Madini yenye thamani ya shilingi za kitanzania zaidi ya milioni 961 zenye uzito wa kilogramu 6.93 yakamatwa wilaya ya Chunya , Mkoani Mbeya yakitoroshwa kwenda kuuzwa nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa Oktoba 28, 2023 na Waziri wa Madini Anthony Mavunde akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mbeya katika machimbo ya dhahabu wilayani Chunya.
Mavunde amesema dhahabu iliyokamatwa ina thamani ya zaidi shilingi za kitanzania milioni 961ambapo kama ingetoroshwa Serikali ingekosa mapato ya zaidi shilingi milioni 68.
Akizungumza na wafanyabiashara wa Madini katika soko la madini Mbeya Mavunde amewataka wafanyabiashara wote wa madini kutojihusisha na njama zozote za utoroshaji madini kwani kufanya hivyo kunakosesha mapato ya nchi na kudumaza juhudi za kuleta maendeleo.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira ya dhati ya kuikuza sekta hii ya madini,hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunafanya biashara hii kwa uadilifu,uaminifu na uzalendo mkubwa na pia kwa kuzigangatia.
Wafanyabiashara wa madini nawatangazia tena kuacha kujihusisha na utotoshaji wa madini,tutachukua hatua kali kwa watu wote wanaohusika bila kusita.
Niushukuru uongozi wa Mkoa wa Mbeya chini ya Mkuu wa Mkoa, Juma Homera na uongozi wa Wilaya ya Chunya kwa ushirkiano mkubwa wanaotoa kudhibiti utoroshaji wa madini," alisema Mavunde
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mayeka S. Mayeka amesema kuwa mazingira ya uchimbaji madini wilayani Chunya yanaendelea kuimarishwa isipokuwa changamoto kubwa ni utoroshaji wa madini na wizi wa carbon katika mialo ya uchenjuaji.
Awali, akitoa taarifa kuhusu Sekta ya Madini Wilayani Chunya , Afisa Madini Mkazi Sabahi Nyansiri amesema mpaka sasa vituo vidogo vya ununuzi wa dhahabu 24 vimefunguliwa ili kusogeza huduma ya ununuzi na uuzaji kwa wachimbaji wadogo wasio na uwezo wa kufika katika soko kuu pamoja na wale wenye kiasi kidogo cha dhahabu
Katika ziara hiyo Mavunde amekagua machimbo ya wachimbaji wadogo wa Itumbi na kufanya mkutano kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili.
0 Comments