Ticker

7/recent/ticker-posts

TANZANIA YAITAKA DUNIA KUTOFANYA MZAHA NA ATHARI ZA MMOMONYOKO WA FUKWE


Mjumbe Maalum na Mshauri wa Rais kuhusu Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Richard Muyungi (Picha zote kwa hisani ya mtandao).

NA. JIMMY KIANGO

Athari za mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira katika ukanda wa Pwani wa Tanzania si jambo la nadharia, ni uhalisia unaoathiri maisha, uchumi na ikolojia ya bahari.


Bahari ambayo zamani ilikuwa chanzo cha riziki, sasa inageuka kuwa kitisho kwa jamii zinazotegemea rasilimali zake.

Kwa mujibu wa ripoti ya Jopo la Serikali mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabianchi (IPCC) kuhusu Tanzania, mmomonyoko wa fukwe, kupanda kwa kiwango cha bahari, na kuharibika kwa mikoko na matumbawe ni miongoni mwa athari zinazotishia maisha ya mamilioni ya Watanzania ambao maisha yao yanategemea rasilimali za bahari.


Haishangazi kwa mvuvi ambaye miaka 10 iliyopita alikuwa na uhakika wa kuvua kilo 50 hadi 00 kwa safari fupi, leo hii analazimika kusafiri umbali mrefu na kuambulia kilo 20 au 30 pekee.

Katika Mkutano wa COP30 unaofanyika Belem, Brazili, Tanzania kupitia Mjumbe Maalum na Mshauri wa Rais kuhusu Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Richard Muyungi, imetoa wito kwa dunia kutotazama kwa jicho la mzaha suala la mmomonyoko wa fukwe.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwito wa kwanza wa maombi ya ufadhili chini ya Mpango wa Utekelezaji wa Barbados (BIM), Dkt. Muyungi alisisitiza kuwa mfuko wa kukabiliana na hasara na uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi (FRLD) lazima uwe wa haki, wa haraka na wenye usawa katika kusaidia mataifa yanayokumbwa na majanga ya tabianchi.


“Kwa Afrika, athari za mabadiliko ya tabianchi si hatari za siku zijazo, ni hali halisi ya kila siku. Mafuriko, ukame, vimbunga na mmomonyoko wa fukwe tayari vinaharibu maisha, riziki na mifumo ya ikolojia ya bara zima,” alisema Dkt. Muyungi.

Mpango wa Barbados umeidhinisha mgawo wa awali wa dola za Marekani milioni 250 kwa ajili ya miradi ya mwaka 2025–2026, ikiwa ni hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa ahadi za kimataifa. Dkt. Muyungi alibainisha matarajio matatu ya bara la Afrika, ambayo rasilimali za kutosha na zinazopatikana kwa uhakika, mfumo wa ufadhili ulio wazi na unaoweza kuongezwa na ukuzaji endelevu wa mfuko kwa mahitaji ya muda mrefu.

Athari za mmomonyono wa fukwe zilizosababishwa na mabadiliko tabianchi.
Kwa Tanzania, utupaji holela wa taka ngumu, hasa plastiki umechangia kuharibu ikolojia ya bahari, ambapo mikoko inakauka, nyasi bahari zinatoweka, matumbawe yanadhoofika na fukwe zinamomonyoka. 

Vitendo hivyo vinasababisha kupungua kwa maeneo ya kuzaliana kwa samaki, kupanda kwa joto la bahari, na hatari kubwa ya mafuriko katika miji ya pwani kama Dar es Salaam, Bagamoyo na Pangani.


Kwa upande wake Shomari Salmini mkazi wa Geza manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam anasema hali ya bahari ni mbaya, hivyo mkutano wa COP30 unapaswa kutoa majawabu ya kudumu na kufanya jitihada za haraka za kuinusuru bahari.

“Hali ni mbaya, sisi tunaoishi kwa kutegemea bahari ndiyo tunajua ubaya wake, leo mvuvi hana uhakika wa Kwenda baharini na kurudi na samaki, maisha yetu yapo hatarini,” alisema.

 

 


Post a Comment

0 Comments