Ticker

7/recent/ticker-posts

MATUMIZI BORA YA ARDHI KUMALIZA MIGONGANO BAINA YA BINADAMU NA WANYAMAPORI

  

Afisa Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. Stephen Nindi akitoa maelezo ya namna serikali ilivyoshiriki katika kukabiliana na Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori katika ukanda wa Ruvuma.

NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI -DSM

 

Ni jambo la kawaida kusikia taarifa kuwa tembo wamevamia makazi ya watu na watoa taarifa ziko nyakati kwa kujua ama kutokujua hujikuta wakikoleza chumvi kwa kudai kuwa kundi la tembo 400 wamevamia Kijiji.

 

Ukweli ni kwamba tembo 400 hawawezi kuvamia Kijiji kimoja na hicho Kijiji kikabaki salama, lakini pia wanyama hao inaelezwa na wataalamu kuwa wana kawaida ya kurithishana maeneo miaka kwa miaka hivyo huwa hawavamii makazi ya binadamu badala yake shughuli za kibinadamu ndio hufanyika kwenye njia zao.

 

Kwa kuliona hilo Serikali ya Tanzania imeamua kuendesha mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yaliyopakana na hifadhi na ukanda wa Ruvuma ni miongoni mwa maeneo yaliyofikiwa na mpango huo.

 

Lengo kuu la mpango huo ni kuondoa kabisa migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori, ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ni tatizo kwa baadhi ya maeneo kwenye ukanda huo wa Ruvuma.

 

Akieleza jitihada zilizofanywa na serikali katika kuondoa migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori, Afisa Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. Stephen Nindi ameweka wazi kuwa mpango wa kuipanga ardhi utasaidia kukabiliana na migangono hiyo.

 


Dkt. Nindi aliyesema hayo kwenye mdahalo ulioandaliwa na  Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migongano Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani kwa ufadhili wa (BMZ).

 

Mdahalo huo uliofanyika leo Mei 6,2024 kwenye Hoteli ya Colosseum, jijini Dar es Salaam ulilenga kuwapa nafasi wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuileza jamii kile ambacho serikali kwa kushirikiana na wadau wake wamefanikiwa kukifanya katika kukabiliana na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori kwenye ukanda wa Ruvuma. 

 

Dkt. Nindi amesema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika kukabiliana na migongano hiyo na miongoni mwao ni kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi.

 

“Ikitokea maeneo yote yakawekwa kwenye mpango wa matumizi bora ya Ardhi, hii migongano baina ya Binadamu na Wanyama itapungua ama kwisha kabisa.

 

“Shoroba za wanyamapori , maeneo ya uvuvi wa mabwawa, sehemu za kulishia mifugo na maeneo ya kilimo yote yatatengwa kwa utaratibu utakaokuwa na faida kwa pande zote.”

 

“Serikali imeshaanza kulifanya hilo na mpango wa matumizi bora ya ardhi umeanzia ngazi ya taifa na umeshuka mpaka kwenye ngazi ya wilaya, hii inatoa nafasi kwa wadau wengi zaidi kushriki katika kuutekeleza mpango huu, maana mpango uliopo ngazi ya chini unakuwa umebeba taarifa nyingi zaidi ambazo zinarahisisha utekelezaji wake.”

 


Alisema kama tembo na wanyamapori wengine wakitengewa njia zao, haitakuwa rahisi kwao kuingia kwenye maeneo ya binadamu iwe ya mashamba au makazi, kama ambavyo binadamu wakizijua shoroba za wanyamapori hawataweza kuziharibu kwa kufanya shughuli zao humo.

 

Mdahalo huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ).

 

Kwa upande wake Meneja Mtekelezaji wa Mradi huo kutoka GIZ, Cristina Georgii, alisema wanafurahia kutekeleza mradi huo, ambapo ameahidi shirika hilo kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

 

“Tunafurahia kutekeleza mradi huu wa Kupunguza Migongano Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, tunaamini hatua hii itasaidia kufanya binadamu kuishi kwa amani na wanyamapori, GIZ tutaendelea kushirikiana na serikali na wadau wetu kama tunavyofanya kwa JET,”alisema.

 

Kimsingi ongezeko la shughuli za kibidamu hasa kilimo na ufugaji vinatajwa kuwa chanzo kikuu cha migongano baina ya binadamu na wanyamapori na kwamba suala hilo limekuwa ni changamoto kwenye baadhi ya maeneo nchini.

 

Meneja Mtekelezaji wa Mradi huo kutoka GIZ, Cristina Georgii


Takwimu za TAWA za wanyamapori kuingia kwenye makazi na mashamba ya binadamu kwa mwaka 2016/17 zinaonesha kuwa kulikuwa na matukio 833 na mwaka 2027/18 kulikuwa na ongezeko la matukio 164 huku mwaka 2018/19 yalifikia matukio 1510, mwaka 2019/20 matukio hayo yalipungua kutoka 1510 hadi 1426.

 

Kupungua huko kulichangiwa na uzuri wa hali ya hewa iliyochangia kupatikana kwa malisho ya kutosha kwenye maeneo yao.

 

Hata hivyo mwaka 2020/21 hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi kwani matukio 1706 yaliripotiwa na kuanzia hapo hali iliendelea kuwa mbaya zaidi kwani mwaka 2021/22 yaliripotiwa matukio 2304 na mwaka 2022/23 yalifikia matukio 2817.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 23.76 kwa mwaka na uharibifu wa mazao ukiwa ni ongezeko la wastani wa asilimia 118..1 kwa mwaka.   

 

Kwa mujibu wa takwimu hizo za TAWA, ni wazi mwaka 2018 kulikuwa na ongezeko kubwa la matukio ya migongano, ongezeko liliifanya Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa Mkakati wa Taifa wa kusimamia migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020-2024.

 

Mkakati huo ulizinduliwa Oktoba 5,2020 na hadi sasa unatekelezwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa -TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro -NCAA, TAWA, Wakala wa Misitu Tanzania -TFS, TAWIRI  na wadau wengine wa masuala ya uhifadhi.

 

Ukubwa wa tatizo hilo unazigusa wilaya 44 ambazo zinakabiliwa na changamoto ya wanyamapori kurejea kwenye njia zao za awali hatua inayoonekana ni kama wanavamia maeneo ya watu na kusababisha uharibifu wa mazao, kujeruhi na wakati mwengine kusababisha vifo kwa binadamu.

 

Hatua hiyo haiwaathiri binadamu pekee, kwani hata wanyama nao wanaathirika kwa kujeruhiwa na wakati mwengine kuuawa na binadamu.

 

Busega, Kilosa, Meatu, Nachingwea, Rufiji, Lindi, Manyoni, Itilima, Tunduru na Bunda ndiyo maeneo yanayotajwa kuwa na tatizo hilo huku tembo akitajwa kuongoza kwa asilimia 80 kuwa na matukio ya kurejea kwenye njia zake na kuingia kwenye makazi ya watu, simba, fisi na nyani wanabeba asilimia 20 ya matukio yote.

 

Moja ya njia zinazotajwa kuwa sehemu ya kusaka suluhu ya mgongano huo ni kuwepo kwa matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yote yaliyozunguka hifadhi na mapori ya akiba kama alivyosema Dkt. Nindi.

 

 

Post a Comment

0 Comments