Iwe jua ama iwe mvua ya mawe na matofari, ni lazima mchezo wa Simba dhidi ya Yanga uchezwe.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa leo Novemba 5,2023 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Saa 11:00 jioni.
Leo jiji la Dar es Salaam limetawaliwa na mvua tangu alfajiri, lakini tayari Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB) imewatoa hofu wapenzi wa mpira wa miguu kwa kuandika kupitia ukurasa wao wa Instagram kuwa "Hata inyeshe vipi lazima mchezo huo uchezwe.
Simba SC ni mwenyeji katika mchezo huo nambari 111, tangu wakutane kuanzia miaka 1960's.
Matokeo ya ushindi kwa timu moja kati ya hizi mbili, yataisogeza hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hadi sasa, wote wana points 18. Yanga, ipo mbele kwa mchezo mmoja, imeshacheza michezo 7 huku Simba ikiwa na michezo 6.
Mchezo wao wa mwisho ulikuwa katika kuwania Ngao ya Jamii, Agosti 13, 2023 katika Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Simba ilishinda kwa changamoto ya penalti 3-1 baada ya dakika 90 kuisha bila mbabe.
0 Comments