Kocha wa Yanga, Nasedine Nabi
Nasredine Nabi kocha wa Yanga ambao ndio mabingwa wa soka Tanzania, huyu ndie mtu anayapeswa kutangulizwa mbele ya mafanikio ya timu hiyo ndani ya uwanja.
Nabi ameonesha uwezo wa Hali ya juu sana katika kukinoa na kukipa mbinu kikosi chake.
Yanga ya sasa haikamatiki nyumbani na hata uganini. Inacheza soka la kujiamini, lenye malengo ya kushinda kila mchezo.
Ukweli wa hilo umeonekana kwenye mchezo wao dhidi ya TP Mazembe, uliopigwa mjini Lubumbashi kwenye uwanja wa matajiri hao wa DRC.
Katika mchezo huo Yanga iliwakosa wachezaji wake watano wa kikosi cha kwanza,lakini hakukuwa na tofauti na walifanikiwa kuondoka na alama tatu ugenini.
Yanga ya Nabi inacheza kwa lengo la kusaka ushindi na ziko nyakati kwa jicho la kawaida unaweza kuamini wanacheza hovyo, na hawawezi kushinda, ukweli hauko hivyo.
Timu inabadilika kulingana na nguvu ya mpinzani na ndio maana inakuwa na mabadiliko makubwa na uhakika wa kushinda katika dakika 45 za kipindi cha pili.
Na hivyo ndivyo ilivyofanya ikiwa ugenini nchini DRC, sekunde 42 za dakika ya 62 zilitosha kubadilisha matokeo.
Pasi ya upendo ya Aboubakar Salum kwa Moloko ndio ilikuwa silaha ya kuiangamiza TP Mazembe mbele ya mmiliki wao tajiri Katumbi.
Super sub Fareed Mussa Maliki ndie aliyekuwa mwiba kwa lango la TP Mazembe, kutokana na kuupiga kwa ufundi mpira uliotemwa na mlinda mlango wa mabingwa hao wa zamani wa klabu Bingwa Afrika.
Hii imedhihirisha kuwa Yanga ya sasa haina mchezaji kinara, wote wanaweza kufanya lolote ,muda wowote.
0 Comments