Ticker

7/recent/ticker-posts

MAMBO 9 YANAYOGUSA BAHARI NA MASLAHI YA WANANCHI YANAYOPASWA KUBEBWA NA UJUMBE WA TANZANIA COP30

  

NA. JIMMY KIANGO
Bahari ina umuhimu mkubwa kwa maisha ya binadamu na ustawi wa dunia, ni msingi wa uhai, uchumi, hali ya hewa, chakula na ikolojia, hasa ikzingatiwa kuwa asilimia 50 ya oksijeni inayovutwa na binadamu duniani kote inatokana na viumbe vidogo vya baharini kama vile Phytopankton.


Phytopankton ni viumbe vidogo sana mara nyingi huonekana kwa darubini tu, vinaishi kwenye maji ya bahari na maji baridi, ambavyo hutumia mwanga wa jua, maji, na hewa ukaa (kaboni dioksidi) kutengeneza chakula (glukosi) na kutoa oksijeni kama bidhaa ya ziada, kwa kifupi Phytopankton ni injini ya uzima wa bahari na sehemu muhimu ya mfumo mzima wa dunia.

 

Aidha Bahari huzuia mabadiliko makubwa ya hali ya hewa kwa kufyonza joto na hewa ukaa kutoka angani, hii inamaanisha bila uwepo wa bahari, dunia ingetawaliwa na joto kali sana.

 

Kimsingi bahari ni maisha kwa sababu inabeba afya ya dunia na binadamu kiuchumi, hata hivyo ongezeko la shughuli za binadamu zinaiathiri bahari kutokana na kuwepo kwa uzalishaji mkubwa wa taka ngumu, huku kiwango cha ukusanyaji wake kikiwa kidogo, hali inayosababisha taka nyingi kuishia baharini.

 

Hatua hiyo husababisha athari kwenye mazingira ya bahari na kuchangia tatizo la mabadiliko tabianchi duniani kote na Tanzania ikiwemo. Mathalani baadhi ya fukwe za mwambao wa pwani ya jiji la Dare es Salaam nchini Tanzania ni miongoni mwa majiji yanayokumbana na changamoto hizo kutokana na kupokea wastani wa tani 1,000 hadi 2,500 za taka ngumu kwa siku. 

 

Ukweli wa hilo unaifanya dunia kukutana Brazili kwenye mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaoendelea kwenye jiji la Belem ili kutafuta suluhu ya kudumu ya kuiokoa bahari.

 Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) Dkt. Richard Muyungi (Picha kwa hisani ya mtandao)

Hata hivyo wadau wa mazingira wameiona haja ya kupaza sauti ili kuukumbusha ujumbe wa Tanzania uliopo Brazili kuwa unapaswa kuwa sehemu ya harakati za kuikoa bahari.

 

Ifahamike kuwa suala la ulinzi wa bahari na mazingira yake hapa nchini si la kubahatisha, ni suala lenye nguvu ya kisheria kama inavyoainishwa kwenye sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na marekebisho yake ya mwaka 2025.

Kifungu cha 54 (1,2) na kifungu cha 55(1-3) cha sheri hiyo vinatoa mamlaka kwa waziri mwenye dhamana ya Mazingira kutoa miongozo mbalimbali ya ulinzi na uhifadhi wa mto, ukingo wa mto, ziwa, mwambao wa ziwa au ufukwe kwa mujibu wa sheria.  

Aidha kifungu cha 114(1-3) cha sheria hiyo kinaelekeza wajibu wa serikali za mitaa kushiriki katika kusimamia na kupunguza kiwango cha taka ngumu kwenye maeneo yao. 

 

Baadhi ya wadau wa mazingira nchini akiwemo Dkt. Ellen Otaru ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) amesema hali ya uchafuzi wa mazingira ya bahari ni mbaya, na kwamba ni jukumu la serikali, taasisi binafsi na mtu mmoja mmoja, kuhakikisha kwa pamoja wanashiriki kikamilifu kupambana na hali hiyo na hii inamaanisha kuwa ni lazima ujumbe wa Tanzania uliopo Brazili kuhakikisha unabeba mambo mahususi na kuyasemea kwenye vikao rasmi na hata vile vya kando. 

 

Haki na Usawa wa Bahari

Dkt. Otaru anasema ipo haja ya kukuza usawa na kujenga uwezo wa kupata taarifa za bahari na rasilimali za baharini kuhakikisha kwamba watu wote wananufaika na kuchangia katika dunia yenye afya na endelevu.

 

“Kuunda sera zinazoweza kulinda jamii za pwani dhidi ya athari za mabadiliko ya mazingira, ikiwemo wale ambao watalazimika kuhama au tayari wamehamishwa na kuhakikisha maarifa ya asili yanathaminiwa na kuunganishwa katika mikakati ya uhifadhi, uhimilivu na upunguzaji wa athari za mabadiliko ya tabianchi,” ameeleza.

 

Rasilimali Endelevu za Bahari

Afya ya bahari ni msingi wa uhai wote duniani. Pia ni hazina ya rasilimali ambazo zinaweza kuwa ufunguo wa kupunguza athari za binadamu kwa mifumo ya sayari inayofanya dunia iweze kuishiwa.

Tunapaswa kuwa na mifumo inayoweza kusawazisha mahitaji ya binadamu na afya ya bahari, na hivyo kulinda afya ya dunia, kuwa na teknolojia bunifu na mbinu mpya zitakazoweza kusaidia kufuatilia, kurejesha na kusimamia kwa uendelevu matumizi ya rasilimali sambamba na uhai wa mifumo ikolojia.

