NA. JIMMY KIANGO
Jua lilikuwa ni kali kwenye ufukwe wa pwani ya Kunduchi, jijini Dar es Salaam, mawimbi yalikuwa yakigonga kwa upole mchanga mweupe uliosambaa kwenye eneo kubwa la ufukwe wa bahari, cha kustaajabisha kilikuwa ni utofauti wa rangi ya maji ya bahari, badala ya maji hayo kung’aa kwa uzuri wake wa asili, yalionekana kutawaliwa na rangi isiyo yake.
Hali hiyo ilisababishwa na uchafu uliokuwa ukisukumwa na maji ya Bahari, vipande vya taka za plastiki, chupa zilizotupwa, mifuko milaini iliyoanikizwa kwa rangi tofauti tofauti za bluu, nyeupe na nyeusi, vipande vya miti, nyasi, na matambara ya nguo chakavu ni miongoni mwa taka ngumu zilizokuwa zikishindana na maji ya bahari kusukumwa nje. Bahari ilionekana kama inatumia nguvu kubwa kujisafisha.
Asha Makalala, mwanamke wa umri wa miaka 38 anayeuza samaki wa kukaanga katika eneo la Basihaya, alisimama akitazama maji hayo. Kwa huzuni alisema: kati ya mwaka 2005 na 2010 tulikuwa tukipata samaki wengi mnadani kwa bei rahisi. Siku hizi, hali ni tofauti, hata dagaa wamepungua, tunaambiwa taka nguvu zinaharibu mazalia ya samaki hali inayosababisha wasizalieni sana.”
Huo ndio ukweli mchungu unaoikumba Tanzania na dunia nzima kwa ujumla,uchafuzi wa bahari unaosababishwa na taka ngumu, hasa plastiki, umefikia kiwango cha kutisha.
Tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya tani milioni saba za taka ngumu hutupwa kila mwaka nchini Tanzania, na karibu asilimia 45 hadi 55 huishia baharini huku mifuko na chupa za plastiki huzuia mifereji, huharibu mandhari ya utalii, na kuua viumbe vya majini kama kasa, papa na samaki wadogo.
Aidha ripoti iliyotolewa mwaka 2022 na Shirika la kimataifa la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) ilieleza kuwa kama hakutakuwa na jitihada za makusudi za urejelezaji wa taka za plastiki, hadi kufikia mwaka 2060 uzalishaji wa taka za plastiki duniani kwa mwaka utafikia tani bilioni 1.2 ambazo ni karibu mara tatu ya kiasi cha uzalishaji wa sasa.
Wavuvi wanalalamika kuwa wanalazimika kwenda mbali zaidi baharini kufuata samaki, hali hii imepunguza kipato cha familia nyingi zinazotegemea uvuvi, pamoja nag kuwepo kwa jitihada za kusafisha fukwe, lakini sekta ya utalii ambayo ni mojawapo ya injini kuu za uchumi inakabiliwa na changamoto ya kupoteza wageni kutokana na uchafu katika fukwe.
ATHARI KWA WANANCHI NA AFYA
Wananchi wengi hawajui kuwa taka hizo za plastiki zinapovunjika na kuwa microplastics ambazo huishia kwenye maji ya kunywa na kwenye samaki ambayo humuathiri mlaji. “Tunachokula leo kinaweza kuwa sumu kesho. Plastiki haziozi, zinabaki kwenye mazingira kwa mamia ya miaka, zikiathiri afya ya udongo.” Anasema Dkt. Festo Mavika.
UMUHIMU WA USHIRIKI WA TANZANIA COP30
Wakati dunia inakutana Belém, Brazil, kwenye Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko Tabianchi (COP30), Tanzania inakuwa na nafasi ya kipekee. Huu si mkutano tu wa viongozi bali ni jukwaa la kusikiliza sauti ya bahari na jamii za pwani ambazo zinabeba gharama ya uchafuzi huu.
Kwa kushiriki kikamilifu COP30, Tanzania inaweza kusisitiza haja ya ufadhili wa kimataifa kusaidia nchi zinazoendelea katika kudhibiti taka za plastiki na mabadiliko ya tabianchi.
Kukuza teknolojia za kuchakata taka na kuhamasisha matumizi ya plastiki mbadala, kulinda maisha ya wavuvi na wanawake wa pwani, wanaoathirika zaidi na kupungua kwa samaki, kushirikisha sauti za vijana, kama Asha na wenzake, wanaoona athari hizi kwa macho yao kila siku.
Ukweli ni kwamba Bahari haijawahi kuongea, lakini sasa inalilia msaada kutokana na mikondo yake kubeba chupa, mifuko, na taka kutoka kwenye miji yetu, bahari inabeba ukimya wa viumbe waliokufa, na matumaini ya vizazi vijavyo.
Tanzania, taifa lenye ukanda wa bahari wa zaidi ya kilomita 1,400, lina wajibu na nafasi kubwa ya kuwa sauti ya Afrika na Afrika Mashariki katika kulinda bahari.
Ushiriki wake katika COP30 si heshima tu bali ni jukumu la kizazi cha sasa na kijacho, kama Asha anavyosema kwa tabasamu la matumaini:
“Kama tutailinda bahari leo, kesho itatulisha tena.”
0 Comments