Ticker

7/recent/ticker-posts

WATU MILIONI 10 KUPOTEZA MAISHA KWA UVIDA NI UGONJWA HATARI ZAIDI YA KANSA


NA JIMMY KIANGO 

Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa (UVIDA) unaosababisha tatizo la maambukizi kwenye damu, unatajwa kuwa hatari na unaoua watu wengi zaidi duniani kuliko maradhi mengi ikiwemo Kansa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), jumla ya watu milioni 4.71 walipoteza maisha mwaka 2021 kutokana na UVIDA, huku likieleza kuwa kwa mwaka 2025 inakadiriwa kuwa bakteria mmoja kwenye bakteria sita  hatibiki kutokana na usugu wa dawa.

 

Mdau wa UVIDA, Bi. Siana Mapunjo ameeleza kuwa ripoti ya WHO imebainisha kuwa kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa tatizo hilo upo uwezekano hadi kufikia mwaka 2050 dunia ikawa inapoteza wastani wa watu milioni 10 kila mwaka, huku ugonjwa wa Kansa ukikadiriwa kuua watu milioni 8.2.

 

HALI ILIVYO KWA TANZANIA

Kwa Tanzania Bi. Siana ameeleza kuwa kati ya watu 236,128 waliougua tatizo hilo mwaka 2021 watu 70,251 walipata maambukizi ya bakteria kwenye damu (Sepsis)  na watu 42,196 walifariki dunia 

 

Watu hao walifariki dunia baada ya dawa kushindwa kuwatibu kutokana na vimelea vya magonjwa waliyokuwa nayo kwua na usugu dhidi ya dawa walizokuwa wanatumia.

 

Bi. Siana ametoa maelezo hayo wakati wa mafunzo maalum yaliyotolewa na Serikali kwa Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya habari nchini Novemba 30,2025, jijini Dar es Salaam.

 

“Idadi hii imetokana na watu waliofanikiwa kufanyiwa uchunguzi kupitia maabara zenye uwezo wa kupima ufanisi wa dawa katika kutibu maradhi.”

 

Aidha alisema kuna watu 9,231 ambao walifariki dunia kwa maambukizi yanayosababishwa na vimelea kama vile bakteria, fangasi au parasiti na virusi, ambavyo vimekataa kutibika kwa dawa za kawaida kutokana na kujenga usugu.

 

Hata hivyo amebainisha kuwa Tanzania iko katika mapambano dhidi ya changamato hiyo na mpango wa mwaka 2023/28 ndio umekuwa ukitumika kupambana na UVIDA.

“Tangu tumeanza mapambano hayo mwaka 2017 tumefanikiwa kubaini changamoto kadhaa, miongoni mwake ni ukosefu wa fedha na uchache wa maabara zenye uwezo wa kubaini changamoto hiyo, ukweli ni kwamba watu wengi wanapoteza maisha kutokana na usugu wa dawa.” Amesema Bi. Siana.

 

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya Bugando-Cuhas, Profesa Jeremiah Semi , ameeleza kuwa nchi inazo maabara zenye uwezo wa kubaini usugu wa vimelea dhidi ya dawa katika ngazi zote za juu, kanda na hospitali za Rufaa za Mikoa.

 

Alisema maabara hizo zipo kwenye hospitali zote za Rufaa za Kanda na za mikoa na kueleza kuwa zote hizo zina uwezo wa kupima hivyo vimelea na kwamba kwa sasa wanakwenda mpaka ngazi za chini ambako kuna hospitali za wilaya.

 

“Najua kipimo hicho kinahitaji fedha nyingi kukinunua, hata hivyo serikali imedhamiria kushusha huduma hiyo mpaka ngazi ya wilaya na tayari zipo hospitali 10 zinazotekeleza mpango mkakati wa ufuatiliaji wa UVIDA.

 

“Mwaka 2020 tulianza na wagonjwa 9,000 na kufikia mwaka 2024 tumefanya ufuatiliaji kwa wagonjwa 49,000.”

 

Mkurugenzi Msaidiziwa Kitengo cha Afya Moja kutoka Ofisi wa Waziri Mkuu, Dkt. Salum Manyata amebainisha kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo kuna haja kwa sekta ya afya kuungana na sekta nyengine ili kulinda usalama wa watu.


