Ticker

7/recent/ticker-posts

COP30 YATAMBUA UMUHIMU WA BAHARI KWA KILA MTU, KILA MAHALI

Mwenyekiti wa UNESCO kwa Uendelevu wa Bahari, Chuo Kikuu cha São Paulo, Alexander Turra 
NA JIMMY KIANGO

Hali ya mazingira ya bahari si nzuri duniani kote na waathirika wakuu ni nchi zinazoendelea Tanzania ikiwemo,huku jiji la Dar es Salaam likikabiliana na changamoto kubwa ya uzalishaji wa kiasi kikubwa cha taka ngumu kila mwaka.

Wastani wa tani 2000 mpaka 5000 huzalishwa kila siku, jijini Dar es Salaam, huku kiwango cha ukusanyaji unaofata utaratibu kikiwa ni kati ya asilimia 45-50 huku kile kinachosalia na kuingia kwenye mito, mabonde, mifereji na kuishia baharini kikiwa ni kati ya asilimia 50 hadi 55, sawa na tani 100–2,500.

Halii inayotokea Dar es Salaam ndio inayoyakumba majiji mengi duniani, kwa kuliona hilo, dunia imeamua kukutana Brazili ili kuujadili mustakabali wa Bahari. Ni saa nne na nusu (10:30) za asubuhi kwa saa za Brazili huku ikiwa ni saa kumi na nusu (16:30)  kwa saa za Tanzania, jopo la wataalamu  wa masuala ya mazingira ya Bahari wakiongozwa na  Mwenyekiti wa UNESCO kwa Uendelevu wa Bahari, Chuo Kikuu cha São Paulo, Alexander Turra limekutana Novemba 12, jijini Belem kunakofanyika mkutano wa COP30 kujadili mikakati ya ufadhili kwa ajili ya kukuza Sayansi inayohitajika kwa Bahari tunayoitaka.


Katika mkutano huo uliofanyika kwa saa moja ukisimamiwa na Baraza la Utafiti la São Paulo (FAPESP), ukiwa na mada kuu za Suluhisho na Ubunifu wa Baharini pamoja na Rasilimali Endelevu za Bahari, dunia imeiona hatari hiyo pamoja na kutambua umuhimu wa uhai wa bahari kwa maisha ya kila mwanadamu kila mahali.


Mkuu wa Sekretarieti ya IOCARIBE, Dkt. Lorna Innis, Mwakilishi wa Taasisi ya Utafiti ya Mabadiliko Tabianchi duniani kutoka Amerika ya Kusini,  Patrcia Suares, Mtaalamu kutoka Baraza la Kimataifa la Sayansi, Bi. Megha Sud na mwakilishi wa shirika la Fundacao Oswoldo Cruz, Paulo Gadelha kwa pamoja walikubaliana kuimarisha mikakati ya kupata ufadhili ili kukabiliana na uchafuzi wa mazingira ya bahari unaochangia kusababisha mabadiliko tabianchi.


Kikao hicho kilieleza kuwa nafasi ya bahari katika kukuza maendeleo endelevu ikiwemo uhusiano kati ya bahari na mabadiliko ya tabianchi inategemea sana misingi ya kisayansi ambayo inahitaji kuimarishwa na kupanuliwana kwamba suala hilo linahitaji mifumo endelevu na bunifu ya ufadhili iliyoandaliwa mahsusi kulingana na mahitaji mbalimbali.


Jopo hilo lilizikutanisha taasisi muhimu duniani lengo likiwa ni kushirikiana juu ya changamoto na mikakati ya kukuza sayansi inayohitajika sasa na hata baadae, ili kufanikisha kuipata bahari tunayoitaka.

HOJA 7 MUHIMU KWA AFYA YA BAHARI TANZANIA COP30

Suares,anasema Bahari ni mfumo wa uhai wa sayari yetu na chanzo cha matumaini, kwamba binadamu wataweza kuepuka janga la tabianchi na kutimiza malengo ya Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris.


