambayo jamii za vijijini zinaweza kupata kutokana na shughuli za wanyamapori pamoja na kupunguza kila inapowezekana migongano baina ya wat una wanyamapori.
Aidha sera inazitambua Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) kama makundi maalum yenye jukumu la kulinda hifadhi. WMAs kimsingi zina miongoni mwa majukumu yake ni kuendeleza urithi wa wanyama wa porini na kuwa sehemu ya kutoa huduma nje ya hifadhi kwa wageni wanaotembelea hifadhi hatua ambayo inawaingizia vipato vya moja kwa moja.
Kwa muktadha huu ni wazi suala la ushiriki wa jamii katika kulinda na kuhifadhi wanyamapori si suala la hisani badala yake linapaswa kutekelezwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ili kulinda maliasili za nchi. Jamii inayoshiriki moja kwa moja kwenye uhifadhi inapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kushiriki kwenye ujangili na matendo mengine yanayoweza kuhatarisha uhai wa wanyamapori na ekolojia
0 Comments