 UVIDA NI NINI?

Usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni hali ambapo vimelea vya magonjwa (bakteria, virusi, vimelea/fungus, au parasaiti) vinabadilika na kutoweza kuuawa tena na dawa zilizokuwa zinaviua hapo awali.

 

Mfano: Bakteria wa homa ya matumbo (typhoid) kutotibika tena kwa dawa zilizokuwa zikitibu vizuri miaka ya nyuma.

 

Hii ina maana mgonjwa anaweza kuendelea kuugua au hata kupoteza maisha kwa sababu dawa zimepoteza nguvu dhidi ya vimelea.

 

SABABU ZA UVIDA

Matumizi mabaya ya dawa hii ikiwa na maana ya kunywa dawa bila maelekezo ya daktari, kuacha dawa kabla ya mgonjwa kupona na kutumia dawa zisizo sahihi kwa ugonjwa husika.

 

Sababu nyengine ni matumizi ya dawa kupita kiasi hasa kwa kutumia antibiotics kwa mafua, kikohozi au magonjwa yasiyotokana na bakteria, ununuzi wa dawa bila usimamizi, kutumia dawa zilizonunuliwa kwenye maduka bila vipimo vya kitabibu na matumizi ya antibiotics kwenye kilimo na ufugaji

 

Aidha kutoa antibiotics kwa kuku, ng’ombe au samaki bila usimamizi wa mtaalamu, mazingira machafu, kutupa majitaka au mabaki ya dawa kwenye mazingira, hivyo vimelea kujifunza kuhimili dawa na safari za kimataifa hii huchangia kusafirisha vimelea sugu kutoka nchi moja kwenda nyingine.

 

ATHARI ZA UVIDA

Kwa mgonjwa, Ugonjwa kutopona haraka, Matibabu kuwa magumu na ya gharama kubwa, Kuwekwa hospitalini kwa muda mrefu na hatari ya kifo kuongezeka.

 

Kwa jamii,kusambaa kwa vimelea visivyotibika, kuongezeka kwa mzigo wa kiuchumi kwa familia na serikali na kupoteza ufanisi wa dawa muhimu kwenye hospitali.

 

Kwa uchumi, gharama kubwa za kununua dawa mpya,  na kushuka kwa uzalishaji kutokana na watu kukosa nguvu kazi.

 



DALILI ZA UVIDA

Usugu hauonekani kwa macho, lakini kuna dalili zinazoashiria uwepo wake ikiwemo ugonjwa kutopona hata baada ya kutumia dawa ipasavyo, maambukizi kujirudia mara kwa mara, dawa zilizowahi kufanya kazi hapo awali kuonekana hazisaidii tena na matokeo ya vipimo kuonyesha vimelea haviitiki kwa dawa (antibiogram).

 

NAMNA YA KUEPUKA UVIDA

Mgonjwa anapaswa kutumia dawa kwa maelekezo ya daktari pekee, kumaliza dozi hata kama mgonjwa anajisikia vizuri na asitumie dawa za mtu mwingine.

 

Mgonjwa asinunue antibiotics bila vipimo vya hospitalini, kuosha mikono mara kwa mara ili  kuzuia maambukizi yanayoweza kumlazimu mtu kutumia dawa bila sababu,  kuhakikisha chanjo zinachukuliwa kikamilifu ili kuzuia magonjwa, kutunza usafi wa mazingira na vyoo na kuzuia matumizi holela ya antibiotics kwenye mifugo.

 

Aidha serikali kupitia sekta ya afya inapaswa kusimamia 

uuzaji wa dawa kwa kufuata sheria, kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi na kufanya ufuatiliaji wa vimelea na kiwango chao cha usugu.

 

Ikumbukwe kuwa UVIDA ni tishio kubwa kwa dunia. Ukiachwa bila kudhibitiwa, unaweza kusababisha dawa nyingi kutokuwa na msaada tena. Kila mtu ana jukumu la kuchangia kupunguza tatizo hili,kuanzia mgonjwa, mfugaji, mfamasia, hadi serikali.

 

Post a Comment

0 Comments