Historia imeandikwa Kardinali wa 3 Mtanzania...
Baba Mtakatifu Francis amempa hadhi ya Ukardinali Askofu Mkuu Protase Rugambwa katika viwanja vya Mt. Petro Vatican leo Septemba 30, 2023.
Leo Maaskofu wakuu 21, wamepewa hadhi ya Ukardinali kutoka nchi mbalimbali duniani. Mmoja wao ni Protase Rugambwa, Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora. Kardinali Rugambwa anakua Mtanzania wa 3 kupata wadhifa huu mkubwa baada ya Baba Askofu Laurean Rugambwa, Mwadhama Polycarp Pengo na sasa Kardinali Protase Rugambwa.
Kardinali Protase Rugambwa ni mzaliwa wa Karagwe, jimbo la Kayanga, kijiji cha Kasheshe, Parokia ya Katojo, katika ukoo wa Abakaraza (Abarigi). Majina yake ya kifamilia ni Protase Abakaraza. Hilo la Rugambwa alipewa kama heshima kwa Askofu Laurean Rugambwa ambaye alifanya ziara Bukoba siku aliyozaliwa Protase.
Baba yake Protase alihama Karagwe akawa anafanya kazi Bukoba. Mama yake alipopata mimba, May 31 mwaka 1960 alijifungua. Siku hiyo Kardinali Laurean Rugambwa alifanya ziara ya kitume Bukoba. Baba yake Laurean akasema kwa kuwa umezaliwa siku ambayo Kardinali Rugambwa amekuja kwetu, basi utaitwa kwa jina lake.
Basi akabatizwa na kuitwa Protase Rugambwa. Na kama ambavyo jina hubeba tabia za mtu, hatimaye nae amekua Kardinali kama mwenye jina lake. Biblia inasema heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi (Mithali 22:1). Kwa hiyo wazazi wapeni watoto wenu majina mazuri kabla ya kuwapa urithi wa mali.
Katika kuonesha mtamgamano wa Kanisa (Church compatibility) Askofu Rugambwa amesindikizwa Vatican na viongozi mbalimbali wa Katoliki na madhehebu mengine. Mmoja wapo ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dr.Benson Bagonza (PhD) ambaye amekwenda Vatican kushuhudia tendo hili kubwa kwa mwana Karagwe mwenzie.
Askofu Bagonza alipopewa nafasi ya kusema neno kuhusu Kardinali Rugambwa amesema "Ni mtu ambaye hekima imemzidi kimo na utu umemtangulia mbele. Ni Mnyenyekevu lakini si Mdhaifu. Mwenye nidhamu lakini si muoga. Makardinali ndio Washauri wakuu wa Papa. Tumuombee Kardinali Rugambwa katika wajibu wake huu mpya wa kuwa Mshauri wa Papa. Roma Locuta, Causa Finita. Roma ikishasema, mjadala unafungwa"
www.radiombiu.co.tz
#RmSautiYaFaraja
0 Comments