NA JIMMY KIANGO
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Magharibi, imefanikiwa kukamata dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 822.8 vilivyokuwa vikiuzwa kinyume cha sheria mkoani Tabora, kufuatia oparesheni maalumu iliyofanyika katika wilaya zote za mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa TMDA Kanda ya Magharibi, Christopher Migoha, amesema jumla ya kilo 2,300 za dawa na vifaa tiba hivyo zilikamatwa na kuteketezwa baada ya kubainika kuwa haziruhusiwi kuuzwa katika maduka ya watu binafsi kwa mujibu wa sheria na kanuni za mamlaka hiyo.
Amefafanua kuwa oparesheni hiyo ilihusisha ukaguzi katika hospitali, vituo vya afya, zahanati pamoja na maduka ya dawa za binadamu na mifugo, ambapo walikagua jumla ya maduka 408 ya dawa, hospitali 16, vituo vya afya 17 na zahanati 17 mkoani
humo.
Aidha, amesema TMDA imeendelea na jukumu la kijamii kwa kutoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 28.2 kwa Hospitali ya Jeshi la Wananchi ya Milambo iliyopo mkoani Tabora.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Mkoa wa Tabora, Paulo Makali, amewataka wauzaji na wasambazaji wa dawa kununua bidhaa hizo katika vyanzo rasmi ili kuepuka hatua za kisheria, huku wadau wa TMDA wakishauri kufanyika kwa semina za mara kwa mara kwa wauzaji wa dawa ili kulinda afya za wananchi.
0 Comments