Sehemu ya Mlima Hanang ilimeguka kutokana na kuwa na miamba dhaifu na kusababisha maafa yaliyotokea, wataalamu wa Wizara ya Madini wamesema kwenye taarifa yao fupi kuhusu chanzo cha maafa wilayani Hanang.
Kauli hiyo imezungumzwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi muda mfupi uliopita na wataalamu Wizara ya Madini walifanya ukaguzi, ambapo taarifa fupi inasema chanzo cha maafa hayo ni kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang, ambayo ilikuwa na miamba dhaifu.
“Baada ya miamba kumekuga, ilinyonya maji na kusababisha mmomonyoko, sehemu ya maporomoko yakasababisha tope, sehemu iliyonyonya maji ilifanya mkandamizo na sehemu ya mlima ilishindwa kuhimili mgandamizo na kusababisha kumeguka na kutengeneza tope lililoporomoka na kuezua nyumba, miti na kuharibu miundombinu,”amesema Matinyi.
Matinyi amesema kulingana na maelezo ya wataalamu hao, Mlima Hanang umeundwa kwa chembechembe za mchanga utokanao na volcano.
Amesema taarifa za matetemeko zilizoanza kutolewa tangu Septemba hakukua na matatetemeko wala volcano katika maeneo hayo.
"Uchunguzi ulifanywa kwa kupita kwa njia ya miguu, helikopta," amesema Matinyi.
0 Comments