Ticker

7/recent/ticker-posts

WAZIRI MCHENGERWA AANZA NA TAWA

 



Waziri Mchengerwa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari hayo, sambamba na watendaji wengine wa Wizara yake na TAWA

 

Na Mwandishi wetu

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa ameanza majukumu yake mapya ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii kw kuzindua magari maalum 22 kwa ajili ya kuimarisha shughuli za doria katika vituo 22 vya Mapori ya Akiba na Tengefu na Vituo vya Kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu.

 Amesema  magari hayo pia yanapaswa kutumika   kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi ili kupata taarifa za uhifadhi wa raslimali.

 Uzinduzi huo umefanyika  kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

 Tukio hili ni la  Kwanza mara baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kumteua Mchengerwa kuongoza Wizara hiyo yeye na aliyekuwa Katibu Mkuu wake Dkt. Hassan Abbasi.

 Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa magari haya ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha makamanda na askari kufika katika maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kuimarisha shughuli za doria za kudhibiti ujangili na  wanyamapori wakali na waharibifu.

 Amemshukuru Rais  Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini na kumteua kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii na kutoa magari haya ambapo amewataka kuyatunza ili dhamira ya Rais ya kutaka  kuboresha uhifadhi na kutangaza vivutio vya Utalii ifikiwe.

 

Amemwahidi Rais kuendelea kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ambapo pia ametoa wito kwa watendaji kufanya kazi kwa bidii.

 

Aidha, amemshukuru Rais kwa kutoa kipaombele katika sekta hii kwa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kwa kutengeneza filamu ya Royal Tour.

 

Amefafanua kuwa katika kipindi hiki kila mtendaji wa Wizara anatakiwa  kubadilika na kufanya kazi zaidi ili kuongeza mchango wa sekta hii katika pato la Taifa.

 

Ameongeza kuwa kazi kubwa ni kuhifadhi na kutangaza ambapo ametoa siku tatu kupata taarifa ya taasisi zote chini ya Wizara hiyo.

 

Amewataka watendaji wabadilike,  na wafanye maamuzi badala ya kusubiri na mambo yaharibike.

 

Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,  Mhe. Fatma Mwasi  kupitia kwa  Waziri Mchengerwa ameiomba Serikali kutafakari lengo la kuwataka watumishi wa TAWA kuhamia Dodoma ambapo amesisitiza kuwa kuhamia huko kutadhoofisha uhifadhi wa raslimali za taifa.

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TAWA, Maj. Gen (Mstaafu) Hamis  Semfuko amemhakikishia,  Mhe. Waziri kuendelea kufanya kazi kwa weledi zaidi kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.

 

Katika ziara hiyo Mchengerwa ameambatana na Naibu Waziri, Mary Masanja,  Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Juma  Mkomi.

Post a Comment

0 Comments