Na
Sidi Mgumia, Morogoro
CHANGAMOTO ya ujangili kwenye hifadhi na mbuga za wanyama
zimeendelea kuzifanya taasisi zinazoangalia maeneo hayo kuendelea kuimarisha
ulinzi.
Moja ya maeneo ambayo yameingizwa kweye mkakati wa kuzuia,
kukabiliana na kudhibiti ujangili ni Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Milima ya
Udzungwa, Abel Peter, ameweka wazi kuwa ulinzi kwenye hifadhi hiyo
umeimarishwa.
Kamishna Peter aliyasema hayo alipoongea na Waandishi wa
Habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) waliofanya
ziara ya siku nne wilayani Kilombero wakitekeleza mradi wa Tuhifadhi Maliasili
unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
“Ujangili bado upo, lakini kuna ulinzi madhubuti ndani ya hifadhi
ambao tunahakikisha kila kitu kipo sawa ikiwa ni pamoja na kulinda Tembo,”
alisema
Aliongeza kuwa hivi karibuni katika maeneo ya Sanche walikamata
meno 12 ambayo ni kutoka kwa tembo sita, pia walikamata meno mengine 3 ambayo
ni kutoka kwa tembo wawili.
Kamishna Peter alisema matukio hayo yamefanyika nje ya
hifadhi, majangili hushughulika na wale Tembo wanaotoka hifadhini kwenda maeneo
mengine.
Alisema wanapata taarifa za ujangili kutoka kwa wanakijiji waishio
kando kando ya hifadhi mara tu baada yakuona ujangili ukitendeka, na wao
huchukua hatua madhubuti mara moja.
Hatua hiyo imetokana na kutoa elimu pamoja na kushirikiana
na jamiina hifadhi imekuwa ikiishirikisha jamii inayoishi kwenye vijiji vilivyo
karibu na hifadhi.
“Tunawaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwalinda
wanyamapori na kuwaambia wana wajibu wa kushiriki mapambano ya kulinda
maliasili zetu kwa kutoa taarifa endapo wataona vitendo vya kijangili
vikiendelea kwenye maeneo yanayowazunguka,” alisema Kamishna Peter
Katika kukabiliana na ujangili, askari wa wanyamapori wanapatiwa
vitendea kazi kupitia Mradi
wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania
(REGROW)
ambavyo vinarahisisha kufanya kazi zao za msingi katika kupambana na ujangili.
Pamoja na changamoto zilizopo, alisitiza kuwa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ambayo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa Shoroba ya Tembo Kilombero ambao unatekelezwa na Shririka lisilo la kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP), bado ni sehemu salama na nzuri kwa watu kwenda kutalii.
Waandishi wa JET wakifurahia mandhari nzuri ya maporomoko ya maji katika Hifadhi ya Udzungwa |
“Hifadhi hii ni eneo maarufu kwa kua na maporomoko ya maji,
viumbe vya pekee, miti inayopatikana hapa tu lakini pia kuna wanyama kama vile Nyati,
Faru na wengineo,” alisema
Hifadhi ina
ukubwa wa kilometra za mraba 1990, na ni hazina ya aina nyingi
za mimea, ndege na wanyama ambao hawapatikani katika sehemu nyingine
yoyote duniani.
Kati ya aina kumi na moja za jamii ya nyani wanaopatikana
katika hifadhi hiyo, mbili hupatikana katika hifadhi hiyo pekee ambao ni Mbega
Wekundu (red colobus monkey) na Sanje (Crested mangabey).
Wapo ndege ambao ni Chozi Bawa Jekundu (rufous-winged
sunbrid) na Kwale wa Udzungwa wanaofanya hifadhi hiyo kuwa ni moja ya
makazi makuu na muhimu ya ndege pori barani Afrika.
Wanyama wengine wanaopatikana ndani ya hifadhi hiyo ni pamoja na Simba, Chui, Nyati na Tembo.
Pia kuna Ua (Flower) liitwalo African Violet ambalo linapatikana ndani ya hifadhi hiyo katikati ya miti mirefu inayofikia mita 30.
Pia kuna Mto Sanje ambao
ni kivutio kikubwa kwakua una maporomoko
ya maji yenye urefu wa mita zipatazo 170 yakianguka
kupitia msituni.
Kamishna Peter
alisema kuhusu utalii, kwa mwaka wanapata wageni 8000, ambao
asilimia 80 ni watalii wa ndani na asilimia 20 ni watalii kutoka nje ya nchi
ambao kwa ujumla wanaingiza jumla ya shilingi milioni 250 mpaka 300 kwa mwaka.
Kwa upande wake Joseph Mwalugelo ambaye ni Meneja wa Shoroba
kutoka STEP alisema wanashirikiana na wadau wa mazingira kama vile Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Serikali
za Vijiji na wadau wengine kuzuia
migogoro kati ya binadamu na wanyama kabla haijatokea.
Mwalugelo alisema wameingia makubaliano kati ya Hifadhi za
Taifa za Udzungwa na Nyerere, wametoa mafuta ya gari ili kusaidia askari
wanyamapori kurudisha Tembo hifadhini ili wasifanye madhara.
“Mwaka huu tumekabidhi gari ambalo TANAPA wametoa,
tumelifanyia matengenezo, litatumika kutatua hizo shida na haswa kuwarudisha Tembo
hifadhini.”
Aliongeza kuwa ili kuleta tija katika ufuatiliaji wa
matukio ya Tembo, wamefunga kamera 18 kwenye shoroba, katika vijiji vya
Kanyenja na Katulukila ambazo kwa mwaka wanakusanya picha zaidi ya 2000, kazi
yake ni kusaidia kujua matukio ya Tembo.
Hii pia imesaidia kwa kiasi kikubwa kuonyesha mwenendo wa
tembo ambapo twakwimu zinaonyesha ongezeko la Tembo, lakini pia kuonyesha kuwa
na wanyama wengine wanapita kwenye shoroba hiyo, kama Swala na Kiboko.
Mwegelo alisema kwa upande mwingine matukio ya ujangili
yamepungua kutokana na juhudi za ulinzi zilizopo katika hifadhi na jamii husika
jambo ambalo linawafanya Tembo kuwa huru kutoka msituni kwa wingi na kwenda
maeneo mbalimbali.
Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wote kwa
ujumla katika juhudi za kuhifadhi wanyamapori kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho.
0 Comments