Ticker

7/recent/ticker-posts

UNAWEZA KUICHUKIA YANGA, NGUMU KUCHUKIA MAFANIKIO YAKE

Yanga imeionesha Afrika na hata dunia kuwa ni kweli Ligi ya Tanzania Bara ni moja ya ligi 10 bora Afrika.

Kikosi cha Yanga kimeonesha uwezo wake mbele ya wapinzani wake wote iliokutana nao Kwenye michuano ya CAF kwa ngazi ya klabu.

Uongozi wa Yanga chini ya kijana Mhandisi Hersi Said umeonesha dhamira ya dhati ya kuwa na timu yenye kikosi shindani ndani na nje ya Tanzania.

Yanga hii tayari imeshakusanya ngao ya hisani na ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku Ikiwa na michezo mkononi.

Yanga na Nabi tayari iko kwenye hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam na kikubwa zaidi ndani ya msimu hii  imefanikiwa kuvaa medali za juu kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Mafanikio haya si ya kubeza na ukweli ni kwamba hayajaja kama kutema mate kutoka kinywani, ni jitihada na uwekezaji uliofanywa na GSM.

Awali Yanga ilichukuliwa kama timu isiyo na uwezo na michuano ya kimataifa, dhana hiyo ilijengwa na ikajengeka mioyoni mwa wanachama,mashabiki, wapenzi na pengine hata wachezaji na viongozi.

Hersy na wenzake wamefanikiwa kuiondoa hiyo dhana, sasa Yanga ni moja kati ya timu zinazosemwa na kutajwa kwa ubora barani Afrika.

Kwa sasa unaweza kuichukia Yanga, lakini huwezi kuyachukia mafanikio yake.

Yanga imefanikiwa pakubwa msimu huu, imekoleza utamu wa soka la Tanzania.

Ni kweli usiopingika kuwa mafanikio yanatafutwa na yanaandaliwa njia, hayaji kwa kubahatisha.

Bila shaka Yanga imeyatafuta mafanikio haya na hatimae imeyapata.

Kipi muhimu sasa baada ya mafanikio haya, muhimu ni kuhakikisha inayalinda mafanikio haya Ili kuondoa Ile dhana ya kubahatisha.

Viongozi wa Yanga wanapaswa kujua mafanikio haya yamewajengea maadui shindani wengi wa ndani na nje ya nchi.

Zipo klabu nyingi zitajitokeza kutaka kuidhoofisha Yanga kwa kutaka kuwanunua wachezaji wake muhimu na pengine pia kumuhitaji kocha wao, hii isiwavuruge.


Muhimu kwa Yanga ni kuhakikisha haiogopi kukumbana na lolote litakalo jitokeza mbele yake, zaidi inapaswa kukua zaidi kwa kuingia kwenye soko la ushindani la kununua wachezaji wazuri zaidi na kubakiza kwa gharama yeyote wale walio bora kwao.

Yanga ya Hersi haipaswi kuwa Yanga ya kubezwa,kunagazwa na hata kusimangwa kuwa haiwezi kupambana kimataifa.

Yanga hii imewaonesha watani zao wa jadi kuwa hakuna linaloshindikana.

Kwa namna yeyote ile Yanga ya msimu huu wa 2022/23 ni bora na haina deni na wanachama,mashabiki na wapenzi wake.

Inaweza kuwa rahisi kuichukia Yanga kama Yanga, lakini ukiyakumbuka mafanikio yake ya msimu huu ni lazima utapiga saluti.

Nategemea kuiona Yanga kubwa na  bora zaidi kwenye msimu wa 2023/24.

Hata hivyo ukubwa wa Yanga hautakuzwa na wasemaji waropokaji wasio na nidhamu ya kuongea na kuzungumza hadharani.

Yanga hii inahitaji watu waliopevuka zaidi katika kufikiri, kutenda na hata kuongea, Yanga hii siioni kama inastahili kuwa na watu ambao hawajakomaa kichwani.

Yanga hii ni kubwa kuliko ukubwa wenyewe.

(c) Jimmy Kiango

Post a Comment

0 Comments