NA JIMMY KIANGO
Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofikia tamati leo, jijini Belem nchini Brazil, utakuwa na maana zaidi kama utabadilisha ahadi za kwenye makaratasi kuwa hatua halisi za kiutekelezaji.
Hayo yamesemwa na mtaalamu wa masuala ya Mazingira ya bahari, Dkt. Robert Katekiro katika mahojiano maalum aliyoyafanya na mtandao huu Novemba 19,2025, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Katekiro anasema wakati mkutano huo ukiendelea uhalisia ni kwamba afya ya Bahari inaendelea kudhoofu kila uchwao kutoka na uchafuzi wa mazingira yake unaotokana na shughuli za binadamu hasa uzalishaji mkubwa wa taka ngumu.
Mkutano wa COP30 ulioanza Novemba 10,2025 umehusisha viongozi, wataalamu na wadau wa mazingira, ambapo miongoni mwa mambo waliyoyajadili ni masuala ya uhifadhi wa Ikolojia ya bahari na pwani.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na kasi ya uchafuzi wa Bahari na pwani kutokana na kuingia kwa kiasi kikubwa cha taka ngumu baharini hasa bidhaa za plastiki.
Inakadiriwa kuwa kiasi cha tani zaidi ya milioni 19 hadi 23, kinaingia baharini duniani kote kwa mwaka huku, huku Tanzania ikikadiriwa kuzalisha tani zaidi ya milioni saba na kati ya hizo tani zaidi ya milioni mbili huingia baharini kwa mwaka.
Hali hiyo inaibua hofu kwa bahari, hali inayoisikuma dunia kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana nayo, hata hivyo katika mahojiano maalum Dkt. Katekiro anaweka wazi kuwa mazungumzo na ahadi za kwenye makaratasi pekee hayatoshi na badala yake vitendo vinahitajika zaidi sasa: Endelea.
AFRINEWS:Bila shaka unafuatailia mwenendo wa Mkutano wa COP30?
DKT. KATEKIRO: Asante sana kwa kunifikia kwa maoni kuhusu mwenendo wa mazungumzo ya COP30 yanayoendelea mjini Belém, Brazil.
Ingawa sipo nchini Brazil kimwili, nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mijadala, taarifa za urais (Presidency) wa COP, mikutano ya kiufundi, kazi za makundi ya mawaziri, na pia kushiriki katika baadhi ya side events (mikutano ya pembeni) mtandaoni, hususan zile zinazohusu bahari, uchumi wa buluu, jamii za pwani, na utawala wa rasilimali.
AFRINEWS: Wewe ni mtafiti wa muda mrefu wa mazingira ya bahari, unadhani mkutano wa mwaka huu utaleta mabadiliko yeyote kwenye uhifadhi wa rasilimali za Bahari?
DKT. KATEKIRO: Kama mtafiti na mtaalamu ambaye najihusisha kwa miaka mingi na masuala ya mazingira, tabianchi, maendeleo ya jamii, nishati jadidi na usimamizi wa rasilimali za bahari, ninauona mkutano huu ukiwa ni mwendelezo wa harakati ndefu za dunia kutafuta majibu ya kudumu kwa changamoto ambazo, kwa bahati mbaya, zinaongezeka kwa kasi kuliko maamuzi ya kisiasa na upatikanaji wa kifedha yanayofikiwa.
AFRINEWS: Je, tangu mkutano uanze Novemba 10, hadi sasa, kuna dalili za suluhisho la kudumu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hususan kwa nchi zinazoendelea na zaidi kwenye uchafuzi wa bahari unaotokana na taka ngumu?
DKT. KATEKIRO: Kwa sasa bado hatujaona suluhisho la kudumu, ingawa tumeshuhudia hatua fulani za kisera na kisayansi zinazoonesha mwelekeo wa matumaini ya muda wa kati na mrefu.
Hili si kwa sababu hakuna jitihada, bali kwa sababu masuala yanayojadiliwa kwa mfano upunguzaji wa gesi joto na hewa ya ukaa angani, ufadhili wa tabianchi na mpito wa nishati kutoka mafuta, gesi na makaa ya mawe (nishati chafu/fossil fuels) yanagusa moja kwa moja maslahi makubwa ya kiuchumi.
