NA JIMMY KIANGO
Kiasi kikubwa cha tani 315,000 za taka za plastiki zinazolishwa Tanzania kwa mwaka kinakadiriwa kuishia Baharini, mitoni na kwenye maziwa hali inayotishia uhai endelevu wa viumbe vilivyopo kwenye maeneo hayo.
Ripoti kutoka IUCN, zinabainisha kuwa nchini Tanzania kiasi cha tani 29,000 za plastiki ziliingia katika mito, mabwawa na bahari kwa 2018 pekee.
Aidha ripoti kutoka shirika la “Prevented Ocean Plastic East Africa” zinaeleza kuwa takribani tani 29 za plastiki huelea baharini kila mwaka.
Hali hii inaashirikia hatari na juhudi za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kuepusha uchafuzi wa mazingira ya pwani, Baharini, kwenye mito na mabwawa nchini.
Hatua hiyo itasaidia kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuupa nafasi uchumi wa Buluu kuwa moja ya maeneo muhimu ya kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) limeuona umuhimu huo na kuamua kutekeleza mradi wa Pwani Yetu wenye lengo la kulinda mazingira ya bahari na pwani sanjari na kukuza uchumi kwa wananchi wanaoitumia bahari kujipatia kipato.
Mshauri wa mradi huo kutoka GIZ, Dkt. Robert Katikira anasema mradi huo ni msaada mkubwa katika kuikoa bahari ambayo inakabiliwa na uharibifu unaotokana na shughuli za binadamu.
“Ni mradi muhimu kwa mustakabali wa nchi na bahari kwa ujumla.”
Katika kufanikisha hatua hiyo GIZ kwa kushirkiana na taaisisi binafsi ya Nukta Afrika yenye makao makuu yake Dar es Salaam Tanzania na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) wameiona haja ya kuwaelimisha wanahabari umuhimu wa jamii kuitunza bahari.
Mradi huo unalenga kuhudumia sehemu ya kilomita za mraba 1,424 za Pwani ya Tanzania bara huku mikoa ya Tanga, Lindi na Mtwara ikihusika moja kwa moja.
Mkurugenzi wa JET, John Chikomo anaweka wazi kuwa kuna umuhimu mkubwa wa Waandishi wa Habari kupewa elimu ya uandishi sahihi wa uhifadhi wa Bahari na Pwani mara kwa mara.
“Waandishi wa Habari ndio jicho, sikio na mdomo wa wananchi wengi, wao wakilielewa jambo kwa undani kwa kuliona, kulisikia na kuwa na uwezo wa kulisemea ni wazi jamii itaelewa kwa haraka kwa sababu maandishi na matangazo yao yanamfikia mwananchi kwa kasi.
“Mafunzo ya uhifadhi wa bahari na pwani yanapaswa kuwa endelevu, hatua hiyo itasaidia kuiokoa bahari na uharibifu unaofanywa na binadamu,”alisema Chikomo.
GIZ, Nukta Afrika na JET, kwa pamoja waliwakutanisha waandishi wa Habari za Mazingira zaidi ya 30 kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini na wataalamu wa masuala ya uhifadhi wa bahari na kuwapa mafunzo ya siku tatu yaliyofanyika jijini Tanga, kuanzia Septemba 17-19,2025.
Miongoni mwa waliotoa mafunzo hayo ni Dkt. Robert, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Jestina Katundukila na Mkuregenzi Mtendaji wa Nukta Afrika, Nuzulack Dausen.
Katika mafunzo hayo, Dausen aliwapitisha waandishi wa Habari za Mazingira kwenye maeneo mbalimbali ya uandishi wa Habari wenye tija, huku akiwasisitiza kutokwepa kutumia teknolojia hasa Akili Mnemba.
“Msiogope kutumia AI,” alisema huku akiwatahadharisha kuongeza akili zao kwenye kila majibu watakayoyapata kutoka kwenye AI.
Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Bilihuda Mbowe, alisema amefurahishwa na elimu aliyoipata, anaamini itamsaidia kwenye kazi zake za uandishi wa Habari za mazingira, hata hivyo ameiomba GIZ kutoa mafunzo hayo mara kwa mara kwao ili kuendelea kuwajengea uwezo. “Tunayahitaji mafunza haya zaidi na zaidi.”
Mazingira ya Bahari nchini yanakabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.
Mathalani katika maeneo ya Mjimwema, Tungi, Somangila, Bamba na Mwongozo wilayani Kigamboni yamekumbwa na adha ya kufa kwa miti ya mikoko, mikoko na nyasi bahari kutokana kusambaa kwa mafuta katika eneo kubwa la bahari na pwani.
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja, jijini Tanga.
Mafuta hayo yalimwagika na kusambaa Desemba 3,2024 baada ya kupasuka kwa bomba la mafuta la TAZAMA.
Hatua hiyo imesababisha kuyaacha maeneo hayo yakiwa tasa, kwa sasa hakuna mmea wowote wa baharini unaomea katika eneo hilo.
Mashuhuda wanasema mafuta yalifika hadi mashamba ya mwani, na wakati wa tukio kulikuwa na harufu kali na uhaba wa maji.
0 Comments