Ticker

7/recent/ticker-posts

JOWUTA YATAKA USHIRIKIANO ZAIDI NA EWURA



 Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Titus Kaguo

NA MWANDISHI WETU

 Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kimeitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),kuendeleza ushirikiano wao ili kuleta tija ya pamoja kwa taifa.

 

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa JOWUTA, Said Mmanga alipozungumza na AFRINEWSSWAHILI mara baada ya kumalizika kwa semina ya siku moja iliyotolewa na EWURA kwa wanachama wa chama hicho, ambayo ililenga kuwaongezea uelewa wanahabari hao juu ya masuala ya udhibiti wa nishati na maji.

 

Mmanga alisema, EWURA ni taasisi kubwa ambayo imebeba maisha ya watanzania, hivyo shughuli zake zinapaswa kujulikana zaidi kwa jamii.

 

“Hawa jamaa wanagusa maisha ya watanzania wote mijini na vijijini maana wao ndio wanadhibiti masuala ya nishati na maji na ukiongelea nishati ni wazi unaongezea mafuta ya petrol, diseli n ahata mafuta ya taa, vyote hivi vinagusa maisha ya watu wote mijini na vijijini.

“Ukiongelea maji ndio kabisa, hapa unayagusa mpaka maisha ya Wanyama, kwa umuhimu wao huu wanapaswa kuwa na ushirikiano wa karibu na vyombo vya Habari na wanahabari na sisi JOWUTA tunawakaribisha, tunaamini huu ni mwanzo tu wa ushirikiano wetu.”

 

Nae Katibu Mkuu wa JOWUTA Suleiman Msuya aliishukuru EWURA kwa mafunzo hayo na kuiomba isichoke kushirikiana nao kwa maslahi ya taifa.

 

Hata hivyo Msuya alitoa rai kwa waandishi wa habari kutumia elimu waliyoipata kutoa taarifa za nishati na maji kwa usahihi zaidi ili jamii ielewe umuhimu wa uwepo wa mamlaka hiyo pamoja na majukumu yake.

 

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Titus Kaguo, aliishukuru JOWUTA kwa kuuona umuhimu wa kushirikiana nao na kuridhia kutoa mafunzo hayo kwa wanachama wake.

 

Katika semina hiyo, Waandishi ambao ni wanachama wa JOWUTA mkoa wa Dar es Salaam, walipewa elimu iliyogusa historia ya EWURA, muundo, majukumu na umuhimu ilionao kwa nchi tangu kuanzishwa kwake.

Naibu Katibu Mkuu wa JOWUTA, Said Mmanga (mbele kulia) akiandika baadhi ya dondoo zilizokuwa zikitolewa na Kaguo kwenye semina hiyo. 

Post a Comment

0 Comments