Na hii si tu kwa mataifa yaliyoendelea, bali pia yale yanayoendelea likiwemo letu ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo waathirika zaidi.
Naweza kusema kwamba katika wiki ya kwanza ya COP ambayo iliishia Jumapili ya Novemba 16, 2025, hoja kubwa iliyojitokeza ni mvutano mkali kuhusiana na fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko tabianchi, maarufu kama ‘adaptation finance’.
Katika mazungumzo ya kuunda vigezo na viashiria vya Lengo la Duniani katika Kukabiliana na mabadiliko tabianchi (Global Goal on Adaptation -GGA), makundi ya nchi zinazoendelea kama Afrika, Amerika ya Kusini na nchi za Kiarabu yameweka wazi msimamo kwamba hawawezi kuendelea kujadili tu viashiria vya kitaalamu bila kujua kwa uhakika vyanzo na ukubwa wa ufadhili utakaopatikana kusaidia utekelezaji wa hatua hizo.
Hali hii imefanya hata rasimu ya maandishi ya mazungumzo iwe imejaa mabano ya maelezo yanayopingana, ikimaanisha kwamba hakuna kipengele kilichokubalika kwa kauli moja hadi sasa.
| Dkt. Katekiro (kulia) akiwa na mwandishi wa makala haya Jimmy Kiango (kushoto) |
AFRINEWS: Kwani makubaliano ya awali yalikuwa ni yapi juu ya ufadhili?
DKT. KATEKIRO: Wakati wa COP26 mwaka 2021 kulikubalika kwamba wafadhili watafikisha angalau dola bilioni 40 kwa mwaka kwa ajili ya kukabiliana na hali ifikapo 2025, tathmini za sasa zinaonesha huenda zikapatikana karibu dola bilioni 25 tu.
Wakati huohuo, makundi ya nchi maskini na zilizo hatarini zaidi yamependekeza malengo mapya ya kifedha kama vile dola bilioni 120 hadi 150 kwa mwaka ifikapo 2030.
Pengo hili kubwa kati ya mahitaji halisi, ahadi za kisiasa na uhalisia wa bajeti za nchi zilizoendelea linaonesha wazi kwamba hatujafikia suluhisho la kudumu.
Aidha, mjadala kuhusu kupunguza gesi joto (mitigation), nao bado upo hatua za awali zinazozingirwa na lugha za kisiasa zaidi.
Nje ya ukumbi wa mkutano kwa mfano, maandamano ya kiraia yamekuwa makubwa, yenye rangi na ujumbe ulio wazi hususan kutoka kwa jamii za kiasili za Amazonia (Indigenous Amazon groups), wanaharakati wa mazingira, vikundi vya kijinsia na vijana wanaohofia mustakabali wa vizazi vyao.
Tumeona hata maigizo ya “mazishi ya coal” kwa maana ya mazishi ya makaa ya mawe, mafuta na gesi, yakionyesha hitaji la dunia ni kuachana na nishati hizi zenye kuchafua mazingira.
Hata hivyo, ndani ya mazungumzo rasmi bado hakuna makubaliano ya wazi kuhusu ratiba ya kupunguza uzalishaji, mustakabali wa uwekezaji katika mafuta, gesi na makaa, au wajibu mahsusi wa nchi tajiri kufadhili mpito wa nishati safi kwenye nchi zinazoendelea.
Hivyo, bado tuko katika hatua ya maneno mazito na misimamo mikali kuliko mipango iliyoainishwa kwa uwazi na yenye uwajibikaji.
AFRINEWS: Kwenye mkutano wa COP29, uliofanyika Baku, Azerbaijan, kuliafikiwa nini na kilichoafikiwa kimetekelezwa?
DKT. KATEKIRO: Hapo ndipo shughuli ilipo, maana naweza kusema sehemu nyingine muhimu ya mazungumzo ni mjadala kuhusu “Baku–Belém Roadmap” inayokusudia kuelekeza dunia kuelekea lengo la kupata dola trilioni 1.3 kwa mwaka kwa ajili ya nchi zinazoendelea ifikapo 2035.
