Ticker

7/recent/ticker-posts

SIMANZI NAMIBIA, RAIS HAGE GEINGOB AFARIKI DUNIA

Rais wa Namibia Hage Geingob amefariki dunia leo asubuhi alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye moja ya Hospitali zilizopo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Windhoek. 

Makamu wa Rais wa Namibia, Nangolo Mbumba alitangaza kuwa Rais Geingob alifariki dunia mapema asubuhi ya leo Jumapili, Februari 4,2024. 

 "Pembeni yake alikuwa mke wake mpendwa mama Monica Geingos na watoto wake," alisema Bwa. Mbumba kwenye taarifa. 

 Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 alikuwa akiugua saratani na yeye mwenyewe aliueleza umma juu ya tatizo hilo mwezi uliopita. 

 Ofisi yake ilitangaza kuwa atasafiri kwenda Marekani kwa matibabu na angerejea Namibia Februari 2,2024. Rais Geingob aliingia madarakani kwa muhula wake wa pili na wa mwisho mwaka 2015. 

Alifanyiwa upasuaji mwaka jana, ambapo mwaka 2014 aliwahi kutangaza kwa umma kuwa alikuwa amepona saratani ya kibofu. Namibia inatarajia kuingia kwenye uchaguzi wa rais na wabunge mwezi Novemba mwaka huu. 

 Chama tawala cha Swapo, ambacho kimekuwa madarakani tangu uhuru mwaka 1990, kilisha mchagua Bi. Nandi-Ndaitwah kama mgombea wake wa urais. 

 Kwa sasa Bi. Nandi ni Naibu Waziri mkuu wa Namibia, na endapo atachaguliwa basi atakuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo.

Post a Comment

0 Comments