Ticker

7/recent/ticker-posts

COP30 KIKOSI KAZI CHAUNDWA KUIMARISHA SULUHISHO ZA TABIA NCHI ZINAZOTOKANA NA BAHARI

 

NA JIMMY KIANGO

Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofikia tamati leo, jijini Belem nchini Brazil umefikia uamuzi wa kuunda kikosi kazi maalumu cha kuimarisha suluhisho za tabianchi zinazotokana na bahari.


Nchi waanzilishi wa kikosi kazi hicho ni wenyeji wa mkutano huo nchi ya Brazili pamoja na Ufaransa, hagua iliyoungwa mkono na nchi 17, huku lengo likiwa ni kutafuta suluhu ya safari ndefu ya dunia ya kukabiliana na mabadiliko tabianchi yanayoathiri mazingira ya Bahari huku uzagaaji wa taka ngumu ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu. 


Baada ya majadiliano marefu, Brazil ikiongoza mazungumzo, jumuiya ya kimataifa ilipitisha uamuzi muhimu wa kuundwa kwa kikosi kazi hicho. Hatua hii ilikuwa kama mwanga mweupe katikati ya mawimbi ya changamoto ishara kwamba dunia imeanza kuona bahari na watumiaji wake sio tu kama mwathirika, bali ni kama washirika.


Kikososi kazi hicho kimepewa jina la ‘Kikosi kazi cha Bahari’ ambacho pamoja na mambo mengine kitakuwa na jukumu la kukusanya fedha zitakazotumika kuendesha miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa kwa nchi zinazoendelea

 

Hatua hii inaleta pamoja muungano mpya wa nchi zinazolenga kuimarisha suluhisho za tabianchi zinazotokana na bahari na ni wazi COP30 sasa iko kwenye hatua ya utekelezaji wa kina.

 

Novemba 19,2025 Mkutano wa COP30 uliingia katika hatua yenye shughuli nyingi zaidi katika siku ya tisa, mataifa mengi yalitoa misimamo yao na mazungumzo yakihama kutoka ahadi za jumla hadi utekelezaji halisi.

 

Msisitizo ulijikita kwenye fedha na njia sahihi ya mpito wa haki, huku Brazil ikitangaza hatua kubwa kuhusu bahari, misitu na haki za jamii za asili.

 

Dhamira kuu ni kuhakikisha bahari inakuwa salama, hakuna taka nguvu wala uchafu wowote unaoingia baharini na kwenda kuathiri ikolojia na baionuai ya bahari.


Wajumbe walieleza wazi kuwa bahari inaweza kutuokoa, kupitia nishati safi ya upepo wa baharini, ulinzi wa mikoko na matumbawe, urejeshaji wa mifumo ya ikolojia, na matumizi ya sayansi ya kina kuchochea uchumi wa buluu. 


Lakini hawakusita kutaja ukweli mchungu kuwa bila usimamizi wa pamoja, bila data halisi, bila ufuatiliaji makini, bahari inaweza kupoteza uwezo wake wa kutulinda.


Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi, amesema ingawa hakushiriki moja kwa moja kwenye kikao hicho kilichounda kikosi kazi, lakini anaamini ni hatua muhimu kwa ustawi wa bahari duniani kote.


“Bahari yenyewe haina mipaka, hii mipaka tunaijua sisi binadamu, hii inamaanisha kuwa kama bahari ya Brazili itaharibika ni wazi athari zake hazitaishia huko tu, zitafika mpaka Tanzania, ni muhimu kushirikiana kuilinda bahari,”amesema.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambae pia ni mtaalamu wa Mazingira ya Bahari Dkt.Jestina Katandukila, amebainisha kuwa ni muhimu kwa dunia kuunda kikosi kazi kitakachotafuta suluhisho la kudumu la ulinzi wa bahari na kwamba ni suala ambalo linapaswa kufanywa pia na Tanzania ikiwemo, kwani zipo changamoto za kikanda za utupaji wa taka ngumu hasa za plastiki ambazo zinapaswa kutatuliwa. 


“Tanzania kuna changamoto ndogo ndogo za kikanda, ikiwemo utupaji wa taka ngumu hasa za plastiki; hili linaweza kuendelea kupungua kwa kadri uelewa wa athari zake utakavyoainishwa kwa jamii ya eneo husika au wazalishaji wa taka hizo.”amesema.


Uamuzi wa kuundwa kikosi kazi unatazamwa kama njia sahihi ya kuharakisha utekelezaji wa Mkataba wa Parisi, kwani ripoti ya Climate Change Performance Index (CCPI) 2026 iliyotolewa na Germanwatch, New Climate Institute na Climate Action Network imeonyesha kuwa kasi ya uchukuaji hatua kwa ngazi ya kitaifa ni ndogo, ikishindwa kufikia malengo ya Mkataba wa Paris.

 

Nchi 17 zimeungana na Michango iliyopangwa Kitaifa katika kukabiliana na changamoto za Bahari (Blue Nationally Determined Contribution Challenge-NDC) na Kuunga Mkono Kikosi Kazi cha Bahari. 

 

Kikosi kazi hicho cha ‘Blue NDC Implementation Taskforce’, kimedhamiria kuongeza kasi ya utekelezaji wa suluhisho za bahari,kuunganisha ustahimilivu wa bahari na upanuzi wa nishati safi,kuibua ajira na kuimarisha maisha ya jamii za pwani.

 

TAMKO KUTOKA BAADHI YA MATAIFA

Umoja wa Ulaya (EU), umetaka mchango wa haki katika mpito wa haki,umekosoa kukosekana kwa NDC kutoka kwa wazalishaji wakubwa,umepigia debe mpango wa mpito wa nishati ya kisasa wa Ubelgiji na thamani ya ushuru wa kaboni.

 

New Zealand, imeonyesha hatua zake zinazolingana na 1.5°C,uwazi wa hatua, ahadi za misaada ya marekebisho ya tabianchi.

 

Israel yenyewe imetangaza kuwa uzalishaji wake wa hewa ulishafikia kilele, imesisitiza matumizi ya teknolojia, kilimo kinachostahimili tabianchi na mfumo wa kitaifa wa kupunguza hatari.


Kikosi kazi hiki kipya kitasimama kama daraja kati ya matumaini na utekelezaji. Kitajumuisha wanasayansi, serikali, jamii za pwani, watu wa asili na taasisi za fedha ili kuhakikisha suluhu za baharini zinakuwa za haki, zinazotekelezeka, na zinazonufaisha mataifa yote hasa yale yanayohatarishwa zaidi kama Tanzania, Indonesia na Visiwa vya Pasifiki.

 

Post a Comment

0 Comments