Ticker

7/recent/ticker-posts

'UJANGILI NA BIASHARA HARAMU YA MENO YA TEMBO IMEKWISHA TANZANIA'

 



Afisa Uhifadhi Kitengo cha Uchunguzi, Tryphone Kanoni,akitoa maelezo ya masuala ya uhifadhi kwa Waandishi wa Habari za Mazingira walio chini ya mwamvuli wa JET.

NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI- BAGAMOYO

Tanzania kwa sasa inatajwa kufanikiwa kukomesha kabisa ujangili sanjari na biashara haramu ya meno ya tembo, tofauti na ilivyokuwa miaka 12 iliyopita.

 

Mwaka 2012 takwimu za Taasisi ya Kimataifa ya Kupambana na Ujangili (Pocs) zilionesha kuwa tangu mwaka 2007 mpaka 2010, Tanzania ilikuwa ni kitovu cha biashara hiyo huku tembo 31,000 wakiuawa katika kipindi cha miaka hiyo mitatu.

 

Katika kipindi hicho haikuwa ajabu kupata taarifa za mauaji ya tembo kila siku hasa katika hifadhi ya Selous ambayo imetandawaa kwenye mikoa ya Lindi, Pwani, Morogoro na Ruvuma. Ilikuwa ni rashisi kwa watu kupata meno ya tembo zaidi ya 200, ndani ya muda mfupi, moja ya matukio makubwa  yaliyowahi kuripotiwa katika kipindi hicho cha mwaka 2012 ni jeshi la polisi kukamata meno 212 yaliyokuwa na uzito wa Kilogram 450.

 

HALI SASA NI SHWARI

Hali sasa ni tofauti, ripoti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), ya hivi karibuni imeonesha kuwa mauaji ya tembo yamepungua kutoka matukio 18 mwaka 2016 hadi matukio matatu mwaka 2023.

 

Kwa mujibu wa wasilisho la TAWA lililowasilishwa Machi 14, 2024 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na Afisa Uhifadhi Kitengo cha Uchunguzi, Tryphone Kanoni wakati wa semina maalumu kwa waandishi wa Habari za Mazingira iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la USAID, hali sasa ni nzuri.

“Kwa sasa biashara ya meno ya tembo nchini kwetu imekwisha, hata matukio ya ujangili wa tembo ni kama vile umekwisha, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma,”alisema Kanoni.

Hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarishwa kwa ulinzi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika mambo ya uhifadhi.

Kupungua kwa mizoga ya tembo iliyouawa na majangili kwenye maeneo mengi ya hifadhi nchini ndio kumeifanya TAWA kuamini kuwa sasa hali ni shwari.Hata hivyo kupungua kwa ujangili dhidi ya tembo hakuifanyi TAWA kubweteka badala yake imekuwa ikiongeza kasi ya ulinzi na kutumia teknolojia mbalimbali za kisasa kulingana na nyakati.

Jitihada zao hizo zimefanikisha kuendelea kukamata watu waliohifadhi meno ya tembo,operesheni za TAWA zimeweza kukamata washukiwa wa mauaji ya tembo 3,700 mwaka 2023, ukilinganisha na 4,800 waliotiwa nguvuni  mwaka 2016.

Kanoni, anasema meno ya tembo yanayokamatwa kwa sasa mengi ni ya miaka ya nyuma, na mapya yamekuwa nadra kuonekana, jambo ambalo linaonyesha kwamba mapambano dhidi ya ujangili yanazaa matunda.

 “Tumedhibiti mauaji mapya ya tembo kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana huwezi kuona meno mapya ya tembo, haya yanayoendelea kukamatwa mengi ni ya miaka ya nyuma.”

 

Kanoni akitoa ufafanuzi zaidi wa kupungua kabusa kwa biashara ya meno ya tembo Tanzania.

Katika kuhakikisha wahalifu wote bila kujali wanatoka nchi gani wanakamatwa mwaka 2019, Tanzania ilimtia hatiani Yang Feng Glan, mfanyabiashara kutoka China kwa makosa ya usafirishaji wa meno ya tembo 860 yaliyovunwa kati ya mwaka 2000 hadi 2014.

Aidha Aprili 12, 2022 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alikamatwa mtuhumiwa mmoja raia wa China akiwa na bangili moja na kidani ambavyo zilitambuliwa kuwa zimetengenezwa kwa meno ya tembo. Mtuhumiwa huyo aliingia nchini Aprili 10 na siku mbili baadaye, alikuwa anaondoka kuelekea Bankok, Thailand. 

SHERIA

Sheria namba 3 ya mwaka 2016 inayohusu makosa ya wanyamapori nayo imeonekana kuwa msaada katika mapambano dhidi ya ujangili kwani imesaidia kuongeza kiwango cha adhabu ambapo sasa mtu atakaetiwa hatiani kwa ujangili atakwenda jela kwa kati ya miaka 20 kifungo cha chini au miaka 30 kifungo cha juu cha adhabu au mahakama kutoa adhabu ya mtu kulipa faini mara 10 zaidi ya thamani ya nyara ya serikali aliyokutwa nayo, tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo mtuhumiwa alikuwa akitiwa hatiani hupewa adhabu ya kifungo kisichozidi miaka 15 jela, licha ya makosa hayo kuwa kwenye kundi la uhujumu uchumi.

Adhabu ya awali ilikuwa inatoa nafasi kwa Mahakama kuamua kiwango cha muda wa adhabu, ambapo uhuru wa sheria ulikuwa unatoa nafasi kwa Hakimu au Jaji kumuhukumu mtuhumiwa hata kifungo cha mwezi mmoja, tofauti na sasa, ambapo kiwango cha adhabu kinapaswa kuanzia miaka 20.

WIMBI LA UJANGILI 2009-2014

Wimbi la ujangili na usafirishaji haramu wa meno ya tembo ulishika kasi barani Afrika kati ya mwaka 2009-2014, na kusababisha kupungua kwa tembo wa Afrika, hali hiyo inaelezwa kuwa ilichangia upungufu wa zaidi ya nusu ya idadi ya tembo nchini Tanzania. Hatua hiyo ya kupungua kwa mauji ya tembo imesaidia kuongezeka kwa idadi ya tembo kwenye hifadhi mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo

Waziri ya Maliasili na Utalii, Angella Kairuki ameliambia AFRINEWSSWAHILI kuwa idadi ya tembo imeendelea kuongezeka kutokana na udhibiti na kupungua kwa mated ya ujangili. Kwa mujibu wa takwimu za serikali zilizotolewa Juni 2015, idadi ya tembo nchini ilipungua kutoka 109,051 mwaka 2009 hadi kufikia 43,330 mwaka 2014. Hali sasa ni tofauti, idadi imeongezeka, hadi kufikia mwaka 2019 wameongezeka na kufikia tembo  60,000.

Post a Comment

0 Comments