Ticker

7/recent/ticker-posts

COP30: SI WAKATI WA MANENO NI MUDA WA KUTEKELEZA AHADI KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI


Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Simon Stiell,(Picha kwa hisani ya mitandao).
NA. JIMMY KIANGO
Bahari ni uti wa mgongo wa maisha ya binadamu kiuchumi, kitamaduni, na kimazingira, mifumo ya ikolojia ya bahari inaendesha uchumi kupitia uvuvi, utalii, na usafiri wa majini. 

Ni mdhibiti muhimu wa hali ya hewa duniani, ikinyonya takriban asilimia 30 ya hewa ya ukaa na zaidi ya asilimia 90 ya joto la ziada linalozalishwa na gesi chafu.


Kwa bahati mbaya, mifumo hii ya maisha inazidi kutishiwa na ongezeko la joto, asidi baharini na uchafuzi wa mazingira, utupaji holela wa taka ngumu hasa za plastiki unatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa.

Kupitishwa kwa Mkataba wa Bahari Kuu (High Seas Treaty) na hatua ya dunia kukutana Brazili kwenye Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofanyika Brazili, unaweza kusaidia uimarishaji wa ulinzi wa sayari na jamii kwa kuzingatia misitu, bahari na bionuwai na kuweza kusaidia kuleta mabadiliko chanya.

 

Kwenye mkutano wa CoP30, pamoja na mambo mengine, wataalamu watatafuta suluhisho jumuishi linaloendana na hali halisi ya ulinzi wa bahari likibeba makundi mbalimbali yakiwemo ya watu wanaoishi kwa kuzingatia asili na tamaduni zao, watoto, vijana, wajasiriamali wadogo na wa kati. 


Hii ni hatua muhimu katika usimamizi wa bahari duniani mkutano huo unaweza kuwa chachu ya kurahisisha ulinzi mkubwa wa viumbe hai vya baharini kwa ngazi ya kitaifa, kuwezesha kuanzishwa kwa maeneo teule ya baharini (Marine Protected Areas), na kuimarisha utunzaji endelevu wa bahari. 


Ni mkutano muhimu utakaosaidia kuunga mkono makubaliano ya mkataba wa Bahari Kuu kwa kulinganisha hatua za hali ya hewa na uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za baharini, ikitambua jukumu muhimu la mifumo ya bahari yenye afya katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhimili na kujenga ustahimilivu.

NI WAKATI WA KUTENDA 
Viongozi wa dunia katika Mkutano COP30, tayari wamefufua wito wa kuchukua hatua za haraka na kwa umoja ili kulinda watu na sayari, wakisisitiza kuwa ni wakati wa nchi kuhamia kutoka kwenye ahadi hadi utekelezaji kwa sababu athari za tabianchi zinazidi kuongezeka.


Mkutano huo, umefunguliwa kwa ujumbe wenye nguvu ya matumaini, utamaduni, na azimio kutoka kwa viongozi wa kimataifa na kitaifa kutoka nchi mbalimbali duniani.


Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Novemba 10, 2025, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Simon Stiell, alisema Mkataba wa Paris uliunda injini ya maendeleo ya tabianchi, lakini akaonya kuwa sasa ni wakati wa “kukanyaga mafuta” kwa ajili ya ustawi wa watu na sayari.


Alizitaka serikali za mataifa yaliyoendelea kubadilisha ahadi kuwa vitendo halisi kupitia sera zinazounda masoko, ufadhili unaotoa matokeo yanayopimika, na suluhisho zinazoboresha maisha ya watu moja kwa moja.

“Mchakato huu wa COP unahusu watu, watu ambao huenda hawafuatilii kila majadiliano, lakini wanaona matokeo ya kuongezeka kwa majanga, bei ya chakula, gharama za bima, na bili za nishati zinaongezeka kila kunapokuwa na ukame, mafuriko, dhoruba, au joto kali,” alisema Stiell.


Stiell aliahidi kushirikiana kwa karibu na Rais wa COP30 kuhakikisha matokeo bora zaidi, akisisitiza haja ya kushughulikia masuala magumu bila kuchelewa. Aidha aliwakumbusha viongozi kuwa dunia inatazama kuona kama mkutano wa mwaka huu utaweza kubadilisha maneno kuwa vitendo na hotuba kuwa suluhisho.


“Huu ni mkutano wangu wa nne wa COP nikiwa Katibu Mtendaji, kila mkutano uliopita umeleta matokeo halisi, nchi ziliweza kushinda tofauti zao na kuusogeza ulimwengu mbele. Tunapaswa kufanya hivyo tena,” alisisitiza.


Alibainisha kuwa mpito wa dunia kuelekea nishati safi na ukuaji endelevu lazima uwe wa haki na jumuishi.

“Tutashinda mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi endapo watu wote katika mataifa yote watanufaika kwa usawa kutokana na faida kubwa zinazotokana na mabadiliko haya,” alieleza.


Stiell alisisitiza kwamba COP30 si mkutano wa kawaida wa kila mwaka, bali ni wakati wa uwajibikaji. Miaka 10 baada ya Mkataba wa Paris, dunia inashuhudia viwango vya juu vya joto, ukame mkali, na pengo linaloongezeka la usawa hali inayofanya utekelezaji kuwa wa dharura zaidi kuliko hapo awali.


Rais wa COP30, Balozi André Corrêa do Lago, alisema ufunguzi wa mkutano ni kama maajabu yanayogusa moyo, ambapo amelitaja onesho la kiutamaduni lililotolewa na Watu wa Asili kuwa ishara yenye nguvu ya uhusiano wa kina kati ya binadamu, asili na utamaduni.


“Nimefurahishwa sana na asubuhi hii ya kwanza, tulikuwa na ufunguzi mzuri uliopambwa na nyimbo nzuri za watu wa asili ya Brazili, ilinigusa sana,” alisema.

Pia alipongeza ujumbe wa nchi mbalimbali kwa kukubaliana juu ya ajenda ya mkutano baada ya majadiliano ya usiku kucha, akilitaja hilo kuwa ni mafanikio makubwa yatakayowezesha mkutano kuanza kazi kwa kasi.

Mkurugenzi Mtendaji wa HUDEFO, Sarah Pima,
TANZANIA INAKUMBANA NA ATHARI ZA MMOMONYOKO WA FUKWE
Mkurugenzi Mtendaji wa HUDEFO, Sarah Pima, akizunggumza alizitaka nchi washiriki kuhakikisha makubaliano yatakayofikiwa katika COP30 yanatafsiriwa katika utekelezaji wa vitendo. 


Alisema mataifa kama Tanzania tayari yanakumbana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame na mmomonyoko wa fukwe katika maeneo kama Dodoma, Bagamoyo na Singida.

“Athari za mabadiliko tabianchi tayari zinavuruga maisha na usalama wa chakula, Watanzania wengi, kama ilivyo kwa mamilioni ya watu duniani, wanasubiri viongozi wa dunia kubadilisha ahadi kuwa suluhisho halisi,” alisema.



Post a Comment

0 Comments