Na
Sidi Mgumia, Mororgoro
HARAKATI na mapambano mbalimbali yamekuwa yakifanyika nchini
ili kupata njia sahihi ya kumkwamua mwanamke kutoka kwenye umasikini wa mawazo
na utegemezi wa kipato na kuwa na uwezo wa kujisimamia mwenyewe.
Mapambano haya yameanza muda mrefu , juhudi na mikutano
mbalimbali imekuwa ikifanyika ili kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Mwendelezo wa juhudi hizo unaungwa mkono pia na wadau wa
mazingira Tanzania ambao wamejitoa kumkomboa mwanamke kiuchumi kupitia mkakati
wa kutafuta suluhu ya kudumu ya kulinda mazingira na kutatua migogoro kati ya
wanyamapori na binadamu waishio kando ya Hifadhi za Taifa.
Umuhimu huo unawaaibua wanamazingira kutoka Shirika lisilo
la kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) ambao
wanatekeleza mradi wa Shoroba ya Tembo Kilombero katika vijiji vya Mang'ula A,
Sole na Kanyenja.
STEP wamejikita katika mradi huu kwa lengo la kutatua
migogoro kati ya binadamu na wanyamapori lakini pia kumwezesha mwanamke kutimiza
malengo yake hasa ya kujikwamua kiuchumi.
Kwakulitambua hilo, Kim Lim ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Uhusiano kati ya Tembo na Binadamu
kutoka STEP anaeleza ni kwa jinsi gani wameweza kuwafikia wanawake wa vijiji
vya Mang'ula A, Sole na Kanyenja na kuwaelimisha juu ya namna bora
yakujikomboa kuchumi kupitia mradi wa shoroba inayounganisha Hifadhi ya Taifa
ya Nyerere na Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa.
Akiongea na waandishi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari
za Mazingira Tanzania (JET) waliofanya ziara ya siku nne wilayani Kilombero
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na
Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), amesema wameweka uzio wa mizinga ya nyuki ili
kuwazuia Tembo kuingia kwenye mashamba ya wanakijiji.
“Kiujumla ni kwamba mizinga hiyo ya nyuki hutundikwa kwenye
uzio na wanakijiji walio katika vikundi maalumu na kuitunza, wakivuna asali
inakuwa ya kwao huku sisi kama shirika tunawasaidia kupata masoko,” alisema Lim
Kwa kawaida, baada ya kupata taarifa za matukio ya Tembo
zinazokusanywa na vijana maalumu,
wataalamu kutoka STEP huwa wanafika nazo kwa uongozi wa vijiji husika
kuwauliza kama wako tayari kupokea na kuutekeleza mradi wa uzio wa mizinga ya
nyuki kwa ajili ya kuwakabili Tembo.
Baada ya kukubaliana huwa wanaongea pia na wanakijiji wote kwa
ujumla ili wawe wanajua na baada ya hapo huwa wanaunda kikundi na kukisajili
wilayani.
Lim anafafanua kwamba, hiyo ni moja ya fursa kwa wanawake
kuwa katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira lakini pia kuwaweka huru kiuchumi
haswa kupitia mauzo ya asali ya mzinga wanayoisimamia ambayo huuzwa kwa
shilingi 15,000 mpaka 20,000 kwa lita.
Hata hivyo, wameanza kuuza asali kwa kilo ambapo kilo moja
ni shilingi 10,000 na hii ni kwasababu wamegundua kuuza kwa lita wanapata
hasara. Walengwa wao haswa ni wanunuzi watalii kwenye kambi za watalii.
Kulingana na maelezo yake, mpaka sasa wanafanya kazi na
wakulima ni 258 na idadi ya mizinga iliyopo ni 450. Kati yao idadi ya wanawake
ni 133 na wanaume ni 125 ambao wako kwenye vikundi mbalimbali.
Kwa taarifa ya kila mwaka anasema, mwaka 2021 walivuna lita
262.5 na 2022 walivuna lita 406.
“Wakishauza hiyo asali, pesa wanazozipata kama kikundi huwa
wanatafuta mradi mwingine mfano kuna kundi wamenunua shamba la miwa kwahiyo
wanalima kama kikundi. Kwa mwaka jana wameshauza lita 210 za asali kati ya 406
ambazo zilivunwa, mauzo ni yenye thamani ya shilingi milioni 2,010,000,” alisema Lim
Aliongeza kuwa wapo wanakikundi wengine ambao wao wamenunua
viti vya plastiki ambavyo wanakodisha na wengine wameanzisha mradi wa sabuni.
Lim anasisitiza kuwa vikundi vyote vimejiunga na VICOBA (vikundi
vya kuweka na kukopa) pia STEP wanatoa mikopo kwa vikundi na wanarudisha bila
riba, kawaida huwa wanaanza na mikopo ya shilingi 500,000 halafu wanaangalia maendeleo
ya kikundi, wakirejesha vizuri wanaongeza pesa inakuwa shilingi 1,000,000. Kuna
kikundi mpaka hivi sasa wana uwezo wa kukopa mpaka shilingi milioni 3,000,000.