Mkutano wa COP30 unawaleta pamoja viongozi wa dunia katika nyanja za sayansi ya bahari, uhandisi na sera, ili kusambaza ujumbe kwamba bahari ni muhimu kwa kila mtu, kila mahali na kwamba sayansi ndiyo inapaswa kuongoza safari yetu ya kutafuta suluhisho salama na endelevu kwa mabadiliko ya tabianchi.


Ili kufanikisha hili, yapo mambo saba ambayo yanapaswa kufungamanishwa na mazingira ya Bahari ya nchi zinazoendelea Tanzania ikiwemo na kupewa umuhimu mkubwa kwenye mkutano huo unaoendelea nchini Brazili.


Mambo hayo ni Kutambua bahari kama mdhibiti mkuu wa hali ya hewa katika mikakati ya kitaifa ya mabadiliko ya tabianchi na mifumo ya kimataifa, kuhakikisha suluhisho za tabianchi zinazotegemea bahari zinapatikana kwa urahisi, ni shirikishi na zenye haki, huku kipaumbele kikitolewa kwa mahitaji ya nchi zilizo na maendeleo duni, visiwa vidogo vinavyoendelea, na jamii za pwani zilizo mstari wa mbele.


Kuongeza kasi ya suluhisho za asili za bahari na fukwe, na kuhakikisha juhudi za uhifadhi zinaunganishwa na malengo ya kupunguza athari za tabianchi, kuhimili mabadiliko na kujenga ustahimilivu.

Kukuza teknolojia mpya za kufuatilia vitisho vya mara kwa mara na vya muda mfupi kama vile kuongezeka kwa kina cha bahari, kukithiri kwa utiririshaji wa asidi baharini, upotevu wa bayoanuwai, uchafuzi wa plastiki, uchimbaji wa rasilimali, na uchafuzi katika bahari zote.


Kujenga mifumo madhubuti ya ufuatiliaji, utoaji taarifa na uthibitishaji kwa ajili ya masuluhisho mapya ya tabianchi yanayotegemea bahari, ili kuhakikisha usalama, usahihi wa kisayansi, na ulinganifu na malengo ya kitaifa na ya kimataifa.

Kuchochea mifumo bunifu ya kifedha inayojengwa juu ya mifumo ya uwajibikaji iliyo wazi na inayoaminika, ikihusisha sekta binafsi na wahisani, ili kupanua uhifadhi wa bahari, masoko ya kaboni ya buluu, na suluhisho za bahari.


Kujitolea kufadhili ramani, ufuatiliaji na uchunguzi wa bahari katika bahari zote na kwenye miunganiko ya bahari na anga, na ardhi na bahari hasa ile inayosaidia miradi ya uhimilivu na kuimarisha uwezo wa nchi maskini na visiwa vidogo vinavyoendelea kwa kutoa taarifa sahihi na zinazoweza kutumika kwa urahisi.


Hatua hizi hazipaswi kugawanywa au kuahirishwa, zinapaswa kuunganishwa moja kwa moja katika sera zote za tabianchi na uhifadhi kuanzia tathmini za kimataifa, ahadi za kifedha, michango iliyokusudiwa kitaifa (NDCs), mifumo ya uhimilivu, hadi mikakati ya mpito wa haki huku ikipewa kipaumbele kwa wale wanaoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.


Misitu na bahari kwa pamoja inatoa suluhisho za kiasili zilizothibitishwa, zenye usawa na zinazoweza kupanuliwa zaidi. Ni kwa kuiweka bahari katikati ya mikakati ya tabianchi pekee ndipo tunaweza kujenga mustakabali thabiti, wenye usawa na endelevu kwa wote na mwaka 2025 ukumbukwe kama mwaka ambao dunia iliunganisha ardhi na bahari kulinda uhai wote duniani.

 

Post a Comment

0 Comments