| Mwenyekiti wa Kikundi cha Majadiliano cha Afrika (AGN) Dk. Richard Muyungi (picha kwa hisani ya mtandao) |
Hatimae mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofanyika kwenye jiji la Belem nchini Brazili umeibua tumaini jipya kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, baada ya kutakiwa kuwasilisha mapendekezo ya kupata msaada wa kifedha kutoka kwenye Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu (FRLD).
Mfuko wa FRLD ulianzishwa rasmi mwaka 2022 kwenye mkutano wa COP27, uliofanyika nchini Misri, hata hivyo tangu kuanzishwa kwake haukuwahi kukaribisha mapendekezo kama ilivyofanya sasa. Uamuazi huo ni hatua muhimu kwa mataifa yanayokabiliana na kupanda kwa kina cha bahari, ukame, mafuriko na madhara mengine yaliyosababishwa na mabadiliko tabianchi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi waathirika wakubwa wa mabadiliko tabianchi, na athari zake zinaonekana wazi wazi hasa kwenye eneo la bahari na pwani, ambapo kiwango cha uvuaji wa samaki kimepungua, joto limeongezeka na kina cha bahari kimepanda, huku moja ya sababu ikitajwa kuwa ni kukithiri kwa taka ngumu ndani na nje ya bahari.
Uamuzi huo utazisaidia nchi kuwa na fursa ya kuwasilisha mapendekezo yao kuanzia mwezi ujao (Desemba 2025) hadi katikati ya Juni 2026, huku idhini za kwanza za ufadhili zikitarajiwa kuanza Julai 2026.
Kwa mujibu wa bodi ya mfuko huo, kiasi cha awali cha dola milioni 250 za Marekani (takriban shilingi bilioni 625) kimetengwa kusaidia miradi inayolenga kushughulikia aina mbalimbali za hasara zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi kuanzia uharibifu wa miundombinu na jamii zilizohamishwa hadi uharibifu wa urithi wa kitamaduni.
Mwenyekiti Mwenza wa FRLD, Jean-Christophe Donnellier, alisema wito wa kwanza wa mapendekezo utasaidia kujaribu, kujifunza na kuboresha mfumo wa uendeshaji wa muda mrefu wa mfuko huo. Alisema tangazo hilo ni "ishara muhimu kwa nchi zinazoendelea sasa msaada sasa unapatikana."
Mwenyekiti wa Kundi la Nchi Masikini Zaidi (LDC Group), Evans Njewa, alisema hatua hiyo ni mwanzo wa kuelekea kupata haki ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na jamii zinazokabiliwa na athari za moja kwa moja za mabadiliko ya tabianchi.
"Mfuko unapaswa kutoa msaada wa haraka, kwa urahisi na unaopatikana kwa masharti ya haki na rahisi kwa nchi zinazokabiliwa na uhalisia mgumu wa mabadiliko tabianchi."
WATAALAMU WAWAPATA HOFURipoti iliyopewa jina Mfuko wa Hasara na Uharibifu Unaofanya Kazi, iliyotolewa na Kikundi Huru cha Wataalamu Wakuu wa Fedha za Tabianchi, inakadiria kuwa ifikapo mwaka 2030, nchi zinazoendelea zitahitaji kati ya dola bilioni 200 hadi 400 kila mwaka kushughulikia hasara na uharibifu.
Kwa kulinganisha, nchi wafadhili zimeahidi dola milioni 788 pekee, ambapo zaidi ya dola milioni 560 ndizo zilizothibitishwa rasmi, na chini ya dola milioni 400 ndizo zilizotolewa hadi sasa.
MATARAJIO YA AFRIKA
Mwenyekiti wa Kikundi cha Majadiliano cha Afrika (AGN) Dk. Richard Muyungi, alieleza matarajio matatu makuu kutoka kwa bara la Afrika kuwa ni kuwa na rasilimali za kutosha na za uhakika ili kuhakikisha mfuko huo unaweza kukidhi mahitaji ya muda mrefu ya uokoaji, umuhimu wa uratibu wa kitaasisi kati ya FRLD, Mtandao wa Santiago, na Utaratibu wa Kimataifa wa Warsaw ili kuepuka kurudiwarudiwa kwa kazi na kuongeza ufanisi wa ushirikiano.
Tarajio la mwisho ni haja ya upatikanaji sawa na ushirikishwaji, akihimiza taratibu rahisi na msaada wa kiufundi kwa nchi masikini ambazo zinapata ugumu katika kushughulikia mifumo tata ya fedha za kimataifa.
"Uhalisia wa chombo hiki kipya utategemea jinsi kilivyo rahisi kupatikana kwa wale walio mstari wa mbele,rasilimali lazima zifikie kwa haraka, moja kwa moja, na kwa uwazi kwa nchi zilizoathirika. Kundi la Afrika liko tayari kushirikiana kwa ujenzi ili mfuko huo uwe mkombozi kwa mamilioni ya watu,”amesema Dkt. Muyungi.
| Mratibu Mkuu wa Vijana na Jinsia ndani ya AGN, Sarah Pima |
PESA ILIYOTENGWA HAITOSHI
Ili kufanikisha nia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, baadhi ya wanaharakati wa mazingira ambao wanashiriki mkutano wa COP30, wameweka wazi kuwa fedha iliyotengwa haitoshi, hata hivyo walitoa wito kwa serikali na wadau wa mazingira kuhakikisha wanaongeza ujasiri katika kuifanya kazi hiyo hata kama mgao unaotolewa na wafadhili ni mdogo.
Mkurugenzi wa Hudefo na Mratibu Mkuu wa Vijana na Jinsia ndani ya AGN, Sarah Pima, alisema rasilimali zilizopo kwa sasa ni sehemu ndogo sana ya mahitaji halisi hasa ikizingatiwa kuwa majanga ya tabianchi yanaendelea kuharibu mataifa yaliyo hatarini.
Alitoa mfano wa Kimbunga Melissa, kilichosababisha hasara na uharibifu wa takriban dola bilioni 7 nchini Jamaica na Ufilipino.
Mkurugenzi Mtendaji wa FRLD Ibrahima Cheikh Diong, alikiri kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa rasilimali, lakini akaahidi kuwa mfuko utaendelea kuhamasisha ufadhili zaidi ili kufanikisha malengo ya muda mrefu.
UHALISIA WAMAHITAJI
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea ambazo zimeliweka suala la hasara na uharibifu kama kipaumbele katika Mchango Wao Uliodhamiriwa Kitaifa (NDCs), na mipango ya kitaifa ya hatua za tabianchi iliwasilishwa Umoja wa Mataifa kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa COP30.
Uamuzi huo ulikuja kutokana na ukweli kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi zilizo hatarini zaidi kutokana na ukame, mafuriko na kupanda kwa kina cha bahari, imeeleza katika NDC yake ya mwaka 2021 kwamba athari za mara kwa mara za tabianchi zinaathiri mafanikio ya maendeleo na kuongeza gharama za uokoaji.
Ingawa NDC hiyo haijataja moja kwa moja hasara na uharibifu kama kipaumbele cha pekee, imeainisha sekta kama usimamizi wa fukwe, kilimo na upunguzaji wa hatari za majanga kama maeneo ambayo athari za tabianchi tayari zimevuka mipaka ya urekebishaji.
Mfuko mpya wa FRLD unatoa fursa muhimu kwa Tanzania kutafuta msaada mahsusi wa kujenga upya maisha, kurejesha miundombinu iliyoharibiwa, na kulinda jamii zilizo hatarini.
0 Comments