Baadhi ya wanawake wanaounda kikundi cha Mazingira, Mang'ula B, Mkoani Morogoro ambao wanashiriki ulinzi wa Hifadhi za misitu kwa kutengeneza mkaa mbadala unaopunguza uwezekano wa ukataji miti kwa ajili ya kuni.
NA JIMMY KIANGO-IFAKARA-MOROGORO
Halikuwa jambo rahisi kumuona mwanamke akiwa mstari wa mbele katika ushiriki wa utunzaji wa misitu na mazingira kwa ujumla. Kwa miaka mingi wanawake wamekuwa aidha wakitengwa ama kujitenga katika kushiriki kwenye baadhi ya shughuli za kuleta maendeleo hasa zile zenye kuhitaji matumizi nguvu.
Hali hiyo imechangia wanawake wengi hasa waliopo kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi ama mapori ya akiba kujiona hawastahili kuwa walinzi wa maliasili hizo. Ikumbukwe kuwa akina mama wengi hasa wa vijijini hutazamwa kama washiriki wakuu wa ukataji miti kwa ajili ya kujipatia kuni.
Hali sasa ni tofauti kabisa, wanawake wengi ndio wamekuwa vinara wa uhifadhi wa mazingira na shoroba za wanyamapori wilayani Kilombero, mkoani Morogoro. Inaelezwa kuwa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa nafasi wanawake kushiriki kwenye utunzaji wa mazingira na maliasili kwa ujumla.
Wanawake sasa wamekuwa mstari wa mbele kwenye usimamizi wa maliasili mbalimbali zikiwemo shoroba ambazo zimo ndani ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili. Lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha unaiongezea jamii uelewa katika kulinda shoroba ili ziendelee kuwa salama na kuwapa fursa wanyama pori kuhama kutoka eneo moja kwenda jengine kwa kupita kwenye njia zao za asili.
Meneja wa miradi wa Taasisi ya Reforest Africa, iliyopo Kilombero mkoani Morogoro, Lasima Nzao. |
Meneja wa miradi wa Taasisi wa Reforest Africa, iliyopo Kilombero mkoani Morogoro, Lasima Nzao anasema moja ya watu wanaoshiriki kwa kiasi kikubwa katika urejeshaji wa misitu ni wanawake na vijana.
“Suala la jinsia tunalizingatia sana, na moja ya mambo yanayotufurahisha ni ushiriki wa akina mama na vijana katika kufanikisha kazi zetu.
“Wanashiriki kwenye kutafuta mbegu, kuotesha vitalu na hata kuotesha miti. Tunafurahia hatua hii maana wanawake ni walezi wazuri wa mazingira.
“Kundi hili la akina mama na vijana likishiriki moja kwa moja, tegemea matokeo makubwa kwenye kazi mnayoifanya,”alisema.
Nzao alisema uwepo wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umekuwa na tija kubwa kwenye shoroba ya Nyerere Selous-Udzungwa, ambapo mradi huo umewezesha shughuli mbalimbali za kuongoa misitu na kufanya urejeshaji wenye tija.
Nzao anaweka wazi kuwa pamoja na kupanda miti zaidi ya 15,000 kwenye shoroba ya Nyerere Selous, lakini pia wamekuwa wakiusimamia na kuutunza msitu wa Magombera na msaada mkubwa wa kufanikisha shughuli hiyo umekuwa ukitolewa na USAID kupitia mradi wake wa Tuhifadhi Maliasili.
“USAID imekuwa ikisaidia kwenye uoteshaji wa miti kwenye shoroba, ukusanyaji wa mbegu, uoteshaji wa vitalu, usimamizi na uangalizi wa shoroba.”
Kwa upande wake Afisa Mahusiano ya Jamii wa mradi kutoka Reforest Africa, Peter Nyiti, amesema akina mama na vijana wa vijiji vya Sore, Kanyanja na Mang’ula A, ambavyo vimepitiwa na shoroba ya Nyerere Selous-Udzungwa wamekuwa wakirahisisha kazi ya taasisi hiyo kutokana na kushiriki kwao moja kwa moja kwenye majukumu yote muhimu.
