Hatua ya timu ya Yanga, kuifunga Simba bao 5-1 imesababisha Bi. Amina Narcis Ndunguru (39) - mkazi wa Makoka, Dar es Salaam kunusurika kifo baada ya kujeruhiwa vibaya kwenye jicho la kushoto na Charles Jackob Kulemba anaedaiwa kuwa ni mume wake.
Amina maarufu kwa jina la Mama Vai, Mama wa watoto wanne amelazwa katika Hospitali ya Bochi iliyopo Mbezi kwa Msuguri, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Amina alikutana na kipigo hicho mara baada ya kuonesha furaha ya ushindi wa mabao 5-1 ambao Yanga iliupata kwa kumwadhibu mtani wake wa jadi - Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliofanyika Jumapili Novemba 5, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Amina ni shabiki wa Yanga na Mume wake ni shabiki wa Simba. "Ndugu mwandishi, kilichoniponza mimi ni Yanga, tuliwapiga Makolo 5-1," anasema Amina kwa shida akiwa Wodi ya Wanawake - ghorofa ya pili, Jengo namba mbili hospitalini hapo.
Fausta Ndunguru, mama Mzazi wa Amina, anasema: "Ninyi Waandishi, nimewaita hapa kuelezea uchungu wangu. Huyu ni Binti yangu, uzao wangu wa kwanza. Anapigwa sana na Mume wake, mimi nimechoka... nimechoka. Naona anaelekea kumuua. Naona bora Dunia ijue tu.
"Anapigwa, wanaombana radhi na mimi naombwa radhi. Yanaisha kifamilia, lakini safari hii nimechoka jamani. Oneni jicho la Binti yangu, mimi nimechoka.
"Naomba Serikali, vyama vya siasa vikiongozwa na CCM na watetezi wa haki za binadamu wajue wanisaidie. Nimechoka, tangu wameona Arusha ni vipigo tu," anasema Fausta Ndunguru.
Mama huyo anasema mkwe wake anafanya hayo kwa sababu ndugu zake ni askari mmoja ni mstaafu wa Jeshi na mwingine Ofisa wa Jeshi la polisi.
"Kesi ipo Kimara polisi lakini inazimwa," anasema Mama Fausta aliyelalamika kuuguza kwa gharama kubwa kwa kuwa mume wake pia anauguza ndugu yake huko Mbinga mkoani Ruvuma.
Polisi Kimara wamekiri kupokea malalamiko hayo, lakini wakasema mwenye dhamana ya kutoa taarifa ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.
Juhudi za kumtafuta Kulemba hazikuzaa matunda baada ya mwanahabari kuambiwa kwamba yuko kazini Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
0 Comments