NA. JIMMY KIANGO
Bonde la Ruvuma ni moja ya mandhari muhimu zaidi barani Afrika. Mustakabali wake utategemea namna tunavyosimamia maendeleo na uhifadhi kwa pamoja.
Mradi wenye lengo la Kuimarisha usimamizi shirikishi wa mpakani wa mfumo wa chanzo hadi bahari wa Bonde la Mto Ruvuma na maeneo yake ya pwani ili kuhakikisha afya ya mifumo ya ikolojia na usalama wa maisha ya wananchi, ndio umepewa jukumu la kusimamia maendeleo na uhifadhi.
Mwenyekiti wa mradi wa Usimamizi na Maendeleo ya Pamoja ya Bonde la Ruvuma, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa ARA-Norte, IP, Carlitos Momade Omar amesema yapo maeneo matano muhimu yanayopaswa kutiliwa mkazo ili kufanikisha lengo.
Maeneo hayo ni kuimarisha mifumo ya taasisi, kuboresha maamuzi yanayotegemea sayansi,kuongeza uwekezaji na uhamasishaji wa rasilimali na kuimarisha uwezo wa utekelezaji wa sera na sheria.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Omar, amesema ushirikishwaji wa jamii hususan wanawake na vijana utaongezwa, huku sekta binafsi ikihamasishwa kushiriki katika mifumo endelevu ya ufadhili.
“Ni heshima kubwa kwangu kufungua rasmi Warsha ya Uzinduzi wa Mradi wa Kuimarisha Usimamizi Shirikishi wa Chanzo hadi Bahari wa Bonde la Ruvuma.
“Kwa niaba ya nchi wanachama wa Bonde la Ruvuma na mwenyeji wetu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninawakaribisha wote katika warsha hii muhimu.
“Kwa kufika kutoka nchi zenu mbalimbali, mmeonesha dhamira yenu ya dhati katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na usimamizi wa pamoja wa Bonde la Ruvuma.” Amesema.
MWANZO WA SAFARI
Akizungumzia mwanzo wa safari ya mradi huo, Omar amesema safari ya mradi huo haijaanza sasa, badala yake ni mchakato wa muda mrefu.
Anasema safari hiyo imejengwa juu ya miaka ya majadiliano, tafiti za bonde na ushirikiano wa kiufundi, na muhimu zaidi ni kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) Julai 2024 jijini Dar es Salaam na serikali zetu tatu.
MWANZO WA MRADI
Mradi ulianza na ‘Project Identification Form mwaka 2024’ambapo uliidhinishwa kikamilifu mwaka 2025, bajeti yake ikiwa ni USD 7,122,018 ambazo ni zaidi ya tsh. 18 biliano na zimetolewa na GEF na utatekelezwa kwa miaka mitano (2025–2030).
SHUKURANI
Omar amewashukuru Global Environment Facility (GEF) kwa ufadhili, IUCN kwa uongozi wake pamoja na washirika Global Water Partnership Southern Africa na Wetlands International na serikali za Malawi, Msumbiji na Tanzania.
Amesema thamani kubwa ya mradi huo ni kushughulikia changamoto za bonde kwa mtazamo jumuishi wa chanzo hadi bahari.
“Tunatambua kuwa usimamizi wa ardhi unaathiri afya ya mito, afya ya mito inaathiri maeneo ya pwani na maamuzi katika sehemu moja ya bonde yana athari katika maeneo mengine.”
Alisema Warsha hii itasaidia kuoanisha utekelezaji wa mradi, kupitia mpango kazi, kufafanua majukumu ya taasisi na kuboresha mipango ya wadau, jinsia na ufuatiliaji.
Akifungua warsha hiyo alisema: Ni matumaini yangu kuwa kupitia warsha hii tutaimarisha ushirikiano wetu, tutajenga uaminifu na kuhakikisha ustawi wa wananchi na mazingira unakuwa kitovu cha maamuzi yetu.
MRADI WA RUVUMA GEF
Nchi za Malawi, Msumbiji na Tanzania zimeamua kushirikiana kulinda mifumo ya ikolojia na kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
Katika kufanikisha zoezi hilo kiasi cha takribani dola za Marekani milioni 7.12 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi bilioni 18.3 kinatarajia kutumika katika kulinda mifumo ya ikolojia katika nchi hizo tatu zilizopitiwa na bonde la Mto Ruvuma.
Mradi huo unaojulikana kama GEF Ruvuma, umelenga Kuimarisha usimamizi shirikishi wa mpakani wa mfumo wa chanzo hadi bahari wa Bonde la Mto Ruvuma na maeneo yake ya pwani ili kuhakikisha afya ya mifumo ya ikolojia na usalama wa maisha ya wananchi.
Akiuzungumzia mradi huo ambao pia utasaidia maisha endelevu na jumuishi ya wananchi, Afisa Mradi huo kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Maliasili Tanzania (IUCN-Tanzania),Bi. Ng’walu Kidayi amesema mradi huo ni wa kikanda ambao unatekelezwa katika nchi zinazopitiwa na bonde hilo ambazo ni Malawi, Msumbiji, na Tanzania.
Bi. Kidayi amesema kuwa mradi huo una thamani ya takribani dola za Marekani milioni 7.12 na unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 60 kutoka mwaka huu wa 2026 hadi Desemba 2030.
Aliwataja wafadhili wa mradi huo kuwa ni Global Environment Facility (GEF) na unaongozwa na IUCN kama wakala wa utekelezaji wa GEF, kwa kushirikiana na Global Water Partnership Southern Africa (GWPSA) na Wetlands International Eastern Africa (WIEA) ambazo ni taasisi zinazotekeleza mradi huo.
“Lengo la mradi ni kulinda uadilifu wa mifumo ya ikolojia huku ukiimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kusaidia maisha endelevu na jumuishi ya wananchi katika nchi zote tatu zinazopitiwa na bonde la Ruvuma.
“Taasisi za kikanda na za kitaifa katika nchi hizo tatu zina nafasi muhimu katika utekelezaji wa mradi, huku mifumo ya uratibu wa pamoja wa mpakani ikitumika kama kitovu cha usimamizi na ushirikiano wa bonde,”amesema.
SHUGHULI ZA MRADI WA GEF
Mradi wa GEF utatekeleza shughuli mbalimbali ili kuimarisha upangaji na usimamizi shirikishi wa ardhi, maji safi, mifumo ya pwani na bahari kwa kutumia mfumo wa chanzo hadi bahari (source-to-sea approach).
Shughuli hizi zimepangwa katika vipengele vitano vikuu vya mradi ambavyo ni Kuimarisha mifumo ya taasisi kwa ajili ya usimamizi wa bonde na maeneo ya pwani katika mipaka ya nchi na Kuwezesha usimamizi wa bonde na maeneo ya pwani kupitia maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kisayansi.
Shughuli nyengine ni Kusaidia upangaji wa kimkakati wa uwekezaji na uhamasishaji wa rasilimali kwa ajili ya usimamizi jumuishi wa bonde na pwani,Kukuza usimamizi endelevu wa ardhi na maji kwa njia ya ushirikishwaji wa jamii na wadau na Usimamizi wa mradi, uzalishaji wa maarifa, mawasiliano na usambazaji wa taarifa.
Kwa pamoja, vipengele hivyo vinalenga kuimarisha ushirikiano wa nchi katika usimamizi wa maji ya mipakani, kulinda mifumo muhimu ya ikolojia kutoka milimani hadi baharini na kuleta manufaa ya kijamii, kimazingira na kiuchumi kwa jamii za Bonde la Ruvuma.
0 Comments