![]() |
| Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga, Kennedy Musonda |
Uwezo huu umeoneshwa na Yanga katika michezo yake yote ya hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Ingawa ilifungwa bao 2-0 kwenye mchezo wake wa kwanza wa kundi D dhidi ya US Monastir ya Tunisia, lakini pia ilicheza mchezo mzuri kama ilivyofanya kwenye michezo yake iliyofuata ukiwemo wa leo dhidi ya US Monastir.
Katika mchezo wa leo Yanga ilianza kwa dhamira ya kusaka alama tatu, huku wapinzani wao wakionekana kusaka alama moja. Ingawa watani zao wanaitania Yanga kuwa nguvu zao ziko kwenye jezi nyeusi, lakini hakuna ubishi wowote kikosi cha Yanga kinacheza soka safi lenye kutoa burudani huku likiwaaminisha mashabiki wake kuwa wataibuka na ushindi.
![]() |
| Mfungaji wa bao la pili la Yanga, Fiston Mayele |
Pamoja na kucheza nyumbani kwenye dimba la Mkapa uliokuwa umelowa maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha leo, Yanga imeweza kuumiliki mchezo huo kwa zaidi ya asilimia 50 tofauti na wapinzani wao ambao walikuwa wakitazamwa kama timu ngumu kwenye kundi D.
Hadi sasa ni Yanga pekee ndio imeweza kuifunga timu hiyo kutoka kwenye kundi lao, mshambuliaji kutoka nchini Zambia Kennedy Musonda ndie alifuta dhana na fikra kuwa timu hiyo ni ngumu baada ya kuwanyanyua mashabikiwa wao katika dakika ya 33 akifunga bao kwa kichwa akimalizia pasi ya Jesus Moloko.
Kikosi cha mabingwa hao wa kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara, hawakuzulika na badala yake iliiona haja ya kuendelea kuzikusanya hela zinazotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwafurahisha mashabiki wake waliofika uwanjani kuwashangilia.
Mayele alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya upendo kutoka kwa Kennedy Musonda na alikimbia na mpira kwa mwendo wa hatua tano kisha kwa wepesi wa hali ya juu aliachia shuti la mguu wa kulia lililokwenda nyavuni moja kwa moja.Kwa matokeo hayo Yanga SC wamefikisha Pointi 10 na kuongoza kundi D wakilingana na US Monastir, lakini wakipishana kwenye idadi ya mabao ya kufungwa.
Alama za Yanga haziwezi kufikiwa na Real Bamako ambayo iko nafasi ya tatu wakiwa na Pointi tano na TP Mazembe wakiburuza mkia kwa Pointi zao tatu, hatua inayowafanya kwenda DRC Congo kumaliza mchezo wa hatua ya Makundi dhidi ya TP Mazembe bila presha.
Matokeo hayo ya Yanga yanaifanya Tanzania kwa mara ya kwanza ikuandika historia kwa kupelekea timu mbili katika mashindano ya CAF baada ya jana Simba SC kutinga hatua ya Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika kwa kuichapa Horoya AC ya Guinnea bao 7-0.



0 Comments