*WWF waitekeleza kwa vitendo watoa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya bilioni moja vitakavyosaidia ulinzi wa Misitu.
NA JIMMY KIANGO
Moja kati ya tafsiri za maandiko ya Biblia yaliyotafsiriwa ndivyo sivyo na waamini wengi ni yale yaliyopo kwenye kitabu cha Mwanzo 2:16-17 yanayosema:
Mwanzo 2:16, Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu (Adam) akisema Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, 17: walakini matunda ya mti wa ujuzi wa me mana mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika, aidha maandiko kutoka kwenye Msahafu tukufu,Surat Al-Baqara Quraan 2:35 maandiko yanasema: Na tukasema, Ewe Adam kaa wewe na mkeo katika bustani na kuleni humo kwa furaha kila mtakapo, lakini msikaribie mti huu, mkawa miongoni mwa madhalimu."
Watu wengi wameyafungamanisha maandiko haya na masuala ya uzinzi, kwamba Adam ambae kwenye andiko hilo anatajwa kama mtu huyo alirubuniwa na Hawa wakajikuta wanazini, ukweli hauko hivyo.
Ukweli ni huu simulizi hilo ni dhana ya picha iliyowekwa ili kuwasaidia akina Tomaso kuamini kwa haraka, hebu sasa twende taratibu ili unielewe:
Masuala ya uhifadhi wa mazingira na mimea ni sehemu ya maisha ya kila binadamu. Dunia tuliyopewa na Mungu imejaa miti, mimea, wanyama, maji na hewa safi, rasilimali zinazowezesha maisha kuendelea.
Ukweli ni kwamba jukumu la kuzihifadhi mali hizo halikuanza leo ni dhana ya kale ambayo hata maandiko matakatifu yanaonyesha kuwa chanzo chake ni mapema sana katika historia ya mwanadamu.
Na hapa kwa lugha ya kisasa tunaweza kusema kazi ya kwanza ya Mungu kwa dunia ilikuwa ni kuunda Wizara ya Maliasili na Utalii na Waziri wake wa kwanza alikuwa ni Adam huku Naibu wake akiwa Haw ana aliwapa na sheria kabisa. Tutaelewana tu:-
UHIFADHI KATIKA MUKTADHA WA KIROHO:
Sheria ya kwanza ya uhifadhi ilikuwa ni katazo la kwanza ndani ya bustani ya Edeni, katika kitabu cha Mwanzo kama nilivyoandika hapo juu, tunasoma simulizi ya bustani ya Edeni.
Mungu alimpa Adamu na Hawa bustani nzuri yenye kila aina ya miti ya kupendeza na yenye matunda mazuri kwa chakula.
Hata hivyo, Mungu aliweka katazo maalum: “Usile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya”.
Katazo hili linaweza kutazamwa si tu kama kanuni ya kiroho, bali pia kama ishara ya sheria ya kwanza ya uhifadhi duniani.
Kwa nini? Kwa sababu Mungu aliweka mipaka. Alionyesha kwamba si kila kitu kilicho duniani ni cha kutumiwa kiholela.
Kuna baadhi ya ndege, samaki, wanyama, mimea na matunda ambayo yanahitaji kuheshimiwa, kuachwa bila kuguswa, ili kuhakikisha uwiano na maana ya maisha vinabaki salama.
Kwa mtazamo huu, kanuni ya uhifadhi haianzi na sayansi ya kisasa pekee bali inarudi hadi kwenye mizizi ya kiroho ya mwanadamu katika Edeni.
UMUHIMU WA UHIFADHI WA MIMEA:
Mimea ina nafasi ya kipekee katika mfumo wa maisha duniani, ni chanzo cha hewa safi, miti na mimea hutoa oksijeni tunayopumua.
Kinga ya mazingira, misitu huzuia mmomonyoko wa udongo, kuhifadhi maji, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Chakula na dawa, asilimia kubwa ya vyakula na dawa zinazotumiwa na binadamu duniani kote hutokana na mimea, makazi ya viumbe hai, mimea hutengeneza makazi kwa wanyama, ndege na wadudu wanaohitajika katika mnyororo wa maisha.
MAFUNZO YA KIROHO KWA UHIFADHI:
Kama katazo la Edeni lilivyokuwa wito wa heshima na utiifu, vivyo hivyo uhifadhi wa mazingira leo unahitaji nidhamu, heshima na uwajibikaji.
Binadamu wanapoheshimu mipaka ya matumizi ya rasilimali, wanakuwa washiriki wa mpango wa Mungu wa uendelevu wa maisha.
Lakini pale tunapovunja sheria za kiasili kwa kukata miti kiholela, kuchafua mito, au kuharibu misitu matokeo ni dhahiri,magonjwa, ukame, mafuriko na upotevu wa uhai.
Katazo la Mungu kwa Adamu na Hawa linaweza kufasiriwa kama mfano wa sheria ya kwanza ya uhifadhi na kanuni kwamba dunia na mimea si mali ya mtu binafsi pekee bali ni urithi wa vizazi vyote.
Uhifadhi wa mazingira si wazo jipya la karne ya 21, bali ni agizo la kale lenye mizizi ya kiroho. Kwa kuheshimu kanuni hizi, tunadumisha uwiano wa uumbaji na kushirikiana na Mungu katika kulinda dunia aliyoiumba kwa upendo na kwakulijua hilo ndipo Shirika la Kimataifa la linalojihusisha na Uhifadhi wa mazingira na Kulinda Wanyamapori (WWF) limeiona haja ya kuitii sheria ya Mungu kwa kuikabidhi Serikali ya Tanzania vifaa vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya sh. Bilioni moja kwa ajili ya kulinda na kufanya doria kwenye misitu nchini.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utali, Dkt. Hassan Abbasi, Septemba 11,2025 kwenye viwanja vya ofisi za WWF vilivyopo, Mikocheni Dar es Salaam.
Akipokea vifaa hivyo ambavyo ni magari manne, pikipiki 10, boti ya mwendokasi moja, mashine za malipo 25, mifumo ya mawasiliano ya redio mbili, Kompyuta za mezani tano,jenereta tano, kamera tano pamoja na samani na vifaa vingine vya ofisi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja Dkt. Abbas amesema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) vitasaidia kuongeza ufanisi katika kulinda misitu na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Abbasi alisema msaada huo kutoka Umoja wa Ulaya unaonyesha mshikamano wa kimataifa katika kulinda rasilimali za misitu na mazingira; Nawapongeza Umoja wa Ulaya na wadau wote kwa mchango huu. Vifaa hivi vitachangia si tu katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa misitu, bali pia katika kusaidia sekta muhimu kama nishati, maji na mazingira, ambazo zote zinategemea misitu," alisema.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa kupitia mradi wa kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji katika uhifadhi wa misitu unaotekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi 2026 katika mikoa saba ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Tabora, Tanga na Pwani.
0 Comments