Ticker

7/recent/ticker-posts

ZAIDI YA TANI MILIONI TATU ZA TAKA NGUMU HUISHIA BAHARINI KILA MWAKA TANZANIA

Taka ngumu zikiwa zimezagaa pembezoni mwa fukwe, jijini Dar es Salaam.
NA JIMMY KIANGO
Takribani asilimia 45 hadi 55 ya taka ngumu hasa za plastiki zinazozalishwa nchini kila mwaka zinaishia baharini kutokana na kukosekana kwa njia na miundombinu sahihi ya ukusanyaji na uchakataji wa taka hizo hasa jijini Dar es Salaam, hatua inayoibua wito kwa ujumbe wa Tanzania kuhakikisha unaisimamia kidete agenda ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira ya bahari kwenye Mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko Tabia Nchi (COP30), unaotarajiwa kuanza Novemba 10,2025 jijini Belém nchini Brazil.


Takwimu za Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) zinaonyesha kuwa kila mwaka Tanzania inazalisha kiasi cha tani milioni saba za taka ngumu, huku uwezo wa kuzikusanya na kuzitupa kwa utaratibu stahiki ni kati ya asilimi 45 hadi 55,kati ya asimilia 45 hadi 55 hubaki kwenye mazingira na kuzagaa kwenye mifereji, mito na kuishia baharini na jiji la Dar es Salaam likitajwa kuwa mzalishaji kinara wa taka ngumu nchini, ambapo linakadiriwa kuzalisha kati ya tani 4,100 hadi 5,600 kwa siku.


Hii inamaanisha kuwa katika tani milioni saba za taka ngumu zinazozalishwa nchini, takribani kiasi cha tani milioni 3 hadi milioni 3.5 zinaishia baharini kila mwaka. Hatua hii inachangia kwa kiasi kikubwa kuathiri mazingira ya bahari,fukwe na mifumo ya ikolojia ya bahari kwa ujumla.


Uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya bahari una athari kwa uchumi wa buluu, Samaki na binadamu kwa kuchangia uzalishaji mkubwa wa joto la bahari na kuharibu matumbawe hali inayosababisha kupungua kwa kiwango cha mazalia ya samaki na kushusha kipato cha wavuvi na wachuuzi wakubwa na wadogo wa samaki kutoka kwenye maziwa, mito nag baharini. 


Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP nchini Tanzania, Clara Makenya


Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP nchini Tanzania, Clara Makenya akiwa kwenye Mkutano wa tatu wa Umoja wa Mataiifa kuhusu Bahari UNOC3 uliofanyika mjini Nice, Ufaransa Julai mwaka huu, amesema tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya tani milioni 11 za plastiki huingia baharini kila mwaka na kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2040 endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.


Hatua hiyo inaelezwa kuathiri zaidi ya aina 800 za viumbe wa baharini kwa kumeza mifuko ya plastiki, kunaswa katika taka hizo au kupoteza makazi yao ya asili, Makenya amesema kati ya tani milioni 75 hadi 199 za plastiki zipo ndani ya bahari ulimwenguni kote na zimekuwa zikiathiri kwa kiasi kikubwa jamii za Pwani wakiwemo wavuvi wadogo na wanawake wanaotegemea bahari kwa maisha yao ya kila siku.

Aidha ripoti ya UNEP inaeleza asilimia tisa pekee ya plastiki iliyowahi kuzalishwa nchini ndiyo imeweza kurejerezwa upya hali inayoonyesha changamoto kubwa katika usimamizi kuanzia kwenye ukusanyaji wa taka hizo mitaani nag viwandani.


Makenya ameeleza suala la kutokomeza taka za plastiki linahusisha wadau wote wakiwamo serikali, sekta binafsi na wananchi na kwamba hatua muhimu za kupunguza taka hizo ni kuzirejesha upya kuwezesha kuwa na jamii iliyo salama, mazinzagira na bahari kwa vizazi vijavyo.


Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Waziri Khamis Hamza Khamis amekiri kuwa uzalishaji wa taka ngumu umekuwa ni changamoto kubwa duniani kote hususan katika miji mikubwa kama vile Dar es Salaam na Mwanza nchini Tanzania.

“Takwimu zinaonesha kuwa takribani kiasi cha tani milioni 7 za taka ngumu huzalishwa hapa nchini kwa mwaka, ambapo wastani wa asilimia 45 hadi 50 ya taka hizo ndio hukusanywa na kutupwa kwenye madampo rasmi, huku asilimia 50 hadi 55 hubaki kwenye mazingira na kuzagaa kwenye mito, mifereji na mitaro ya maji ya mvua.” 


