Kikosi cha Yanga leo kimeipiga kama ngoma timu ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Yanga ikiwa na kasi kubwa ya mchezo tangu mwanzo hadi mwisho imeishindilia Simba iliyokuwa nyumbani bao 5-1 mbele ya mashabiki wake.
Yanga ilianza kuandika karamu ya mabao katika dakika ya tatu kupitia kwa Kennedy Musonda, hata hivyo Kibu Dennis alifanikiwa kurejesha goli hilo katika dakika ya tisa na kufanikiwa kwenda mapumziko zikiwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili ndio kilibeba zahama kwa Simba ambapo katika ya 64, Max Nzengeli aliandika bao la pili, Aziz Ki alitia msumari wa tatu katika dakika ya 73, Nzengeli alirudi tena nyavuni katika dakika ya 77 huku Pacome Zouzoua akihitimisha karamu ya magoli katika dakika ya 87.
Ushindi huo umeifanya Yanga kulipiza kisasi cha mwaka 2012, ambapo Simba ilishinda bao 5-0, Mei 6, 2012.
0 Comments