Ticker

7/recent/ticker-posts

SGR KUONGEZA THAMANI YA UTALII MIKUMI

 

Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa Mikumi, Herman Mtei


Na Sidi Mgumia, Mororgoro


Uwepo wa Treni ya Mwendo Kasi ya Umeme (Standard Gauge RailwaysSGR)unatarajiwa kuongeza thamani ya utalii katika Hifadhi ya Taifa Mikumi kwakua itarahisisha ufikaji wa haraka wa watalii hifadhini.


Hayo ni kwa mujibu wa Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa Mikumi, Herman Mtei hivi karibuni mkoani Morogoro alipokuwa akifafanua masuala ya uhifadhi kwa Wahariri waliotembelea hifadhi hiyo ya Taifa.

Wahariri hao kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini walifanya ziara hiyo kama sehemu ya semina ya siku mbili kuanzia Machi 23 hadi 24, 2023 iliyolenga kutoa uelewa juu ya masuala ya bioanuwai iliyoandaliwa kwa ufadhili wa Shirika la Habari la Internews na kuratibiwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Wahariri wakifuatilia kwa makini maelezo wanayopewa na mwenyeji wao 

Mtei alisema kujengwa kwa reli hiyo kutasaidia sana watalii kufika hifadhini kwa haraka na kuweza kurudi pia na treni hiyo baada yakumaliza kufanya utalii wao.

“Ufikaji hifadhini utakuwa ni rahisi sana kwasababu hii reli ya treni ya SGR inakuja Kilosa na Kilosa kuna stesheni kubwa pale kwahiyo na sisi tumeshaanza kufanya taratibu za awali za kufungua geti maeneo ya Kilangali kuhakikisha kwamba mara tu ujenzi wa reli ukikamilika tutaweza kuvuna wageni wengi wanaotoka Dar Es Salaam kwa treni ya mwendo kasi, watapitia kulekule upande wa Kilosa watafanya ‘game drive’ kisha watarudi na treni yao ambayo wamekuja nayo,” alisema Mtei

 

Aliongeza kuwa hii itapunguza changamoto za usafiri kwa watalii wanaokuja kutembelea Hifadhi ya Tiafa Mikumi kwa kuwarahisishia safari yao.

 

Aliongeza kuwa hifadhi hiyo ni rahisi kufikika kutoka Morogoro mjini, Dar es Salaam, Dodoma , Iringa na Mbeya lakini pia ni hifadhi ambayo wanyama wanaonekana kirahisi.


 

“Kutoka Dar es Salaam ni kilomita 238 lakini kutoka Morogoro mjini ni kilomita 107, hifadhi inafikika kwa njia ya ndege ambapo kwa siku moja tunapokea wageni 234, lakini kwa ujumla rekodi ya siku ya watalii wanofika hifadhini ni wageni 1200 kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema Mtei  

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), linafanya jitihada nyingi za kupanua na kuboresha miundombinu ya reli nchini.

Njia ya Reli ya Treni Umeme ya Mwendokasi (SGR) Mradi wa SGR utaanzia Dar es Salaam kisha utapita katika vituo vya Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere, Morogoro, Mkata, Kilosa, Kidete, Gulwe, Igunda, Dodoma, Bahi na Makutopora.

Mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam-Morogoro-Makutopora utatekelezwa katika awamu mbili:  Awamu ya Kwanza ni kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro – kilomita 205, na Awamu ya pili  ni kutoka Morogoro mpaka Makutupora – kilomita 333.

Mtei pia aliwaelezea Wahariri kwa kina masuala yanayoihusu hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na uzuri wake lakini pia changamotoo zinazoikumba kama vile vifo vya wanyama wanaogongwa na magari yaliyo katika mwendo kasi, uelewa wa wanajamii juu ya masuala ya uhifadhi, ujangili na nyinginezo.

“Katika kukabiliana na changamoto hizo tumekuwa tukizishirikisha jamii kwenye masula ya uhifadhi wa bioanuwai kupitia matukio mbalimbali, sherehe za mwisho wa mwaka na kutembelea hifadhi. Pia tunatoa elimu ya uhifadhi kwa shule mbili za sekondari na shule tano za msingi. Tunatoa elimu hiyo pia kwa kuonesha sinema kwa kutumia gari maalumu bila kusahau kutoa fursa kwa wanavikundi kushiriki kikamilifu kupitia vikundi vya TIGP – COCOBA,” alisema Mtei

Pamoja na hayo, Mtei alitaja kuwa mipango mingine madhubuti ya kuzuia vifo vya wanyama wanaogongwa na magari yaliyo katika mwendo kasi ni kuweka geti lenye teknolojia ya kisasa pamoja na kufunga kamera ambazo zitasaidia kufuatilia kwa karibu mienendo ya magari yanayopita kwenye hifadhi.

Akiongea kwa niaba ya wahariri waliofika hifadhini, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dk Ellen Otaru aliipongeza timu ya Mikumi kwa mapokezi mazuri lakini pia kwakuwatembeza katika hifadhi na kujionea vivutio vilivyopo. 

“Tunashukuru sana kwa kutupa fursa mpya ya kuyaelewa masuala yote ya utalii na jinsi hata wanyama pori wanavyoishi katika mazingira haya,” alisema Otaru

 Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dk Ellen Otaru

Kihistoria chimbuko la jina Mikumi, linatokana na mmea unaoitwa Mkoche ambao unaota kwenye ardhi ya unyevunyevu. Wenyeji wa hapo Waluguru, zamani walikuwa wakiita miti hiyo Omikumi wakimaanisha miti inayooota kwenye maji kwahiyo kuanzia hapo eneo hilo likapewa jina la Mikumi na mwishowe hifadhi yenyewe ikaitwa Mikumi.


Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ina vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo ikiwemo, mabwawa ya viboko yaliyosheheni viboko wakubwa wanaofikia ukubwa wa zaidi ya nusu tani, wakiwa sambamba na mamba wakubwa wenye nguvu na urefu wa zaidi ya mita 10.


Wahariri wakipataa maelezo kutoka kwa muongoza wageni 

Pia ndani ya hifadhi hiyo kuna makundi makubwa ya tembo, twiga, nyati, pundamilia, swala, pofu na ndege wa mbalimbaali wakiwemo wakubwa na wadogo.

 


Post a Comment

0 Comments