Aidha ripoti ya kitaifa ya hali ya ukanda wa pwani (State of the Coast ) ya mwaka 2024 inathibitisha kuwa utupaji wa taka unahujumu mifumo ya ikolojia ya bahari na kuporomosha kasi ya kuufikia uchumi wa buluu.

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akihutumia Mkutano wa CoP29 uliofanyika  Baku nchini Azerbaijan mwaka 2024
UMUHIMU WA MKUTANO WA COP30 KWA  MAZINGIRA YA BAHARI
Ili kuinusuru bahari na changamoto hii ya taka ngumu Tanzania inashauriwa kuutumia vema COP30 ambalo ni jukwaa rasmi la kimataifa kwa ajili ya kujadili na kuamua malengo ya kukataa uzalishaji wa hewa ukaa, kutafuta ufadhili wa fedha za kukabiliana na madhara ya mabadiliko tabianchi na kufikia makubaliano ya kimataifa yanayoathiri sera za kitaifa za utekelezaji wake kama vile mkataba wa Kyoto na Paris, kutafuta uwezeshwaji katika mapambano dhidi ya uchafuzi wa bahari.


Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo kwa mazingira ya bahari, mito na maziwa  Mhadhiri na mtafiti wa masuala ya Mabadiliko Tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha SAUT, Dkt. Aidan Msafiri, amesema kuna haja ya ujumbe wa Tanzania unaokwenda COP30 kuhakikisha wameibeba agenda ya uchafuzi wa mazingira ya bahari kwa utupaji wa taka ngumu usiozingatia sheria.


"Ujumbe wetu unaokwenda COP30 unapaswa kulichukua suala hili kama agenda ya dharura. Pengine wavitumie vikao vya pembeni (side events) kuhakikisha wanaieleza dunia juu ya hatari hii inayotukabili," alisisitiza Dkt. Msafiri.

Kwa upande wake Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mkurugenzi wa NEMC, amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa agenda ya Nishati safi ya kupikia, lakini anaamini suala la uharibifu wa mazingira ya bahari ni miongoni mwa agenda muhimu zitakazobebwa na ujumbe wa Tanzania kwenye COP30.

 

"Hili ni suala la dunia. Bahari haipo Tanzania tu, ipo maeneo mengi Afrika na duniani, hivyo tunataka tulifanye jambo hili kuwa la Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa ujumla," alisisitiza Dkt. Semesi.


Mwenyekiti wa AGN, (African Group of Negotiators) ambalo ni Kundi la Majadilino la wataalamu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kutoka Afrika kwenye COP30, Dkt. Richard Muyungi, amebainisha kuwa mkutano huo ni muhimu kwa Tanzania kwani utasaidia kuifanya changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi kuwa faida kwa nchi.


“Dhamira ni kufanya mabadiliko ya tabia nchi kuwa faida kwa nchi, kuna agenda ambazo Rais amekuwa akizibeba, agenda kubwa ni Nishati safi ya kupikia na agenda hii tutaibeba  katika mkutano wa Belem na tayari kama Afrika tumesema ndio moja ya agenda kubwa ambayo tutakwenda nayo. Hata Brazili yenyewe imeweka kwenye maeneo ya vipaumbele, tunayo agenda pia ya kuwaunganisha Waafrika milioni 300 wanaunganishwa na umeme ifikapo 2030.


“Agenda hizi zote ziko chini ya usimamizi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na tayari Umoja wa Afrika umeridhia aendelee kuzisimamia, jambo la kushuruku ni kwamba Rais pamoja nag kuwa msaada kwa nchi, lakini pia amekuwa ni dira kwa Afrika.” 


Pamoja na umuhimu wa agenda hizo alizozisema Dkt. Muyungi, baadhi ya Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Bahari , wanaiomba serikali kuitilia mkazo agenda ya kutafuta suluhu ya tatizo la uchafuzi wa mazingira ya Bahari.


HITAJI LA WANANCHI KWA SERIKALI

Wakazi wa ukanda wa Pwani ya Kigamboni, Dar es Salaam, wao wameitaka Serikali ya Tanzania na wadau wa mazingira kuutumia mkutano huo kusimamia kwa dhati hoja ya uharibifu wa Mazingira ya Bahari unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na utupaji wa taka ngumu, hasa chupa za plastiki. 


Uchafuzi huo unatajwa kuzidisha athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya Pwani, huku umasikini wa wavuvi na wafanyabiashara wa samaki ukiongezeka kutokana na kupotea kwa viumbe bahari hao.