 

Sauti za Bahari

Kwa upande wake Haika Lweitama ambae ni mdau wa mazingira kutoka taasisi ya Sustanable Holistic Development (SUHODE) amesema, bahari imekuwa chanzo cha msukumo kwa binadamu kwa maelfu ya miaka na pia ni kiini cha tamaduni za visiwa na jamii za pwani duniani kote. 

 

“Tunapaswa kubuni sera za bahari na suluhu za tabianchi zinazotambua na kujumuisha umuhimu wa kijamii na kitamaduni wa bahari, hasa kwa jamii za asili,” amesema.

 

Amefafanua kuwa, ubunifu wa sanaa na sayansi za kijamii unahitajika katika kuhakikisha kunajengwa jamii inayotambua, kuthamini na kulinda bahari kizazi hadi kizazi.

 

Uhai wa Bahari na Bioanuwai

Viumbe wa baharini wanabeba mzigo mkubwa wa athari za tabianchi, jambo ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa na yasiyojulikana kwa mifumo ya kijamii na sayari. Mabadiliko ya tabianchi yana maana kubwa kwa bioanuwai ya baharini na mifumo ikolojia inayounga mkono bahari yenye afya na jamii zenye ustawi.

 

Tunapaswa kubaini na kuhifadhi maeneo muhimu ya bahari hai katika mazingira ya kisiasa yanayobadilika na hali ya tabianchi inayobadilika kwa kasi.

Kutoka Msituni Hadi Baharini

 

Bahari ni injini hai inayounganisha mifumo ya nchi kavu na ya baharini kupitia mzunguko wa maji, joto, virutubishi na uhai wenyewe. Mabonde ya mito, maeneo ya pwani, mikoko, matumbawe, kina kirefu cha bahari na bahari kuu vinaunganisha mifumo ya sayari kwa njia zinazowezesha dunia kuishi, lakini sasa viko chini ya shinikizo kubwa. 

 

Hivyo tunalo jukumu la kuelewa na kusimamia vyema uhusiano huu ili kukabili changamoto tatu kuu za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, na upotevu wa bioanuwai na kuangalia  zana na mifumo ipi inayoweza kuunganisha ardhi na bahari, sayansi na sera, maarifa ya kienyeji na hatua za kimataifa.

 

Bahari, Kaboni na Tabianchi

Bahari inaweza kuwa chanzo cha suluhisho katika kukabiliana na mustakabali usio na uhakika. Tunapaswa kuangalia ni nafasi gani bahari inaweza au inapaswa kuchukua katika mikakati ya kupunguza athari za tabianchi kama vile uondoaji na uhifadhi wa dioksidi kaboni ya baharinina pia kujua ni hatua gani zinahitajika kuchukuliwa ili kufuatilia na kudhibiti bajeti ya kaboni ya bahari ili kuepuka madhara yasiyokusudiwa na kulinda huduma za mifumo ikolojia zilizopo.

 

Uchumi wa Bluu na Fedha

Meneja wa Program ya Ustahimilivu wa Pwani na Bahari kutoka taasisi ya kimataifa inayojihusisha na ulinzi wa rasilimali asili (International Union for Conservation of Nature-Tanzania) Joseph Olila anasema uchumi wa bluu ni mojawapo ya sekta za kiuchumi zinazokua kwa kasi duniani, zenye uwezo wa kusaidia kuboresha maisha na afya ya bahari kwa pamoja.

 

Tanzania tunapaswa kujua kama mifumo ya kifedha inaweza kuundwa na kutekelezwa vipi ili kusaidia miradi endelevu ya uchumi wa bluu inayolenga mahitaji ya ndani na kitaifa, huku ikizingatia changamoto za hasara na uharibifu na ni sera zipi zitakazohamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika teknolojia na viwanda rafiki kwa bahari huku zikihakikisha ushirikishwaji wa jamii na wadau.

 

Uhimilivu na Urekebishaji wa Uchumi wa Bluu

Kujenga uhimilivu wa jamii na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya bahari ni muhimu ili kulinda jamii za pwani, kuhakikisha afya ya mifumo ya baharini, na kutekeleza mipango ya kitaifa ya urekebishaji. 

 

Mamlaka zinapaswa kuangalia ni suluhisho zipi bora na sahihi za kiasili zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya sasa na yanayotarajiwa, ni mapengo gani ya maarifa yanayopaswa kujazwa ili kuhakikisha watu, jamii, na mataifa yako tayari zaidi kukabiliana na mabadiliko katika ngazi ya kimataifa na kikanda.

 

Suluhisho na Ubunifu wa Bahari

Mshauri kutoka shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) -Tanzania, wanaoratibu mradi wa Pwani Yetu, Dkt. Robert Katikiro ameweka wazi kuwa: Teknolojia bunifu na mbinu mpya zinaweza kutumia uwezo wa bahari kukabiliana na changamoto za dunia na kukuza uendelevu na maendeleo ya kiuchumi, kuna haja ya kuangalia ni teknolojia zipi mpya na maarifa ya kitamaduni yanayotoa fursa kubwa zaidi kwa usimamizi endelevu wa rasilimali za baharini.

 

Ushirikiano wa taaluma mbalimbali unaweza kuendeleza vipi ubunifu katika suluhu za baharini zinazokabiliana na changamoto za kijamii na kimazingira, huku zikisaidia mataifa kutimiza michango yao iliyodhamiriwa kitaifa na kutekeleza vipengele vya baharini vya mipango yao ya urekebishaji.

 


Post a Comment

0 Comments