Hata hivyo, hatua tuliyofikia hadi sasa bado ina ukungu mzito, baadhi ya nchi zimesema waraka huu unachanganya kati ya hatua za kusaidia nchi zinazoendelea na mpango mpana wa kubadili mifumo ya kifedha duniani, wengine wanasema ni waraka usio na meno kwa sababu haujawekwa kama maandishi ya mazungumzo yanayojadiliwa rasmi (non-negotiated document).
Matokeo yake ni kwamba bado hakuna uwazi kuhusu ni vipi, lini, na kwa mifumo gani fedha hizi zitatiririka kwa nchi kama Tanzania ambazo ndizo ziko mstari wa mbele kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa gharama kubwa za kijamii na kiuchumi.
AFRINEWS: Unadhani mazingira ya Bahari yanapewa uzito kwenye mikutano ya namna hii na hasa mwaka huu?
DKT. KATEKIRO: Ndio, ni lazima tukiri kwamba, tofauti na miaka ya nyuma, bahari imepewa uzito mkubwa zaidi katika COP30.
Hili linajitokeza kupitia kile kinachoitwa ‘Blue Package’, uteuzi wa wajumbe maalumu wanaohusika na bahari, na ongezeko kubwa la maudhui yanayohusu bahari katika ‘Michango iliyopangwa Kitaifa (Nationally Determined Contributions -NDCs) za nchi mbalimbali.
Kwa sasa na hasa wakati huu wa COP30, ni dhahiri kuwa wengi wanaojihusisha na Bahari wanakiri kuwa idadi ya mara (ngapi) ambazo bahari inatajwa katika hati za NDC imeongezeka maradufu ukilinganisha na miaka iliyopita, na maneno kama “sea level,” “fisheries,” “mangrove,” “coral” na mengine yanayotaja mifumo ikolojia ya bahari sasa yanajitokeza karibu mara nyingi katika nyaraka za nchi wanachama.
Haya ni mafanikio ya kimkakati kwa sababu yanaonesha kwamba bahari haitazamwi tena kama mwathirika tu wa mabadiliko ya tabianchi, bali kama sehemu ya suluhisho hasa kupitia blue carbon, ulinzi wa mifumo ikolojia, nishati mbadala ya baharini na uhimilivu wa jamii za pwani.
AFRINEWS: Pamoja na kutajwa sana kwa bahari kwenye COP30, je, suala la uchafuzi wake unaotokana na taka ngumu umeangaliwa?
DKT. KATEKIRO: Kwakweli hapa, pamoja na hatua hizi chanya, bado tunakabiliwa na pengo moja kubwa sana, mazungumzo haya ya COP30 hayaja ainisha moja kwa moja uchafuzi wa taka ngumu (solid waste) na plastiki baharini (plastic litter) kama kipengele mahsusi ndani ya maandishi ya maamuzi.
Uchafuzi huu mara nyingi unagusiwa kwa namna isiyo ya moja kwa moja kupitia mijadala ya uchumi wa buluu, ulinzi wa bioanuwai na uhimilivu wa jamii za pwani pamoja na usafiri wa baharini (maritime transportation).
Kwa lugha nyingine, mjadala wa bahari umeimarika, lakini suala la taka ngumu baharini ambalo kwa nchi kama Tanzania na nchi nyingi za Pwani ya Afrika Mashariki ni tishio kubwa ambalo halijapatiwa mahali pa wazi katika mfumo wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mfumo wa Mabadiliko tabianchi (United Nations Convention Framework on Climate Change -UNFCCC).
Hili ni eneo ambalo kwa maoni yangu linahitaji kusukumwa zaidi na nchi zinazoendelea, taasisi za utafiti na mashirika ya kikanda kama vile Nairobi Convention na Western Indian Ocean Marine Science Association (WIOMSA).
AFRINEWS: Kuna tumaini la kupata suluhisho la kudumu kwa upande wa Bahari na uchafuzi unaotokana na taka ngumu?
