Mara zote imekuwa ikielezwa kuwa pamoja na kuwa na kikosi kizuri, lakini mashabiki nao ni sehemu muhimu katika kupata ushindi.
Umuhimu wa unawafanya kutambulika kama mchezaji wa 12.
Sibishani na ukweli huo, ni kweli shabiki ni chachu ya ushindi wa timu mwenyeji popote pale duniani.
Hata hivyo fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa Jumamosi ya Juni 3,2023 nchini Algeria kati ya USM Alger na Yanga ya Tanzania, iliniaminisha kitu kipya zaidi kinachoweza kulinda ushindi wa timu mwenyeji.
Mchezo huo uliisha kwa Yanga kushinda bao 1-0, matokeo yaliyowafanya walikose kombe hilo ambalo pengine ingekuwa ni mara ya kwanza kulichukua.
Yanga ilizidiwa tofauti ya idadi ya magoli ya kufungwa ugenini.
Sasa naamini kuwa waokota mipira (ball boys) ni muhimu sana katika kutafuta matokeo mazuri.
Tukumbuke USMA iliingia kweye mchezo huo ikiwa na akiba ya bao mbili ilizoshinda Kwenye mchezo wa kwanza wa fainali uliopigwa Kwenye uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam, hivyo ilihitaji ushindi wowote, sare ya aina yoyote au kufungwa goli lisilozidi moja.
Yanga yenyewe iliingia ikiwa inahitaji ushindi wa zaidi ya goli moja, sare au ushindi wa bao moja haukuwa na maana kwao zaidi ya kuweka rekodi tu.
Bao mbili za USMA ziliifanya timu hiyo kuwa na uhakika zaidi ya Yanga.
USMA walishaona wamemaliza kazi Dar es Salaam na kwakuwa walijua Yanga si timu nyepesi wakajipanga kwa namna yeyote ile kuishi na matokeo hayo na kama ikitokea wakipata ushindi kwao basi iwe ziada, lakini walijipanga kuhakikisha wapinzani wao hawaondoki na kikombe.
Kwa umoja na uzoefu wao wa kitimu na kikanda, wakaanza kuicheza mechi nje ya uwanja kwa kuifanyia Yanga tashtiti za hapa na pale.
Jambo la kufurahia kikosi chote cha Yanga hakikutaka kuingia kwenye mtego huo, hawakulalamika wala kusononeka zaidi waliweka akili yao kwenye mchezo.
Utulivu wa Yanga uliwavuruga sana wapinzani wao na ndipo walipoamua kutumia mbinu za nje ya uwanja.
WAOKOTA MIPIRA NI SEHEMU YA USHINDI
Kama nilivyoandika hapo juu.
Awali nami nilikuwa nikiamini wakoleza ushindi ni mmashabiki pekee, kumbe sivyo.
Waokota mipira ni watu muhimu sana katika kusaka ushindi.
USMA walilidhihirisha Hilo, waliwatumia vema waokota mipira waliouzunguka uwanja kuhakikisha wanapunguza kasi ya Yanga ambayo iliwashambulia kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.
Ni kama walipangwa maana kwa makusudi kabisa waokota mipira hao waliamua kuuvuruga mchezo ili kuhakikisha wenyeji wanabaki na kikombe.
Walichokuwa wakikifanya ni kuchelewa kurudisha mpira uwanjani na kama wakiurudisha kwa wakati basi walikuwa wakirusha mpira zaidi ya mmoja, kitendo ambacho kinakinzana na sheria za soka.
Walifanya hivyo Kwa kasi katika dakika 20 za mwisho za kipindi cha pili ambacho kilikuwa kigumu sana kwa USMA.
Na kwakuwa nia yao ilikuwa ni kuuvuruga mchezo, hakika walifanikiwa kwani ilimlazimu mwamuzi kusimamisha mchezo mara kwa mara.
Hatua ya mchezo kusimama mara kwa mara ilimkera kocha wa Yanga Nasreddine Nabi pamoja na wachezaji wake jambo lililowafanya wawe wakali hadi baadhi yao pamoja na Nabi kupewa kadi ya njano.
Fitina hizo za waokota mipira, kujiangusha mara kwa mara kwa wachezaji wa USMA na kuwasha mafataki kuliisaidia timu hiyo ya Algeria kupoteza muda mwingi wa mchezo.
Kimsingi mchezo mzima wa fainali ulichezwa kihalali kwa dakika 50 zilizogawanyika katika dakika 25 za kipindi cha kwanza na 25 za kipindi cha pili.
Nje ya dakika 50 hakukuwa na mpira bali mbinu na hila za wenyeji ili kuhakikisha wanalinda kile walichokipata ugenini.
FUNZO
Nilichokishuhudia kwenye mchezo huo kimenipa funzo kubwa na pengine linapaswa kutumiwa na timu zetu za Tanzania zitakazoshiriki michuano ya kimataifa ngazi ya klabu na hata timu ya taifa.
1. Michezo ya kimashindano ya kimataifa haihitaji kumiliki sana mpira, inahitaji matokeo bila kujali unayapataje.
2.Ushindi unatengenezwa katika mchezo wa kwanza, mchezo wa kwanza unapaswa kutumika kwa halali au haramu kusaka matokeo mazuri.
3. Ni kweli mashabiki ni kichocheo cha ushindi, lakini waokota mipira ni muhimu zaidi katika kulinda ulichonacho.
Wao wanaweza kusaidia timu kupoteza muda na hata kumvuruga mpinzani na kuvuruga mchezo.
PONGEZI
Pamoja na mambo yote hayo, kwangu Yanga ni timu bora na nathubutu kumpa pongezi zaidi mlinda mlango wa timu hiyo Djigui Diarra, Nabi na Rais wao Injinia Hersi.
Diarra anajua vema kulinda lango lake na kuanzisha mashambulizi.
Nabi anajua kumsoma mpinzani na kumbadilikia muda wowote.
Hersi ameweza kukifanya kikosi cha Yanga kuwa na utulivu wa mwili na kuamini inaweza kupambana na yeyote.
Hongera Yanga kwa ushindi wa bao moja ugenini, poleni kwa kukosa kombe.
Mategemeo Yangu ni kuona uendevu wa hiki mlichokifanya katika msimu huu.
Aidha mafanikio ya Yanga yawe chachu ya kufanya vizuri kwa timu nyengine na yasiwe chuki ya kutaka kuihujumi.
(c) Jimmy Kiango
0 Comments