NA MWANDISHI WETU
Wakati leo Septemba 22, dunia ikiadhimisha siku ya faru duniani, maisha ya faru mweusi yanatajwa kuwa hatarini pamoja na kupungua kwa ujangili kwa miała 10 sasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi ya taasisi ya Kimataifa wa Faru, (International Rhino Foundation) iliyotoka kwenye ripoti ya State of the Rhino yam waka 2025 ujangili uko katika kiwango cha chini kwa miaka 11, lakini bado unatishia baadhi ya makundi
Inaelezwa kuwa kwa mwaka jana 2024 Faru mmoja aliwindwa na kuuawa kila baada ya saa 15 barani Afrika, hata hivyo sasa kumekuwa na ongezeko la Wanyama hao.
Takwimu mpya zinaonesha kwa sasa viwango vya ujangili vipo chini zaidi kuliko ilivyokuwa kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita. Idadi ya faru barani Asia na Afrika kwa ujumla imeongezeka kwa faru 430 na kufikia faru 26,700 tangu sensa ya mwisho rasmi ya mwaka 2022.
Wild Africa inasisitiza kuwa licha ya hatua hii chanya, janga la ujangili bado ni tishio kubwa kwa Wanyama hao. Ikumbukqwe kuwa Afrika ndiyo makazi ya faru wengi zaidi duniani, wakiwemo faru weusi walioko kwenye hatari kubwa ya kutoweka (critically endangered) ambao pia ni sehemu ya “Big Five”, huku faru weupe wakiwa kwenye hatari ndogo zaidi (near-threatened). Makadirio ya sasa yanaonyesha kuwa faru weusi ni 6,788 na faru weupe 15,752.
Ujangili na biashara haramu ya pembe za faru bado ndizo hatari kuu kwa uhai wao, zikichochewa na mahitaji kutoka Vietnam na China, changamoto za kijamii na kiuchumi barani Afrika, na magenge ya uhalifu yaliyoandaliwa.
Pembe za faru hutumika kama dawa nchini Vietnam na China, pia hutengenezwa mapambo na vitu vya kifahari katika tiba ya jadi ya Kichina.
Katika jitihada za pamoja za kuzuia kutoweka kwa faru, serikali za Afrika na mashirika ya uhifadhi yameweka mikakati mbalimbali ya kupambana na ujangili. Hii ni pamoja na ulinzi wa moja kwa moja, ufuatiliaji wa kijasusi, mafunzo ya hali ya juu kwa walinzi na ukaguzi wa mara kwa mara, pamoja na ushirikiano thabiti na jamii za wenyeji.
Pia miradi mingi inatumia teknolojia bunifu kama kamera maalumu, doria za angani, na vihisi mwendo, pamoja na mpango wa kuhamisha faru kutoka maeneo yenye hatari kubwa. Ingawa maendeleo ni ya polepole, njia hizi mseto zinaanza kuonyesha matokeo.
Tangu kuanza kwa janga la ujangili mwaka 2008, zaidi ya faru 12,000 wameuawa barani Afrika, huku idadi kubwa zaidi ikiwa mwaka 2015 ambapo faru 1,349 waliwindwa. Kwa kulinganisha na mwaka 2024 kulikuwa na matukio 516 pekee vilivyoripotiwa.
Kwa mujibu wa ripoti ya The African and Asian Rhinoceroses – Status, Conservation and Trade (CITES 2025), ujangili ulihusika na upungufu wa asilimia 2.15 pekee ya idadi ya faru barani Afrika mwaka 2024 kikiwa ni kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka 13.
“Japokuwa ujangili wa faru umepungua mwaka huu na idadi yao inaongezeka kwa ujumla, bado faru wapo hatarini kutokana na tamaa ya pembe zao. Ukaguzi na uadilifu wa walinzi unatakiwa kufanyika kwa wote kwani umethibitishwa kuwa na mafanikio. Vilevile, elimu na kupunguza mahitaji nchini Vietnam na China ni muhimu katika kuzalisha upya idadi ya faru,” anasema Peter Knights OBE, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Africa.
Ingawa kuna matumaini kwa faru, bado safari ni ndefu, mafanikio haya ni muhimu lakini bado ni dhaifu. Uwekezaji endelevu katika ulinzi, ushirikiano wa kimataifa ulio thabiti, na juhudi endelevu za kupunguza mahitaji (hasa katika nchi zinazonunua) ni muhimu ili kuhakikisha mustakabali wa spishi hizi.
Katika Siku ya Faru Duniani 2025, Wild Africa inatoa mwito kwa serikali, vyombo vya sheria, mashirika ya uhifadhi na umma kubaki macho na kuendeleza dhamira ya kuhifadhi faru kwa kubeba kauli mbiu ya Kataa ujangili na biashara haramu ya wanyamapori, linda makazi ya faru na ripoti uhalifu wa wanyamapori.
0 Comments