DKT. KATEKIRO: Kuna matumaini ya muda wa kati na mrefu zaidi kuliko ya muda mfupi.
Matumaini hayo yanatokana na mambo kadhaa, kwanza, ajenda ya bahari imeimarika kuliko kipindi chochote tangu COP1, pili, nchi nyingi zinatanguliza bahari katika sera zao za mabadiliko ya tabianchi kupitia NDC na mipango ya kitaifa ya uhimilivu, tatu, kumekuwepo na msukumo mkubwa wa kuwekeza katika blue carbon kama mikoko (mangrove) na nyasi Bahari (seagrass), ambayo si tu inahifadhi kaboni bali pia inalinda bioanuwai na kuchuja taka.
Eneo la nne ni jamii za pwani, hususan za kiasili, zimepata jukwaa la kuzungumza moja kwa moja na viongozi wa dunia, jambo ambalo linaongeza uwazi kuhusu changamoto zinazoanzia ngazi ya kijiji hadi kimataifa.
Hata hivyo, bado hatujaona malengo ya kisheria ndani ya UNFCCC ya kupunguza taka za plastiki, wala mfuko mahsusi wa kusaidia nchi zinazoendelea kupambana na uchafuzi huu kwenye bahari zao.
AFRINEWS: Tanzania inapaswa kufanya nini ili kupunguza changamoto hii inayotishia kasi ya ukuaji wa uchumi wa Buluu?
DKT.KATEKIRO: Tanzania iko kwenye nafasi nyeti sana, tuna ukanda mrefu wa pwani ya Bahari ya Hindi, tunategemea kwa kiwango kikubwa uvuvi mdogo, utalii wa bahari, miundombinu ya bandari, usafiri wa baharini na shughuli nyingine kama ufugaji wa viumbe Bahari (aquaculture).
Ni kweli uchafuzi wa bahari kwa taka ngumu, hususan plastiki zinazoingia kutoka kwenye mito, miji na viwanda, unatishia sio tu mazingira, bali pia kasi ya maendeleo ya uchumi wa buluu.
Kuna maeneo kadhaa ya kipaumbele ambayo ningependekeza Tanzania iyafanyie kazi kwa nguvu zaidi ili kupunguza changamoto hii na kulinda mustakabali wa uchumi wa buluu.
Kwanza, ni kuimarisha mifumo ya udhibiti na ufuatiliaji wa taka ngumu kutoka nchi kavu, tafiti nyingi zinaonesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya taka zinazoishia baharini zinatoka nchi kavu kupitia mito, mifereji na mifumo duni ya ukusanyaji taka mijini.
Hivyo, suala si bahari pekee, bali uendeshaji wa majiji na miji yetu, kuimarisha sheria na taratibu za usimamizi wa taka, kuwekeza kwenye vituo vya kuchakata taka, na kuanzisha mifumo ya uwajibikaji kwa wazalishaji (Extended Producer Responsibility -EPR) ambamo wazalishaji na waingizaji wa bidhaa za plastiki wanawajibika kifedha na kisheria katika mzunguko mzima wa bidhaa zao, ni hatua muhimu sana.
Pili, ni kuwekeza katika miundombinu ya miji ya pwani, maeneo kama Dar es Salaam, Tanga, Bagamoyo, Mtwara na Lindi yanahitaji maboresho makubwa ya mifereji ya maji ya mvua na maji machafu, masoko ya samaki yenye miundombinu bora ya maji safi na mifumo ya taka, pamoja na maeneo rasmi ya kutupa taka yaliyo mbali na vyanzo vya maji.
Bila miundombinu ya aina hii, taka za plastiki, mifuko, chupa na mabaki ya vifungashio vitaendelea kutiririka kuelekea baharini, na kuharibu si tu mazingira bali pia taswira yetu kama nchi inayotaka kuwekeza katika utalii wa bahari, fukwe safi na uvuvi endelevu.
