Moja ya mikutano ya vijiji
NA JIMMY KIANGO-MOROGORO
Haikuwa kawaida kwa mwananchi kujiona anayo kila sababu ya kushiriki masuala ya uhifadhi wa misitu, wanyamapori na maliasili za nchi. Mwananchi alijitoa kwenye dhamana hiyo kwa sababu hakuwa akijiona kuwa ni mnufaika wa moja kwa moja wa rasilimali hizo.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi hasa wanaoishi pembezoni mwa hifadhi kuwa ndio washirika wakuu wa ujangili na uhalifu mwengine wa wanyamapori na maliasili za misitu.
Hali sasa ni tofauti, uwepo wadau wa maendeleo kama vile Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa kushirikiana na taasisi za ndani wamefanikisha kupunguza kabisa dhana ovu kuwa mwananchi hahusiki na ulinzi wa maliasili za misitu.
Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili ambao unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) na taasisi nyengine ikiwemo Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa misitu Tanzania (MJUMITA), umefanikisha suala la uhifadhi kuwa agenda ya kudumu kwenye vijiji vilivyopo wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Afisa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili-MJUMITA, Kelvin Shirima, akizungumza na Waandishi wa Habari za Mazingira, hawapo pichani. |
Afisa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili-MJUMITA, Kelvin Shirima, amesema kuwa kwa kiasi kikubwa wamefanikisha suala la uhifadhi kuwa agenda ya kudumu kwenye mikutano ya vijiji, tofauti na ilivyokuwa awali.
Shirima anasema MJUMITA imekuwa ikifanya kazi na vikundi vyote vinavyojihusisha na masuala ya mazingira kwenye mitandao 129 iliyopo katika Kanda sita, Mikoa 14, Wilaya 32 na vijiji zaidi ya 452.
“Tumekuwa tukishirikiana na vikundi kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya misitu, lengo letu ni kuhakikisha jamii inaujua umuhimu na thamani ya kulinda na kunufaika na maliasili zilizopo kwenye maeneo yao hasa misitu na wanyamapori,” alisema Shirima.
Amesema MJUMITA pia wanaliangalia suala la utawala bora kwenye ngazi za vijiji wanavyofanya navyo kazi na kuangalia utekelezaji wa mradi wa urejeshaji wa shoroba ya Nyerere Selous-Udzungwa kwa kushirikiana na taasisi za Mazingira zilizopo wilayani Kilombero.
“Tunafanya ufuatiliaji wa masuala mbalimbali kwenye jamii kwa kutumia mfumo wa Pima kadi hasa katika vijiji vya Sole, Mang’ula A na Kanyenja.
“Utendaji wetu unajumuisha jamii kwa kukusanya makundi mbalimbali ya kijamii na tunawapa jukumu la kuangalia uwajibikaji wa viongozi kwa kutumia mfumo unajulikana kama Social Accountability Monitaring (SAM).”
MJUMITA imefanikiwa kutoa mafunzo ya ufuatiliaji huo kwa zaidi ya watu 50 wa vijiji vya Mang’ula A na Msolise.
“Hawa tunaowapa mafunzo ya ufuatiliaji na wao wanafuatiliwa kwa kuwapa fomu ambazo zina alama za ubora, kuanzia alama moja mpaka tano, ambapo mfuatiliaji akipata alama za chini mara kwa mara anakosa sifa ya kuendelea na kazi hiyo.”
Kwa upande wake Benedict Minja kutoka MJUMITA, alisema moja ya mambo yanayowafurahisha ni kuona vijiji vinaipa thamani agenda ya uhifadhi jambo ambalo linaongeza kasi na ubora wa kulinda hifadhi.
Salum Mnanga ambae ni mkazi wa Kijiji cha Mang’ula A, ameiambia AFRINEWS SWAHILI kuwa elimu inayotolewa mara kwa mara na MJUMITA imewasaidia kufaidika na rasilimali za misitu na kwamba sasa wanavijiji wengi wanashiriki ulinzi na utuzaji wa rasilimali hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa JET, John Chikomo aliipongeza MJUMITA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwenye ulinzi wa maliasili za misitu kwa kushirikisha jamii zilizopo pembezoni mwa hifadhi.
0 Comments