Ticker

7/recent/ticker-posts

WANANCHI WASHIRIKI KIKAMILIFU KUANDAA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo

Na Mwandishi Wetu

Katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kwenye kuandaa maendeleo yao, Serikali imefanikiwa kupata maoni ya wananchi zaidi ya milioni moja wakati wa maandalizi wa rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini Dsemba 6,2024, serikali ilitumia njia mbalimbali za kupata maoni ikiwa ni pamoja na kuandaa makongamano 12 na kuwafikia viongozi 44 baadhi yao wakiwa ni wastaafu.

Prof. Kitila amesema kuwa rasimu hiyo ya kwanza inatarajia kuzinduliwa, Desemba 11, 2024 katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar. 

Prof. Mkumbo alisema mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi. 

Ukusanyaji wa maoni hayo kutoka kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi ulianza kufanyika Desemba mwaka jana na Oktoba mwaka huu. 

Wananchi na wadau hao walitoa maoni kwa njia za tafiti katika ngazi ya kaya, ujumbe kwa njia ya simu (USSD), tovuti, makongamano, mahojiano mahsusi na ya kina na viongozi mbalimbali waliopo madarakani na waliostaafu, mikutano na semina na nyaraka zilizokusanywa.

“Uzinduzi wa Rasimu ya Dira 2050 utaenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya kukusanya maoni ya wadau. Awamu hii itahusu maoni ya uhakiki wa Rasimu ya Dira 2050 (validation),” alisema Prof. Mkumbo. 

Alisema zoezi la kukusanya maoni ya uhakiki wake litahitimishwa Januari 18, 2025 kwa Waziri Mkuu kupokea rasimu ya pili ya Dira 2050 iliyoboreshwa kutokana na maoni ya wadau katika hatua ya uhakiki. 

Aliongeza kuwa kati ya Januari na Machi 2025, Rasimu ya Dira 2050 itajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika vyombo vya serikali (Makatibu Wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango na Baraza la Mawaziri).

Baada ya hapo, kati ya Aprili na Mei 2025, Rasimu ya Dira 2050 itapokelewa, kujadiliwa na kuidhinishiwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuizindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwezi Mei/Juni 2025. 

“Maandalizi ya Dira 2050 yanaenda sambamba na maandalizi ya Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Maendeleo (Long-Term Perspective Plan – LTPP) utakaotafsiri maono na matamanio yaliyopo katika Dira 2050,” alisema Prof. Mkumbo.

“Dira hii ni ya Watanzania wote na naomba kuwasihi Watanzania wote washiriki kikamilifu katika hatua zote hadi siku rasmi ya uzinduzi.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile alisema anapenda kuona Tanzania itakayo tengeneza mazingira ya Serikali kuwa na ushirikiano mzuri na vyombo vya habari. 

“Lazima tuwe na utamaduni wa Serikali kuwafikishia wananchi taarifa, na Serikali kupata taarifa kutoka kwa wananchi,” alisema Balile. 

Sanjari na hilo, alieleza shauku yake ya kuona Tanzania inayotoa kipaumbele kwa sekta ya viwanda na elimu bora. 

“Ili tuweze kulipeleka mbele Taifa letu la Tanzania, lazima Dira ya Taifa iwe chombo kinachounganisha Taifa kwa muktadha kuwa mabadiliko yoyote ya viongozi yasije yakapelekea mabadiliko ya vipaumbele vilivyopo kwenye Dira.”

 

Post a Comment

0 Comments