Tatu, Tanzania inapaswa kuhakikisha kwamba ajenda ya uchumi wa buluu inaingizwa kwa uwazi katika NDC, mpango wa Taifa wa uhimilivu (National Adaptation Plan -NAP), na mipango mingine ya kitaifa ya tabianchi.
Bahari haipaswi kutajwa tu kwa ujumla, bali lazima kuwe na malengo mahsusi yanayohusu kulinda mikoko, nyasi bahari, matumbawe, maeneo tengefu ya baharini, pamoja na kuendeleza mbinu shirikishi za usimamizi kama vile Collaborative Fisheries Management Areas (CFMAs).
Kwa kufanya hivyo, Tanzania itaweza kujipambanua kama nchi inayotangaza kwa uwazi mchango wake wa blue carbon na hivyo kuomba kwa uhalali ufadhili wa kimataifa kujenga uhimilivu wa jamii za pwani.
Nne, ni kuwekeza kwa makusudi katika utafiti wa bahari na mifumo ya uchunguzi (ocean observations).
COP30 imeonesha wazi umuhimu wa mifumo kama Biogeochemical-Argo, ufuatiliaji wa DNA ya mazingira (eDNA), matumizi ya satelaiti na mifumo ya tahadhari za mapema ya mawimbi makubwa na vimbunga.
Tanzania inaweza kunufaika kwa kushirikiana na taasisi mbaimbali duniani ikiwemo IOC-UNESCO na UNEP na mashirika mengine ili kuimarisha uwezo wa ndani wa kuchunguza na kufuatilia hali ya bahari, kiwango cha uchafuzi, mabadiliko ya joto, asidi na athari zake kwa wavuvi na jamii za pwani. Bila data thabiti, sera zetu zitakuwa zinabahatisha.
Tano, na pengine muhimu kuliko yote, ni kuwatambua na kuwaweka mbele binadamu wanaoishi na kutegemea Bahari hasa wale wa vijiji vya pwani, wavuvi wadogo, wanawake wanaochakata na kuuza samaki, na vijana wanaojitafutia riziki kupitia shughuli za baharini.
COP30 imeonesha kwa uwazi kwamba kuna uhusiano wa binadamu na bahari ni kiini cha uchumi wa buluu ulio endelevu.
Jamii hizi zinapaswa kuwekwa katikati ya sera, kupitia kuimarisha taasisi kama BMUs na CFMAs, lakini pia kwa kuwajengea uwezo wa kushiriki kwenye majadiliano ya kitaifa kuhusu uchumi wa buluu, mabadiliko ya tabianchi na upangaji wa matumizi ya maeneo ya pwani.
Elimu kwa vijana, utafiti wa kijamii, na ushirikishwaji wa ujuzi wa jadi wa jamii za pwani ni nguzo kuu za uhimilivu wa muda mrefu.
AFRINEWS: COP30 inapaswa kuhitimishwa vipi?
DKT.KATEKIRO: Naweza kusema kwamba COP30 ni hatua muhimu ya mpito kuelekea kile kinachoitwa “implementation COP” yaani mkutano unaotakiwa kubadilisha ahadi za karatasi kuwa hatua halisi.
Tumeshuhudia uamsho na shinikizo kutoka kwa jamii za kiraia, tumeshuhudia bahari ikipewa jukwaa kubwa zaidi, na tumeona nchi zinazoendelea zikipaza sauti kudai haki katika kugawana mzigo wa mabadiliko ya tabianchi.
Lakini pia tumeshuhudia mwendelezo wa mvutano kuhusu fedha, kasi ndogo ya makubaliano kuhusu kupunguza gesi joto, na ukosefu wa maamuzi ya moja kwa moja kuhusu uchafuzi wa bahari kwa taka ngumu.
Kwa Tanzania, fursa iko katika kutumia jukwaa hili kuimarisha misingi ya uchumi wa buluu, kuboresha sheria na mifumo ya usimamizi wa taka, kuwekeza katika utafiti na miundombinu ya pwani, na kuendelea kusukuma mijadala ya kimataifa ili bahari na jamii za pwani zipate nafasi wanayostahili katika maamuzi ya tabianchi.
0 Comments