Na Sidi Mgumia, Morogoro
Wahariri wa vyombo mbalimbali nchini wameshauriwa kuyapa
kipaumbele masuala ya bioanuwai ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuokoa mazigira
kwa ujumla wake.
Ushauri huo ulitolewa hivi
karibuni mkoani Morogoro na Mtaalamu wa Uhifadhi Kiundu Waweru kutoka Shirika
la Habari la Internews
alipokuwa akiongea na wahariri katika semina ya
siku mbili kuanzia Machi 23 hadi 24, 2023 iliyoandaliwa kwa ufadhili wa Shirika
la Habari la Internews na kuratibiwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za
Mazingira Tanzania (JET).
Waweru alisema kuwa bioanuwai (biodiversity) ambayo ni ulimwengu
wa asili unaotuzunguka, na aina mbalimbali za viumbe, mimea, wanyama na wadudu kwenye
sayari yetu, iko hatarini kutoweka kutokana na shughuli za binadamu kama vile
ukataji wa miti, uvuvi, uchafuzi wa hewa, uchimbaji wa madini na mengine mengi
hivyo ni vyema kufanya jitihada za muhimu kutatua changamoto hiyo.
“Kwa waandishi ni vyema kuzipa kipaumbele habari za bioanuwai,
kuziandika kwa kina na ziwe na vyazo vya habari vya uhakika ikiwemo sauti za
wanasayansi, wanajamii, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali,
watunga sera na wengineo, jambo ambalo litawavutia wasomaji lakini wakati huo
huo kutoa na suluhu za kuweza kusaidia wanajamii namna za kupambana na
uharibifu wa mazingira,” alisema Waweru
Kwa upande mwingine ameshauri wahariri kutumia mitandao ya
kijamii kuandika habari zao kwakua sasa teknolojia imekuwa, na ni rahisi sana
kuwafikia wasomaji wengi kwa njia hiyo ukilinganisha na namna ilivyo kwakutumia
magazeti, televisheni na redio.
“Pia ni vyema kufikiri kidunia lakini myafanyie kazi
masuala haya ya mazingira katika ngazi za chini, kitaifa kwakua changamoto za
mazingira zilizopo Tanzania mnazifahamu,” aliongeza Waweru
Waweru amesisitiza pia kuwa upo uwezekano wa kurudishwa kwa bioanuwai katika hali yake ya awali, muhimu ni kuzingatia utunzaji mzuri wa maliasili, sheria ya wadau kuhifadhi, kuheshimu sauti za wanajamii na kuendelea kutoa elimu kwa wazawa juu ya umuhimu wa uhifadhi wa wanyama pori na bioanuwai.
Akichangia mada katika mafunzo
hayo, Mhariri Joyce Shebe kutoka Clouds Media Group alisema kitu cha kwanza ni
lazima wahariri wenyewe wayapende masuala ya mazingira ili iwe rahisi kwa wao
kuwashawishi waandishi wao kuyazingatia masuala ya bioanuwai lakini pia masuala
ya mazingira kwa ujumla.
“Japo changamoto ya mazingira
iliyopo ni kubwa bado waandishi hawana ujuzi na maarifa yakutosha, kwahiyo sisi
kama wahariri tukiyapenda na kuyapa kipaumbele masuala haya itatusaida kupata
namna yakuondokana na changamoto zilizopo pia kuweza kuyaandika kwa ufasaha
kwakua tutakuwa na uelewa wa kutosha na kufahamu ni kipi kinatakiwa kuwafikia
wasomaji,” alisema Shebe
Hata hivyo, Jimmy Charles, Mhariri wa mtandao wa AfriNewsSwahili
amesema wanaunga mkono hoja ya kuyapa kipaumbele masuala ya bioanuwai na
mazingira kwa ujumla wake nia ikiwa ni kueneza uelewa kwa wanajamii juu ya
changamoto zilizopo kwenye mazingira na namna yakuzikabili katika ngazi zote za
taifa.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Utafiti na Ufuatiliaji wa Ikolojia
kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dk Barakaeli Ndosi, amesema kuwa
changamoto kubwa iliyopo katika kukabiliana na biashara haramu ya wanyamapori
ni kwamba majangili wanatumia vifaa vya teknolojia ya kisasa huku wao
wakikabiliwa na upungufu wa vifaa katika kulitekeleza suala zima la mapambano
dhidi ya ujangili.
Akifafanua zaidi juu ya mafunzo hayo kwa
wahariri, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania
(JET), Dk Ellen Otaru alisema lengo kuu ni kuhakikisha upatikanaji wa habari
ambazo ni za uchunguzi zilizoandikwa kwa kina, zenye uwazi na uelewa mkubwa
ambazo zitawafikia kuanzia wananchi, watunga sera na wadau wengine wa masuala
ya mazingira.
“Kikubwa hapa ni kutengeneza mtandao mzuri
wa kazi kwa waandishi kutoka katika mikoa, halmshauri na wilaya mbalimbali pamoja
na wahariri ambao kila mmoja ana nafasi yake katika kazi yake na maeneo husika,
kwa pamoja tunaweza kushirikiana kwa ndani na nje ya nchi ili kuhakisha habari
za mazingira zilizo na ubora wa hali ya juu, uwazi na kina zinapewa kipaumbele
kwenye vyombo vyetu vya habari,” alisema
Semina hiyo ya siku mbili iliambatana na ziara katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, ambapo Wahariri hao kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini walipata fursa yakufahamu kwa kina masuala yanayoihusu hifadhi ikiwa ni pamoja na uzuri wake lakini pia changamotoo zinazoikumba kama vile vifo vya wanyama wanaogongwa na magari yaliyo katika mwendo kasi, uelewa wa wanajamii juu ya masuala ya uhifadhi, ujangili na nyinginezo.
0 Comments