Mkulima akipulizia viuatilifu kwenye mimea
NA MWANDISHI WETU-AFRINEWS SWAHILI DSM
Viuatilifu visivyo na ubora stahiki vimetajwa kuwa moja ya vyanzo vinavyochangia ugonjwa wa Saratani pamoja na utindio wa ubungo.
Wataalamu wa afya wamebaini kuwa kundi lililo kwenye hatari kubwa ya kuathiriwa na viatilifu visivyo na ubora vinavyoingizwa nchini kwa njia za magendo ni Wanawake na Watoto.
Mhadhiri Mwandamizi mstaafu wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dkt. Vera Ngowi, ndiye ameyasema hayo leo Machi 6, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Kutathmini shughuli zilizofanywa na Mtandao wa Asasi zisizokuwa za kiserikali Tanzania katika kuondoa viuatilifu chakavu barani Afrika iliyoandaliwa na Asasi ya AGENDA kwa kushirikiana na TAPOHE.
Dkt. Ngowi amesema wanawake na watoto wako katika hatari kubwa ya kupata madhara ya kiafya yanayotokana na viutilifu na kwamba tafiti mbalimbali zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika nchini zimeonesha hivyo.
“Mara nyingi wanawake wanajiona kwamba wao ni salama kwa kuwa tu hawabebi mabomba kwenda kupulizia viuatilifu shambani au majumbani, lakini tafiti ambazo zimefanyika katika nchi mbalimbali ikiwamo hapa Tanzania tumeona kwamba wanawake wanaathirika zaidi na viuatilifu hivi kuliko wanaume wanaobeba mabomba kwenda kupulizia mazao.
“Hii ni kwasababu wanaume wanakuwa wamechukua tahadhari kwa kujikinga kisha baada ya kukamilisha kazi yao wanarudi nyumbani na kuoga, changamoto inakuja kwa wanawake ambao wanachukua nguo hizo ambazo tayari zina viuatilifu na kuzifua bila kuchukua tahadhari hatua inayosababisha kunasa viuatilifu hivyo kwa njia ya ngozi.
“Pia utaona kuwa wanawake hawa ndio wanakuwa na jukumu la kurudi shambani kwa ajili ya kupalilia mazao au kuvuna, sasa mama anapoathirika na mtoto pia ameathirika sababu wanakweenda nao shambani na kemikali hizo wanazigusa.
“Iwapo mama atakuwa mjamzito zitaenda moja kwa moja kwa mtoto au hata baadae akija kupata ujauzito madhara yataonekana kwa mtoto atakayezaliwa,” amesema Dkt. Ngowi.
Kulingana na mtaalamu huyo, athari za kemikali hizo zinazotokana na viuatilifu ni pamoja na kuzaa mtoto mwenye mtindio wa ubongo, saratani, mtoto asiye na utulivu na madhara mengine.
Madhara ya viuatilifu hasa vile bandia au vilivyoisha muda wake kwa wanawake ni mara nne zaidi ikilinganishwa na wanaume huku akisema kuwa jamii hususan wakulima wanapaswa kuelimishwa na kutambua kuwa viuatilifu ni hatari.
“Tunatamani watu watambue kuwa kuna viuatilifu vilivyoisha muda wake ambavyo vinauzwa katika maduka ya pembejeo, wakulima nao hawajui sababu wanataka kupata mazao mengi na bora bila kujali athari zake baadae.
“Tunaendelea kusisitiza elimu zaidi kwa jamii ili watambue kuwa viuatilifu ni hatari…ni hatari kwa wote ila mwanamke anaathirika zaidi kwa sababu ya maumbile yake na shughuli za kila siku.
“Ushauri kwa wakulima angalia kama huna ulazima wa kupuliza viuatilifu usifanye hivyo, hata wale wa majumbani wanaopuliza kwa Sh 2,000 wengi wanapuliza viuatilifu vilivyoisha muda wake ,” ameongeza Dkt. Ngowi.
Amesema ni vyema Serikali hususan Wizara zinazohusika ikiwamo ile ya Kilimo kuangalia namna ya kudhibiti viuatilifu ambavyo vimekuwa vikiingia nchini.
Awali, Afisa Program Mkuu wa Asasi ya AGENDA inayojihusisha na masuala ya Mazingira na Maendeleo, Silvani Mng’anya, amesema kumekuwa na matumizi yasiyo ya lazima ya viuatilifu nchini hususan katika kilimo hatua inayochochea madhara zaidi ya kiafya kwa binadamu.
“Kumekuwa na madhara mengi katika matumizi ya viuatilifu yasiyo sahihi na si ya lazima hasa ambavyo vimeisha muda wake na kwa sehemu kubwa vimekuwa vikitumika katika kilimo hapa nchini.
“Wananchi wengi wanatumia viuatilifu bila kuwa na elimu, matokeo yake vinakuja kuleta madhara baadae, kwa hapa nchini ukiangalia hali bado hairidhishi kwani uelewa uko chini na baadhi ya maeneo wanatumia viuatilifu zaidi ya kimoja kwenye ndoo moja matokeo yake mazao anayopulizia yanaenda kuleta madhara kwa mlaji ikiwamo kuathiri mazingira, hivyo matumizi ya viuatilifu bado siyo mazuri nchini,” amesema Mng’anya.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani(WHO) ya mwaka 2010 ilikadiria kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwamo yale yanayosababishwa na viuatilifu yatasababisha vifo Barani Afrika kuliko magonjwa ya kuambukiza na ya lishe ikiwamo vifo vya mama na watoto kwa pamoja ifikapo mwaka 2030.
Akitoa ushauri kwa wanawake juu ya kupulizia dawa ndani, Katibu Mtendaji wa AGENDA, Dorah Swai, amesema ni vema wanawake wakaelimishwa juu ya madhara hayo.
“Ushauri kuhusu kupiga dawa ndani, wanawake waambiewe kabisa madhara ya viautilifu, kwani tunafahamu kuwa madhara yake kwa watoto ni makubwa zaidi kuliko inavyochukuliwa,” amesema Dorah.
Akizungumzia changamoto hiyo ya viuatilifu, Wakili Kitua Kinja kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Kilimo Tanzania(TPAWU) amesema sheria pia bado ni changamoto, kwani haiwawajibishi watu wanaofanya kazi ya kuuza viuatilifu hasa vile ambavyo ni bandia.
“Madhara yatokanayo na matumizi ya viuatilifu ni mengi na hii inasababishwa na kutosimamia sheria na zilizopo haziwabani watu wanaoingiza bidhaa hizi hasa zile bandia, sumu zinapoingia mwilini zinaenda kuharibu mifumo ya neva, ukiangalia mfano kijijini bado elimu haijafika juu ya matumizi ya viuatilifu.
Wananchi wengi hawana uelewa, mkulima anajua tu kwamba hii ni dawa naenda kupuliza kwenye shamba kwa ajili ya kuua wadudu wanaoshambulia mazao bila kuwa na elimu.
Kama wadau tunalo jukumu la kuendelea kuishinikiza Serikali ichukue hatua ikiwamo kuangalia tena sheria,” amesema Wakili Kinja.
SERIKALI KUANZISHA MAABARA NDOGO
Katika kukabiliana na changamoto ya viuatilifu bandia, Machi mosi, 2023 Serikali kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania (TPHPA) ilisema kuwa inatarajia kuanzisha maabara ndogo kwenye vituo 17 vya ukaguzi mipakani.
Hatua hiyo ilikuja kufuatia mamlaka hiyo kudai bado kuna changamoto ya viatilifu bandia kuingia nchini kupitia maeneo ya mipakani na njia zisizo halali.
0 Comments