Wakizungumza na AfrinewsSwahili mwanzoni mwa wiki hii, baadhi ya wakazi wa Mbwamaji na Tungi, wilayani Kigamboni, Dar es Salaam,walikiri kutojua chochote kuhusu mkutano huo muhimu wa COP30. Hata hivyo, walipoelezwa umuhimu wake katika kuikabili changamoto ya mabadiliko tabianchi, walisisitiza kuwa ujumbe wa Tanzania unapaswa kuwasilisha kwa dunia janga la taka za plastiki na athari zake.


UHARIBIFU WA IKOLOJIA YA BAHARI

Yohana Rwehemeja, mkazi wa eneo hilo, ameiambia AfrinewsSwahili kuwa hali ya mazingira ya Bahari kwa sasa si nzuri hasa katika maeneo ya ufukwe ambapo chupa za plastiki zimezagaa kwa kiwango kikubwa. 


Amesema hali hii inaathiri ukuaji wa miti ya mikoko na kuvuruga uoto wa asili wa Matumbawe ambayo ni mifumo ikolojia muhimu kwa maisha endelevu ya Samaki Pamoja nag kulinda pwani dhidi ya mmomonyoko wa kingo za bahari unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.


"Chupa za plastiki ni tatizo. Zimezagaa sana kwenye eneo kubwa la fukwe ya Kigamboni. Mbaya zaidi, chupa nyingi zinazoonekana ni zile ambazo hazifai kurejeleshwa, mara nyingi huwa ni  za vinywaji vya kuongeza nguvu, hizi chupa zinadumu kwa muda mrefu na kwa kiasi kikubwa zinaingia baharini na kuathiri viumbe vya bahari na mazingira ya ndani na nje ya bahari kwa ujumla," alisisitiza Rwehemeja.


Juma Hassan, mfanyakazi wa Hoteli ya Mbongwe, alieleza kuwa wanakusanya kiasi kikubwa mno cha taka ngumu kila siku kutoka ufukweni. "Siwezi kusema kiwango cha ujazo kwa namba, ila ni kiasi kikubwa tunachokizoa kila siku," alisema.


Aliongeza kuwa, "Nadhani hiyo COP30 ni muhimu na ni vema watakaotuwakilisha wasiende kushangaa majengo marefu, badala yake wakawe wawakilishi wa kweli ili kuiokoa bahari."


KUPUNGUA KWA SAMAKI NA  ATHARI ZA KIUCHUMI
Mariam Kaulime, mfanyabiashara wa Samaki, katika soko la Feri, Kigambani anathibitisha kuwa biashara yake inazidi kuwa mbaya, akilinganisha hali ilivyokuwa miaka mitano hadi 10 iliyopita na sasa, ameeleza kuwa bei ya samaki imepanda kwa asilimia kubwa kutokana na upatikanaji wake kuwa mgumu.


"Miaka ya nyuma upatikanaji wa Samaki ulikuwa wa kiwango cha juu. Kwa sasa, ndoo moja ya lita 20 iliyojaa samaki wadogo inaweza kununuliwa kwa Shilingi 75,000 hadi 90,000, wakati miaka mitano iliyopita tulikuwa tukiinunua kwa Shilingi 30,000 hadi 50,000," alisema Kaulime. 


Hali hiyo inatokana na uchafuzi wa mazingira ya bahari ambapo makazi ya samaki yamevurugwa na sababu ikiwa ni uwepo wa taka ngumu,ukataji wa mikoko na uvuvi haramu, hivyo wavuvi wanalazimika kwenda mbali zaidi.


Mmoja wa wavuvi wanaoendesha shughuli zao Kigamboni, ambae ni mvuvi wa kutumia jahazi la kusukuma kwa kasia, alikiri kuwepo kwa ugumu katika kupata Samaki na kuishauri Serikali kuchukua hatua za haraka. 


"Mimi sijui lolote kuhusu huyo COP30, lakini kama ni eneo linaloweza kutumika kuikoa bahari na uchafuzi wa mazingira, basi itusaidie. Kwa sasa huwezi kurudi pwani na kiasi kikubwa cha samaki , tofauti na huko nyuma, tulikuwa hatuendi mbali kuvua Samaki, lakini sasa hivi tunalazimika kwenda umbali mrefu na hata huko mbali mnakokwenda, hakuna uhakika, wenye uhakika ni wale wenye kutumia majahazi yenye mashine."


Post a Comment

0 Comments