Ticker

7/recent/ticker-posts

RAIS WA UJERUMANI AWAOMBA MSAMAHA WATANZANIA

Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Dkt.Frank-Walter Steinmeier amewaomba radhi Watanzania kuhusu ukatili wa wajerumani wakati wa  Vita vya MajiMaji na kuahidi kutafuta majibu ya maswali magumu kuhusu vita hivyo ili kujenga mahusiano mazuri zaidi baina ya Tanzania na Ujerumani.

Rais Dkt.Steinmeier ametoa kauli hiyo leo tarehe 1 Novemba 2023 wakati alipotembelea Makumbusho ya Vita vya Majimaji ambapo amejifunza historia ya vita hivyo na kupata fursa ya kutembelea na kuweka shada la maua kwenye kaburi la halaiki la Mashujaa 66 walionyongwa na Wajerumani na kaburi la kiongozi wa vita hivyo Nduna Songea Mbano.


"Vile vile, ana kwa ana, ninaomba msamaha kwa mambo yote ambayo Wajerumani waliwatendea mabibi na mababu zenu hapa" amesema Mhe. Rais.

Amesisitiza kuwa amefurahi kujifunza historia ya Shujaa Songea Mbano kwa undani na kukutana na familia ambapo amesema kinachomgusa ni namna ambavyo Watanzania wanahuzunika kuhusu historia ya Mashujaa na namna ilivyoathiri vizazi vilivyopo.

Ameongeza kuwa ni Wajerumani wachache wanaoifahamu historia ya vita vya Majimaji hivyo amefika katika Makumbusho ili akawaeleze Wajerumani historia ya matukio yaliyotokea huko nyuma kwa lengo la kuendelea kujenga na kuboresha historia njema siku za usoni baina ya Tanzania na Ujerumani.


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Songea Mjini ameomba Serikali ya Ujerumani kujenga jengo kubwa la Makumbusho ya kisasa kuhusu historia ya Vita vya MajiMaji.

Aidha, ameomba ushirikiano baina ya mji wa Songea na mji mwingine wa Ujerumani kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano.

"Tunaamini ushirikiano wa kiuchumi na kijamii ndio utakuwa daraja zuri la kujenga mahusiano mazuri na kuondoa historia mbaya ya siku za nyuma" amesema Dkt. Ndumbaro.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe.Dunstan Kitandula amesema Wizara yake inathamini mchango unaotolewa na Taifa la Ujerumani hususan kwenye  eneo la mafunzo na utafiti mbalimbali kwenye masuala ya  Malikale.

Kitandula amesema kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kwa majadiliano ya namna ya kutumia Vita vya MajiMaji kwa faida ya mataifa yote mawili.


Post a Comment

0 Comments