NA MWANDISHI WETU
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua hatua muhimu za kuchunguza na kutatua changamoto zinazouhusu mgogoro wa ardhi na utekelezaji wa uhamaji wa hiari kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni moja ya maeneo muhimu ya kiutalii na urithi wa kimazingira nchini Tanzania.
Awali Rais Samia akizungumza katika mkutano na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai Desemba 1, 2024, Rais Samia aliahidi kuundaa tume mbili muhimu.
Alisema tume ya kwanza itakuwa na jukumu la kufanya tathmini kuhusu masuala ya ardhi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, huku tume ya pili itachunguza utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari kwa wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, na kusambazwa Desemba 24, 2024 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, Rais Samia amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dkt. Gerald Ndika, kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Wajumbe wengine walioteuliwa katika tume hiyo ni pamoja na Philemon Luhanjo, Zakia Hamdani Meghji, Jaji George Mcheche Masaju, Dkt. Richard Muyungi, Balozi Salome Sijaona, Prof. Wilbard Kombe, Prof. Emmanuel Luoga, Mollel James Moringe, na Moi Aprakwa Sikorei.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amemteua Mhandisi Musa Iyombe, Katibu Mkuu Mstaafu, kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Wajumbe wa tume hii ni pamoja na Sihaba Nkinga, Alphayo Kidata, Balozi Valentino Mlowola, Balozi Mohamed Mtonga, Balozi George Madafa, Haruna Masebu, Edward Maura Nduleti, na Rehema Moisare.
Rais Samia amesisitiza kuwa hatua hizi za kuunda tume mbili ni sehemu ya juhudi za serikali kutatua changamoto zinazokumba jamii za wakazi wa Hifadhi ya Ngorongoro na kuhakikisha haki, ustawi, na usawa kwa wote wanaoishi katika eneo hilo lenye urithi wa kimataifa.
Katika hatua hii, Rais Samia aliahidi kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu na viongozi wa jamii, taasisi mbalimbali, na wananchi ili kufanikisha lengo la kulinda haki za ardhi na kuhakikisha uhamaji wa hiari unatekelezwa kwa maslahi ya wananchi na uhifadhi wa mazingira.
Kwa sasa, jamii ya Kimasai inayokaa katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro inakutana na changamoto kubwa za utawala wa ardhi, na Serikali inaendelea kutafuta suluhisho endelevu ili kuboresha hali ya maisha na haki za ardhi kwa wakazi wa eneo hilo.
0 Comments