Ticker

7/recent/ticker-posts

WWF YAKABIDHI VIFAA VYA KISASA KULINDA MISITU

  



NA MWANDISHI WETU

 

Shirika la Kimataifa la linalojihusisha na Uhifadhi wa mazingira na Kulinda Wanyamapori (WWF) limeikabidhi Serikali ya Tanzania vifaa vya kisasa vyenye thamani ya zaidi y ash. Bilioni moja kwa ajili ya kulinda na kufanya doria kwenye misitu nchini.

 

Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utali, Dkt. Hassan Abbasi, Septemba 11,2025 kwenye viwanja vya ofisi za WWF vilivyopo, Mikocheni Dar es Salaam.

 

Akipokea vifaa hivyo ambavyo ni magari manne, pikipiki 10, boti ya mwendokasi moja, mashine  za malipo 25, mifumo ya mawasiliano  ya redio mbili, Kompyuta  za mezani tano,jenereta tano, kamera tano pamoja na samani na vifaa vingine vya ofisi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja Dkt. Abbas amesema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) vitasaidia kuongeza ufanisi katika kulinda misitu na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

 


Dkt. Abbasi alisema msaada huo kutoka Umoja wa Ulaya unaonyesha mshikamano wa kimataifa katika kulinda rasilimali za misitu na mazingiraNawapongeza Umoja wa Ulaya na wadau wote kwa mchango huu. Vifaa hivi vitachangia si tu katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa misitu, bali pia katika kusaidia sekta muhimu kama nishati, maji na mazingira, ambazo zote zinategemea misitu," alisema.

 

Vifaa hivyo vimekabidhiwa kupitia mradi wa kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji katika uhifadhi wa misitu unaotekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi 2026 katika mikoa saba ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Tabora, Tanga na Pwani.

 

Alisema mradi huo unalenga kupunguza uharibifu wa misitu kwa kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia mijini na kuboresha mifumo ya usimamizi wa misitu.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kiongozi wa Programu ya Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi, Savinus Kessy alisema mradi huo unatekelezwa kwa bajeti ya Euro milioni 2.5 na unahusisha wadau mbalimbali wakiwemo Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu.


 “Mradi huu utaleta mabadiliko chanya  katika mnyororo  wa nishati hususani  katika uzalishaji kupitia misiti lengo likiwa kuboresha uhifadhi wa misitu nchini , mifumo ya ufuatiliaji wa misitu katika halmashauri nchini,” alisema.

 

 Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WWF Tanzania, DkT. Amani Ngusaru alisema shirika hilo likiwa mshirika mkubwa wa uhifadhi wa misitu nchini, imejiunga na juhudi za serikali katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kulinda mazingira dhidi ya uharibifu unaotokana na matumizi ya nishati isiyo endelevu kama mkaa.

 

Alisema misitu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa uvunaji usio endelevu wa rasilimali za misitu, ongezeko la kilimo katika maeneo ya misitu, na mahitaji makubwa ya mkaa  yote hayo yanachangia katika uharibifu na upotevu wa misitu ya asili.

 

Changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya misitu ni sheria zinazokinzana, ukosefu wa rasilimali fedha, teknolojia duni na ukosefu wa zana muhimu za kufanikisha usimamizi endelevu wa misitu.

 

Mradi huu umebuniwa kwa msingi wa kuelewa changamoto hizi na kutoa suluhisho kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii na TFS kwa sababu  mradi huo umelenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa TFS katika ngazi ya kitaifa, kikanda na wilaya kwa kuwapatia mafunzo ya kiufundi, vifaa vya kazi, mifumo ya TEHAMA, magari na pikipiki za kusaidia shughuli za ufuatiliaji na ulinzi wa misitu.

 


WWF imekabidhi jumla ya vifaa 74 tofauti kwa TFS hivyo vitasaidia kuimarisha ufuatiliaji wa biashara haramu ya mazao ya misitu, ulinzi wa maeneo ya hifadhi na kuboresha mifumo ya taarifa za usimamizi wa misitu.

 

Mradi huo unalenga kuimarisha ushiriki wa jamii katika uhifadhi wa misitu kwa kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, kupunguza utegemezi mkubwa wa mkaa kama chanzo cha nishati ya kupikia.

 

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi kutoka TFS, Profesa  Dos –Santos Silayo aliishukuru WWF kuwapatia vifaa hivyo kwani vitachangia katika ulinzi wa rasilimali za misiti na kuongeza pato kwa jamii.

 



Post a Comment

0 Comments