Lakini pia wanatoa pesa kwa waliotoa maeneo yao ambapo kila
kijiji hupatiwa shilingi milioni 10 kila mwaka, ili waweze kufanya miradi ya
maendeleo.
Pia mikopo hiyo bila riba anasisitiza kuwa sio changamoto
kwao kwani kuna usimamizi mzuri na wa karibu wa kila wiki kutoka STEP ambao
unawahamasisha wanavikundi kurudisha pesa kwa wakati. Na kwa ufuatiliaji huo wa
karibu huwa wanaweza kuzitatua changamoto mara tu zinapotokea.
Mafunzo ya mara kwa mara yanayotolewa na STEP huwa pia
yanawasaida sana katika kuhakiskisha mikopo inafanya kazi ipasavyo lakini pia
kurejeshwa kwa wakati kutokanna na wanakijiji kufahamu umuhimu wa kuwa makini
na waminifu kweye mikopo.
“Sisi tunatumia mfumo wa tofauti, hatutumii vitabu vya hisa,
tunatumia simu za mkononi ambazo tunawapatia wanavikundi ambao wanatumia
program maalumu inayoitwa CHOMOKA iliyoanzishwa na Shirika la Care International,
kwahiyo tunawapa mafunzo ya namna yazikutumia, wakati huo huo na sisi tuna
namna yakuangalia maendeleo ya kikundi kupitia programu hiyo hiyo,” alisema Lim
na kuongeza:
“Hii inasaidia kwasababu kuna watu walikuwa hawataki kabisa
kucheza VICOBA kwa mazoea ya mtaani ya watu kutoroka na michango ya wengine,
ama kutolipa mikopo lakini sisi tuna mfumo kabisa ambao kuna fomu maalumu mtu
anajaza, kuna wadhamini, dhamana ambapo tunahakikisha hata mtu akitoroka hawezi
kutoroka na hela ya kikundi.”
Mwaka 2021 kuna mikopo 114 ilitoka na thamani ya hiyo
mikopo ni shilingi milioni 12,900,8000 ambayo ni wao wenyewe wanakijiji
walikuwa wanakopeshana kupitia mifuko ya vikundi vyao, kwa upande wa STEP ilitoa mikopo ya shilingi milioni 3,500,000.
Mwaka 2022 idadi ya mikopo ilikuwa137 na thamani ya mikopo ni shilingi milioni
22,540,000.
Pia wanakikundi hao wanaingiza fedha kwa kuwaruhusu watu
kufanya utalii kutoka ndani na nje ya nchi, kuona uzio wa mizinga ya nyuki,
kujifunza juu ya namna unavyofanya kazi na faida zake lakini baada ya hapo hutoa
kama mchango kidogo ambao unakwenda kwa mfuko wa kikundi kinachosimamia uzio
huo.
Kuchangia
maendeleo ya jamii
Lim alisema kuwa kikundi kinafanya kazi ya kujitolea, wanajitolea
kwenye kujenga vyoo, shule na zahanati. Mfano kijiji cha Kanyenja wamejenga Zahanati
1, Magombera wanajenga Ofisi ya Kijiji huku STEP nao wakitoa pia misaada kama vile mifuko ya simenti na
vinginevyo.
Mwajuma Iddi kutoka kijiji cha
Kanyenja yupo katika kikundi cha wanufaika
wa mradi wa SHOROBA ambao msimamizi wao mkuu ni STEP na ndiye aliyewashawishi
wajiunge na kuwapa mafunzo ya namna yakuweka pesa walizolipwa fidia ili
ziwasaidie.
“Mambo mazuri sasa kwasababu kupitia
vikundi vyetu vinatusaidia tunakopa na kufanya shughuli zetu za maendeleo pia
sasa tuna elimu inayotuelekeza tufanye nini kupitia changamoto tulizonazo kama
vile kutatua shida za karo za shule, matibabu na mengineyo, inatusaidia sana,”
alisema Mwajuma
Naye Mrashi Dongwe mnufaika wa
mradi na mkazi wa kijiji cha Sonjo, Kata ya Mkula na mwanakikundi cha TUNZA
KIKUTUNZE anasema kikundi chake kimemsaidia sana kwakua sasa anaweza kujikimu
yeye na familia yake lakini pia pesa anazopata zinamsaidia sana katika
kuendeleza mashamba yake ya mpunga na miwa
“Utaratibu huu wa vikundi
umetukomboa kwa kiasi kikubwa sana hasa sisi wanawake, kwakua sasa tuko huru
tunaweza kujitegemea na kujiendeleza kiuchumi,” alisema Dongwe
0 Comments