“Akina mama na vijana wana msaada mkubwa katika kuhifadhi shoroba kwenye vijiji hivyo ambavyo vinatekeleza mradi wa kulinda na kutunza shoroba kwa ufadhili mkubwa wa USAID.
“Tunaishirikisha jamii katika maeneo hayo kwa kuwapa kazi mbalimbali za muda mfupi na hata zile za muda mrefu maana wapo ambao tumewaajiri, USAID wametujengea uwezo wa kutekeleza majukumu yetu vizuri.”
Amesema katika watu 150 waliopewa elimu ya utunzaji wa misitu na shoroba, wanawake ni 76 na hata kwenye vikao mbalimbali vya masuala ya uhifadhi wao ndio wamekuwa wakijitokeza kwa wingi.
Peter Nyiti
ELIMU YA UTUNZANI MAZINGIRA SHULE YA MSINGI
Katika kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linakuwa endelevu, Reforest imeandaa kitabu maalum cha kufundishia uongoaji wa misitu, ambapo walengwa wakuu ni wanafunzi wa darasa la tano na sita na walimu wa shule za msingi zilizopo katika vijiji vilivyopitiwa na shoroba ya Nyerere Selous-Udzungwa.
Nyiti amesema elimu hiyo ikiwaingia wanafunzi wa shule za msingi itakuwa imesaidia kuzalisha vizazi vinavyoweza kujua umuhimu wa utuzaji wa misitu tangu wakiwa wadogo.
“Hitaji letu ni kuhakikisha mradi huu haufi hata pale wafadhili wetu USAID watakupomaliza mradi wa Tuhifadhi Maliasili na kundi pekee la kulifanikisha hili ni wanawake na vijana waliopo mashuleni kwa sasa,”alisema Nyiti.
Nyiti aliongeza kuwa kwa sasa wanaishirikisha jamii kuotesha miti ya asili na wanafanyia kazi aina 27 za miti ya asili.
CHANGAMOTO
Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo katika kufanikisha kazi ya urejeshaji wa misitu, Nzao alisema mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi na kusababisha mafuriko.
“Mvua zimeturudisha nyuma sana, maana maeneo yote tunayoyafanyia kazi yalijaa maji, hayakuwa yakiingilika na hatukuweza kufanya shughuli yoyote ya kuokota mbegu, kuotesha vitalu na hata kuotesha miti yenyewe.
“Eneo kubwa tunalilosimamia ni bonde hivyo mvua ikinyesha maji yanatuama kwa muda mrefu.”
Aidha alisema changamoto nyengine ni wanyama kula miti midogo ambayo wameshaotesha, lakini pia kumekuwa na uvamizi wa ardhi kwenye baadhi ya maeneo, hata hivyo masuala hayo yamekuwa yakishughulikiwa na serikali za vijiji husika.
Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa katika shoroba za Kwakuchinja, Amani Nilo, Udzungwa na Hifadhi ya Nyerere, Ruaha Rungwa na Katavi, Ruaha Rungwa na Inyonga na Kigosi Moyowosi- Burigi Chato umezingatia usawa wa kijinsia ambao umesaidia makundi yote kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Mkurugenzi wa JET, John Chikomo (kulia) akimkabidhi Nzao, gazeti la KASUKU ambalo linatolewa na JET.
Ufuatiliaji na tathmini ambayo imefanywa na watalaamu wa mradi huo wameona kuwepo kwa ushirikishwaji wa makundi yote wakiwemo wanawake, vijana, watoto na walemavu inasababisha rasilimali zote zinazopatikana kwenye hifadhi kuwa salama na kila mwana jamii kujiona ni mnufaika.
Ili fursa zinazopatikana kwenye uhifadhi ziwe endelevu ni lazima ushirikishwaji wa kijinsia uzingatiwe, hatua hiyo inasaidia hifadhi kutunzwa na kuwa endelevu.
Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unashirikiana na wananchi waliopo karibu na shoroba ili kuhakikisha wananufaika na fursa zilizopo, ikiwemo kuanzisha vikoba, ujasiriamali na kupata tija nyengine.
Taarifa za kitafiti zinaonesha wanawake na vijana ndio waathirika wakuu wa uharibifu wa mazingira, hivyo uamuzi wa kuzingatia usawa wa kijinsia utawanufaisha zaidi.
0 Comments