Ticker

7/recent/ticker-posts

‘WANAOPEWA HUDUMA MBOVU NA TANESCO WANA HAKI YA KUDAI FIDIA’

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, akitoaelimu kwa waandishi wa Habari wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) 

 NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI DSM

Wateja wanaopewa huduma na Shirika la Ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO) wanayo haki ya kudai fidia na kulipwa kama mtoa huduma huyo atashindwa kutoa huduma kwa wakati na  inavyostahili kwa mujibu wa Sheria na kanuni za umeme.

 

Hatua hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wateja, 2001 (The Fair Competition Act) ambayo inalinda haki za wateja dhidi ya huduma duni na inatoa mwongozo wa jinsi fidia inavyopaswa kutolewa kwa wateja wanaopata hasara au usumbufu kutokana na huduma zisizo za kuridhisha.

 

Aidha Kanuni za Huduma za Nishati (The Electricity (Standard of Service) Rules) zilizotungwa chini ya Sheria ya Umeme, 2008, zinaweka viwango vya huduma vinavyopaswa kufuatwa na TANESCO, kama vile muda wa kuunganisha umeme, kushughulikia malalamiko, na kurekebisha matatizo ya umeme.

 

Sheria ya Umeme, 2008 (The Electricity Act, No. 10 of 2008) ambayo inasimamia usimamizi wa sekta ya umeme nchini Tanzania,  inaiwezesha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kudhibiti utoaji wa huduma za umeme, kuhakikisha ushindani wa haki, kudhibiti viwango vya huduma, bei, na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watoa huduma kama TANESCO endapo hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

 

Desemba 13,2024,EWURA iliwataka waandishi wa Habari wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA)mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha inatumia kalamu zao kuwaelimisha wananchi juu ya haki wanazostahili kuzipata pale wanapopata huduma isiyoridhisha kutoka TANESCO.

 


Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, alitoa darasa muhimu kwa waandishi waliohudhuria semina ya siku moja iliyotolewa kwa wanachama wa JOWUTA, kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

 

Kagua alitoa mafunzo ya elimu ya udhibiti wa huduma za nishati na maji kwa waandishi wa Habari kwa dhana kuwa endapo waandishi watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa watoa huduma kutoa huduma stahiki ni rahisi kwa taasisi hiyo kupunguza au kumaliza malalamiko kabisa.

 

“Ndugu zangu waandishi mnapaswa kuielimisha jamii juu ya suala la haki ya huduma, mteja anastahili kupatiwa huduma stahiki wakati wote, sheria na kanuni zipo, kama mtoa huduma hasa TANESCO atashindwa kumuhudumia vema mteja wake, mteja anayo haki ya kushtaki na kudai fidia na anaweza kulipwa,”alisema Kaguo.

 

Kaguo alisema kama ilivyo kwenye umeme, hali iko hivyo pia kwenye huduma ya maji, mteja anastahili kupewa huduma bora na salama na kama mtoa huduma atashindwa kufanya hivyo ipo nafasi kwa mteja kuwasilisha malalamiko yake EWURA na kusikilizwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za maji.

 

Hii inamaanisha EWURA inapata nguvu za kisheria kutoka kwenye Sheria ya EWURA, 2001 na Sheria ya Umeme, 2008, ambazo zinatoa mamlaka kamili ya kuisimamia, kuifuatilia, na kuiwajibisha TANESCO ili kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wateja wake.

 


Post a Comment

0 Comments