KIONGOZI wa Korea Kaskazini Kim Jong-un amelitaka jeshi la nchi yake kuwa tayari kufanya mashambulizi ya nyuklia wakati wowote ili kuzuia vita.
Uamuzi huo unakuja pamoja na shutumu dhidi ya Marekani na Korea Kusini kwa kupanua mazoezi ya pamoja ya kijeshi yanayohusisha nyuklia ya Marekani.
Juzi taifa hili lilieleza kuwa raia wake 800,000 wamejitolea kujiunga na Jeshi la Taifa ili kupatiwa mafunzo ya kivita dhamira ikiwa ni kupambana na Marekani.
Imeelezwa kuwa wananchi wa taifa hilo wanaokadiriwa kufikia 800,000 wameonesha utayari wa kujiandikisha na kulitumikia Jeshi la Taifa ili kukabiliana na Marekani, Gazeti la Serikali la Korea Kaskazini Rodong Sinmun limeripoti taarifa hiyo.
Idadi hiyo ya wananchi inajumuisha wanafunzi na wafanyakazi ilijitokeza siku ya Ijumaa Machi 17,2023.
Madai hayo yamekuja baada ya Korea Kaskazini kurusha kombora la Hwasong-17 (ICBM) ikiwa ni hatua ya kujibu mapigo ya mazoezi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini yanayoendelea.
Kim Jong Un amekuwa akiishutumu Marekani na Korea Kusini kwa kuongeza mvutano baina yao kwa kitendo cha wao kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi.


0 Comments