Ticker

7/recent/ticker-posts

OCP YATAKA MAAMUZI YA HARAKA KUIOKOA BAHARI


NA JIMMY KIANGO

Siku 11 za mchakamchaka wa hoja na mijadala katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) zimehitimishwa katika   jiji la Belem nchini Brazil, huku Jukwaa la Bahari na Tabianchi (Ocean & Climate Platform-OCP) likizitaka serikali zote duniani kufanya maamuzi ya haraka katika kuilinda bahari dhidi ya uchafuzi.

OCP ni mtandao wa kimataifa unaounganisha zaidi ya taasisi 115 kutoka asasi za kiraia, ikijumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), taasisi za utafiti, mbuga za baharini,viumbe hai, sekta binafsi, taasisi za umma, mamlaka za ndani na mashirika ya kimataifa.


Jukwaa hili lilianzishwa wakati wa kuelekea COP21 jijini Paris, kwa msaada wa Serikali ya Ufaransa na Tume ya Serikali za Umoja wa Mataifa ya Sayansi ya Bahari (UNESCO-IOC). 

Lengo lake ni kukuza na kuhamasisha maarifa ya kisayansi kuhusu nafasi ya bahari na mifumo ya ikolojia katika mfumo wa tabianchi duniani, pamoja na kutetea ujumuishaji mpana wa uhusiano kati ya bahari, tabianchi na uhai katika maamuzi ya kimataifa.


OCP hutumika kama kiunganishi kati ya sayansi na sera, likitoa nafasi ya majadiliano kati ya jumuiya ya wanasayansi, asasi za kiraia na watunga sera, ili kujenga mtazamo wa pamoja, jumuishi na endelevu kuhusu afya ya bahari katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bayoanuai.


Jukwaa hili linaamini kuwa kipindi cha   mkutano wa COP30 uliokwenda sambamba na miaka 10 ya Mkataba wa Paris,  unapaswa kufungua enzi mpya ya kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko tabianchi kutoka kwenye mwendelezo wa majadiliano kwenda kwenye utekelezaji.


Serikali zinapaswa kuchukua hatua madhubuti, zikishirikiana na wadau wengine zikiwemo sekta binafsi na  asasi zisizo za kiserikali. 


OCP inabainisha wazi kuwa hatua za bahari ni lazima zilingane na mikataba mingine ya kimataifa kama ule wa Mfumo wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Bioanuai wa Montreal (Kunming–Montreal Global Biodiversity Framework), Bioanuau Nje ya Mipaka ya Kitaifa (Biodiversity Beyond National Jurisdiction) na Ajenda 2030.



Mkataba wa Kunming – Montreal Global Biodiversity Framework, unasisitiza kulinda angalau asilimia 30 ya ardhi na bahari ifikapo mwaka 2030, jambo linaloshabihiana na Ajenda 2030 ya umoja wa Mataifa inayolenga maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo.


Kwenye mkataba wa Ajenda 30, OCP inaweka wazi kuwa imesalia miaka mitano ili kukamilika kwa mkataba huo, lakini inaamini kipindi kilichosalia kinaweza kuleta mabadiliko ya mustakabali wa dunia ikiwa kutakuwa na ujasiri wa kisiasa, ushirikiano na maamuzi ya haraka.


Aidha mkataba wa Ajenda 30 unasisitiza kuwepo kwa kinga ya muda mrefu ili kuondokana na mafuta yanayomwagika baharini,ambayo yanaathiri viumbe bahari na kuzuia uingiaji wa taka ngumu baharini ili kujenga uchumi unaoheshimu bahari na kwamba hiyo ndiyo dhana ya ‘One Health’ ikilenga afya ya binadamu, viumbe na mazingira.


MAPENDEKEZO MAKUU YA OCP KWA WATUNGA SERA

OCP inapendekeza kuongezwa ufadhili kwa utafiti na vyuo hasa kwa nchi zenye uwezo mdogo, kushiriki katika miundombinu ya utafiti kwa kutumia Meli za utafiti, mabwawa, maabara na vituo vya uchunguzi na kuimarisha mifumo jumuishi ya ufuatiliaji wa bahari. 


Jukwaa hilo limeainisha vipaumbele vyake katika maeneo saba ya utafiti, ambayo ni Mzunguko wa kaboni baharini, suluhisho asilia (nature-based solutions),Uvuvi endelevu, Afya ya bahari na ustawi wa binadamu, Ikolojia za kina kirefu, Uhimilivu wa Bioanuai zilizo hatarini na Mabadiliko ya njia za viumbe na binadamu (migration).


Aidha OCP inataka kuthamini kwa maarifa ya jamii za asili na jamii za pwani, kuongeza ushiriki wa kijamii katika sayansi (citizen science), kuimarisha elimu ya bahari kwa watoto na vijana, kujenga mabaraza ya kujifunza kwa ushirikiano (communities of practice) na kuunganisha sayansi katika maamuzi yote.


Jukwaa hili linaamini wakati wa ahadi umeisha, sasa ni muda sahihi wa kuchukua hatua na hasa ikizingatiwa kuwa bahari ni chanzo cha suluhisho jumuishi, inadhibiti tabianchi, inatunza viumbe, inalisha mamilioni ya watu duniani na ni injini ya uchumi.


Wakati mkutano wa COP30 ukiwa umefika ukingoni OCP imetoa mapendezo na hatua muhimu za kuchukua ili kuilinda bahari zikiwemo za kusitisha ruzuku kwa mafuta ya mitambo ambayo yanachangia kuchafua mazingira ya bahari, kuzuia miradi mipya ya uchimbaji mafuta na gesi baharini na kupanga mkakati wa kuifungia miundombinu ya mafuta baharini.


Kwa sekta ya usafirishaji kwa kutumia bahari OCP inapendekeza kufikia uzalishaji sifuri wa gesi chafu duniani hadi kufikia mwaka 2050, ambapo kwa sasa inazalisha asilimia tatu ya uzalishaji kulingana na mkataba wa Taasisi ya Kimataifa ya Majini- IMO), kusaidia matumizi ya mafuta mbadala, upepo na teknolojia mpya, kutumia mapato ya ushuru wa kaboni kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko tabianchi, kupunguza kasi za meli na kubadilisha njia, kupunguza uzalishaji na kuweka viwango vya ulinzi wa baionuai katika miradi ya bandari.


Kwa kuhitimisha, ujumbe wa OCP katika mkutano wa COP30 ni wito unaohitaji kufanyiwa kazi kwa haraka na dunia nzima hasa kutambua bahari si tu chanzo cha chakula na uchumi, bali pia ni mhimili wa maisha na ulinzi wa tabianchi. 

 

 

Post a Comment

0 Comments