Ticker

7/recent/ticker-posts

TMDA YAPONGEZWA KWA KUDHIBITI UBORA WA DAWA NA VIFAA TIBA

 

NA JIMMY KIANGO- TABORA

Ufanisi katika utendaji kazi na usimamizi wa majukumu yake, umemsukuma Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha kuipongeza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA).


Chacha amepotea pongezi hizo Julai 16,2025 mkoani humo alipofungua mkutano wa kikao kazi uliohusisha watendaji wa mamlaka hiyo na Wahariri wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.


Alisema TMDA imekuwa ikifanya kazi kubwa ya udhibiti wa dawa kwenye mkoa wake na Tanzania kwa ujumla, hatua inayoongeza ubora wa huduma za afya nchini.


Katika kuhakikisha TMDA inaendelea kuwa mdau wa mae deleo mkoani Tabora kupitia sekta ya Afya, Chacha aliiomba mamlaka hayo kuendelea na mpango wake wa kujenga Tanuru mkoani humo kwa sababu anaamini ujenzi wa tanuru hilo utaleta tija kwa mkoa.


Ameeleza kuwa  wamejipanga kuhakikisha hati miliki ya kiwanja cha TMDA iliyokwama bila sababu  inatolewa haraka ili kuruhusu TMDA kuendelea na ujenzi wa miundombinu yao.


Chacha amesema kwamba Tabora ina umuhimu wa kimkakati kutokana na kupitiwa na reli ya kisasa ya  (SGR) huku akifafanua kuwa maboresho makubwa katika sekta ya afya yamefanyika chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan .


Ameweka wazi kuwa maboresho hayo ni kuimarishwa kwa taasisi mbalimbali za umma ikiwemo  TMDA ambayo inadhima kubwa ya kujali afya za Watanzania.


Pia ametumia nafasi hiyo kuelezea  wasiwasi wake kuhusu ongezeko la matangazo holela ya dawa za binadamu, na kuiomba TMDA kushirikiana na vyombo husika kudhibiti hali hiyo. 


“Pia ni vema wafanyabiashara wakaelemishwa kuhusu madhara ya dawa na vifaa tiba bandia na duni ambavyo si salama kwa matumizi ya binadamu.”


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, amesema TMDA kwa kushirikiana na taasisi nyingine inaendesha utafiti maalumu kubaini kiwango cha matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs) katika ukuzaji wa mifugo.

Dkt. Fimbo ameeleza kuwa  baada ya utafiti huo  kukamilika, watakuwa katika nafasi nzuri ya kuchukua hatua stahiki za  kudhibiti suala hilo.


Kuhusu kikao cha wahariri amesema lengo la kikao hicho ni kuwaongezea uelewa Wahariri kuhusu majukumu ya TMDA na kuonyesha mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya  Serikali ya Awamu ya Sita.


Pamoja na mafanikio lukuki, Dkt. Fimbo ametaja moja ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na usajili wa jumla ya dawa 8,332 katika kipindi hicho, hatua iliyosaidia kupanua upatikanaji wa dawa muhimu kwa wananchi.


Akitoa neno la shukurani kwa TMDA, aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, Joyce Shebe alisema uamuzi wa mamlaka hiyo kuwaalika kwenye kikao hicho ni hatua muhimu inayowapatia maarifa yatakayowezesha kuandika kwa ufanisi zaidi kuhusu masuala ya afya.


"Hii ni hatua nzuri kwetu Wahariri kujua umuhimu wa TMDA kwa afya ya Watanzania na nikiri kuwa wanafanya kazi kubwa sana na tunapaswa kuwaunga mkono kwa kutoa taarifa pale tunapoona kuna mambo yasiyofaa katika eneo la dawa, vifaa tiba na vitendanishi."

Post a Comment

0 Comments