Ticker

7/recent/ticker-posts

HAKUNA DAWA ZA KUONGEZA UKUBWA WA MATITI NA MAKALIO-TMDA

  

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo.

NA.JIMMY KIANGO

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la matangazo ya bidhaa zinazodai kuongeza ukubwa wa viungo vya mwili hasa kwa wanawake kama vile matiti, makalio na mahipsi. 


Bidhaa hizi huuzwa kama vidonge, mafuta, krimu au hata sindano zisizo na udhibiti wa kitabibu. Hata hivyo, swali la msingi linabaki: Je, kuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha ufanisi wa bidhaa hizi!


UKOSEFU WA USHAHIDI WA KISAYANSI

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali katika nyanja za biolojia ya binadamu na tiba (medical science), hakuna ushahidi wa kisayansi unaokubalika kimataifa unaothibitisha kuwa vidonge au krimu vinaweza kuongeza ukubwa wa sehemu za mwili wa binadamu. Hakuna.


Tafiti nyingi zinazohusiana na ukuaji wa tishu za mwili zinaonesha kuwa ukubwa wa viungo kama matiti na makalio hutegemea mambo makuu yafuatayo:

  • Vinasaba (genetics)
  • Homoni (hasa estrogen na progesterone)
  • Lishe na mtindo wa maisha


Bidhaa zinazodaiwa kuongeza ukubwa wa viungo mara nyingi hazijafanyiwa majaribio ya kliniki (clinical trials) yenye uthibitisho wa kitaalamu.

Ukweli wa hili umethibitishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu, Dkt. Adam Fimbo.

 

Katika mazungumzo yake na Waandishi wa Habari, Dkt. Fimbo alisema matangazo ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara kuwa kuna dawa ambayo inaongeza makalio au viungo vya mwili wa binadamu ni ya uongo.

 

“Hakuna udhibitisho wowote wa kisayansi unaodhibitisha kuwa dawa fulani  alipewa mtu akiwa na makalio madogo na baada ya kutumia kwa kipindi fulani makalio yakaongezeka.

 

“Hakuna utafiti kama huo. Ni upotoshaji. Nilitamani sana waandishi muweze kuielemisha jamii kwa sababu ya huo upotoshaji ili tuweze kuwalinda, lengo letu sisi ni kulinda afya ya jamii, ni muhimu watu kufahamu hakuna dawa inayoweza kukuongezea kiungo chako cha mwili.

 

“Hakuna utafiti wowote wa kisayansi unaothibitisha hilo na wale wanaopotosha waache kufanya hivyo.”amesema Dkt.Fimbo.

JINSI MWILI WA BINADAMU UNAVYOKUA

Ukuaji wa matiti na sehemu nyingine za mwili hutokea kwa njia ya kiasili kupitia mabadiliko ya homoni, hasa wakati wa balehe.


Matiti huongezeka kutokana na ukuaji wa tishu za mafuta na tezi za maziwa na makalio na mahipsi huathiriwa na usambazaji wa mafuta mwilini.


Hakuna dawa ya nje inayoweza “kulenga” sehemu moja ya mwili na kuikuza bila kuathiri mfumo mzima wa mwili.


HATARI ZINAZOWEZA KUJITOKEZA

Matumizi ya bidhaa zisizo na uthibitisho wa kisayansi yanaweza kuleta madhara ya mabadiliko ya homoni yanayoweza kuathiri afya ya uzazi, madhara ya ini na figo kutokana na kemikali zisizojulikana, mzio wa ngozi (skin reactions) na hatari ya saratani endapo bidhaa zina viambato vya homoni bila udhibiti.


TMDA, Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na mamlaka nyingi za dawa duniani zinasisitiza umuhimu wa kutumia bidhaa zilizosajiliwa na kuthibitishwa kitaalamu.


TAMAA ZA FEDHA

Wauzaji wa bidhaa hizi hutumia mbinu za kisaikolojia na matangazo ya kuvutia, ikiwa ni pamoja na kuweka picha zilizohaririwa zinazobeba sura ya watu waliofanikiwa huku wahusika wakijua wazi kuwa ni uongo.


Aidha kuna shuhuda wa watu (testimonials) usio na uthibitisho na kutoa ahadi za matokeo ya haraka

Hizi si mbinu za kisayansi bali ni mikakati ya kibiashara inayolenga kuvutia wanunuzi.


NJIA SALAMA NA SAHIHI

Wataalamu wa afya wanashauri njia zifuatazo kama mbadala salama ambazo ni mazoezi ya mwili hasa ya misuli ya makalio na kifua, lishe bora yenye protini na mafuta yenye afya, ushauri wa kitaalamu wa kitabibu kabla ya kufikiria hatua yoyote ya kimatibabu kama upasuaji.


Kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi uliopo, ni wazi kuwa hakuna dawa zilizothibitishwa kitaalamu zinazoweza kuongeza ukubwa wa matiti, makalio au mahipsi kwa njia ya asili na salama. 


Dkt. Fimbo anawashauri wananchi hasa wanaotamani kuongeza ukubwa wa viungo vyao kuwa wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya bidhaa zinazodai kufanya hivyo bila ushahidi, na badala yake kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.

Elimu sahihi ya kisayansi ni kinga dhidi ya udanganyifu. 

Post a Comment

0 Comments